Software: Apache/2.2.16 (Debian). PHP/5.3.3-7+squeeze19 uname -a: Linux mail.tri-specialutilitydistrict.com 2.6.32-5-amd64 #1 SMP Tue May 13 16:34:35 UTC uid=33(www-data) gid=33(www-data) groups=33(www-data) Safe-mode: OFF (not secure) /usr/share/dasher/ drwxr-xr-x |
Viewing file: Select action/file-type: Makampuni ya kuchapisha vitabu hayakusita kuchapisha kitabu baada ya ithibati ya kamati kupatikana, kwa sababu hiyo ilikuwa thibitisho kwamba kitabu hicho kitatumiwa katika shule za serikali na zile zenye kupata ruzuku ya serikali. Ithibati ilionyesha kwamba kitabu kitapata wanunuzi, jambo ambalo lilisaidia kupunguza gharama ya kuchapisha vitabu vya Kiswahili ambavyo havikuwa, na hadi sasa havina, wasomaji wengi nje ya shule. Waandishi walipata moyo wa kuandika walipojua kwamba vitabu vyao vitatumiwa kote katika Afrika Mashariki. Vitabu viliuzwa kwa wingi. Kwa mfano, vitabu vinne vya Ronald Snoxall viliuzwa takriban nakala 1,000,000. l6* Nguvu za ithibati hazikuishia Afrika Mashariki tu. Uwezo wa ithibati wa Kamati ulikuwa ukiheshimiwa kote ulimwenguni, kama asemavyo Ratcliffe: "Wachapishaji wa Ulaya, Marekani na sehemu zingine za ulimwengu wamekuwa wakitegemea ithibati iliyotolewa na kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kwa miswada waliopelekewa na waandishi binafsi, Waafrika na Wazungu ili kuwasomea na kuwasahihishia." (Ratcliffe, ILC Bulletin Na 21, 1951: 3). Ili kuwatia moyo Waafrika waweze kuandika kusudi watosheleze mahitaji ya vitabu vya fasihi, Kamati ilianzisha mashindano ya kuandika insha mnamo 1935. Ili kuwapa motisha ya kuendeleza vipawa vilivyo- gunduliwa katika mashindano ya insha, mashindano ya uandishi yalianzi- shwa katika mwaka wa 1939. Kutokana na mashindano hayo miswada mingi ilipelekewa Kamati. Mashindano hayo yalianza kuwashirikisha washindani Wazungu katika mwaka 1942 ili kukuza uandishi wa Kiswahili miongoni mwa watawala wa siku za baadaye. (Ratcliffe 1942: 9). Kwa hivyo, kamati ilikuwa ikitekeleza malengo iliyokusudiwa. Ilikuwa ikichapisha vitabu vya Kiswahili sanifu ili iwashawishi waandishi wapya, na ilihakikisha kwamba vitabu vilikuwa vikitafsiriwa kwa Kiswahili. Kamusi ya Kiswahili-Kiswahili ilichapishwa mnamo 1935 hali kamusi ya Kiswahili-Kiingereza na ya Kiingereza-Kiswahili zilichapishwa -- 16* Mahojiano ya mwandishi na R. A. Snoxall Februari 10, 1984. Vitabu hivyo ni: Elimu ya Kiswahili Kitabu cha Kwanza. Kitabu cha Pili na Kitabu cha Tatu vilivyoandikwa na E. G. Morris na R. A. Snoxall; na Kitabu cha Nne kilichoandikwa na R. A. Snoxall na E. A. Ibreck vilivyochapishwa na Longman (hadi 1959.) 28 mwaka 1939. Kamati iliendelea kujibu maswali ya umma kuhusu maneno mapya, asili ya maneno, maneno yaliyoazimwa n.k., na maneno yaliyo- kubaliwa yalichapishwa katika jarida la l.L.C. Bulletin. Hapo awali nakala za l.L.C. Bulletin zilikuwa zikitolewa bure kwa wale waliokuwa wakipenda. Baadhi ya vitabu vya sayansi vilikuwa vimetafsiriwa kwa Kiswahili. 17* Vitabu hivyo vilikuwa msingi bora ambao ungetumiwa kuanzisha utafiti wa masomo ya Kiswahili na uchapishaji. 2.2 Othografia Katika utangulizi wa kitabu kinachoitwa A Handbook of the Swahili Language, Askofu Steere alijadali suala la tahajia au hati za maandishi ya Kiswahili, kwa undani. Karibu maandishi yote ya Kiswahili kabla ya wakati wake yalikuwa yameandikwa kwa hati za Kiarabu. Mengi kati ya maandishi hayo yalikuwa ni tenzi na mashairi ya kidini na mambo ya kawaida yaliyoandikwa kwa lahaja ya kishairi ya Kaskazini ambayo Steere alishuku iwapo ilieleweka na watu wengi. Ingawa Kiswahili cha wakati wake kilikuwa kikitumiwa katika kuandikiana barua, Steere anasema kwamba barua kama hizo zilianzia na salamu kwa Kiarabu na pia maneno na vifungu vya maneno ya Kiarabu vilikuwa vikichanganywa na Kiswahili. Steere alitambua kwamba hati za Kiarabu hazifai kuandikia Kiswahili kwa sababu lugha ya Kiswahili inazo irabu tano ikilinganishwa na irabu tatu za Kiarabu. Kuhusu konsonati, hati za Kiarabu zinao upungufu wa konsonanti cha, g, p, na v. Steere aliandika hivi: "Kwa hivyo, Waswahili wanalazimika kuandika ba, f, au p waki- kusudia kuandika mb au b; wanaandika ghain badala ya g, ng, ng'; fa badala ya v, mv na f; ya badala ya ny na y; shin badala ya ch na sh; pia wanaiwacha n inapozitangulia d, j, y na z." (Steere 1870: 5) Kwa hivyo, ni wazi kwamba hati za Kiarabu hazifai na hazitoshelezi maandishi ya Kiswahili kwa sababu ya kutatanisha. Ili kuonyesha matatizo ya hati hizi, Steere anaandika hivi: "Nilipokuwa Zanzibar, kulikuwa na barua iliyotoka Kilwa kuhusu vita. Barua ilitaja kwamba mtu mmoja kati ya wale waliopigana -- 17* Baadhi ya vitabu hivyo ni Mafunzo Katika Hygiene ya Kuwafunza Watu wa Afrika ya Mashariki, London 1924; Stronomia - Elimu ya Dunia na Jua na Mwezi na Nyota, UMCA Zanzibar 1901; Jiolojia, UMCA Zanzibar 1901; Lojiki - Mlango wa Filosofia 1, UMCA Zanzibar 1901 na Mlango wa Filosofia 2, UMCA Zanzibar 1901. 29 alikuwa amekufa au amevuka na hakuna aliyeweza kusema kile kilichokuwa kimetendeka. Konsonanti mbili za mwisho zilikuwa fa na gaf zikiwa na vitone vitatu juu yake. Ikiwa vitone viwili vilikuwa vya herufi ya kwanza, mtu huyo alikuwa amekufa. Ikiwa vitone viwili vilikuwa vya herufi ya pili alikuwa hai, lakini vitone hivyo vilikuwa katikati hivi kwamba hakuna aliyeweza kuvigawanya. Iwapo Kiarabu kingekuwa na herufi v ingekuwa wazi." (Steere 1870: 6). Zikilinganishwa na hati za Kiarabu, hati za Kirumi hazileti matatizo yoyote katika kuandika Kiswahili. Sababu yake ni kwamba wasomi wengi wa Kiswahili waliokuja baada ya Krapf na Steere waliamua kutumia hati za Kirumi walizokuwa wamezizoea badala ya hati za Kiarabu zilizokuwa zikitumika kuandika Kiswahili. Maneno na mizani katika Kiarabu mara nyingi huishia kwa konsonati. Hili pia ni jambo lingine linalozifanya hati za Kiarabu zisifae kukiandika Kiswahili. Dhehebu la UMCA lilichapisha vitabu kufuatia mtindo uliotumiwa katika kuchapisha vitabu vya Steere. Misheni wa Kizungu walifanana na waanzilishi wa uchunguzi wa Kiswahili kwa kuwa ilikuwa rahisi kwao kutumia hati za Kirumi badala ya zile za Kiarabu. Mkutano wa Dar es Salaam wa 1925 uliamua kutozitumia hati za Kiarabu pamoja na konsonanti za Kiarabu kama vile kh. 18* Uamuzi huu wa l925 uliwakasirisha wengi wakiwa ni pamoja na gazeti la Mombasa, Al-Islah, kama ilivyo- jadiliwa kwa kireru katika sehemu ifuatayo. Profesa Carl Meinhof alipohudhuria mkutano wa Mombasa wa 1928, waliohudhuria walikuwa na nafasi ya kushauriana naye kuhusu othografia ya Kiswahili. Meinhof alikubaliana na nyingi kati ya tahajia iliyopendeke- zwa kwa kuwa ilikuwa rahisi bila kutatanisha, isipokuwa katika herufi ch na ng'. Meinhof alipendekeza c itumiwe badala ya ch. Badala ya kutumia alama tatu za maandishi (ng') kusimamia sauti moja, alipendekeza kutumiwa kwa n yenye mkia itumiwe kama ilivyo katika maandishi ya kifonetiki. Lakini mashauri haya ya Meinhof hayakukubaliwa. Wasomi wa Kiswahili wakati huo walijiona kuwa sahihi, na kwamba mapendekezo ya Meinhof yalifaa tu katika maandishi ya kifonetiki katika isimu lakini hayakufaa othografia ya kawaida ya Kiswahili. Katika majadiliano yao -- 18* Baadaye matumizi ya kh yalikubaliwa. Katika makala ya mhariri ya kitabu cha Hemedi Abdalla - Utenzi wa Vita vya Wadachi Kutamalaki Mrima (uk. 7) Allen anaandika: "Kwa hivyo ninatumia othograria sanifu ikiwa ni pamoja na kutumiwa kwa herufi kh iliyoidhini- shwa kutumiwa kwa hiari mnamo 1958". 30 walitaja kwamba ingekuwa vigumu kupiga taipu n hiyo yenye mkia. Tatizo hili lingetatuliwa hapo mwanzoni kwa kupiga taipu herufi j juu ya n wakingojea kurekebishwa kwa mashine. Suluhisho hili halikukubaliwa, na kwa hivyo tatizo la kuandika sauti ya kwanza ya neno ng'ombe kwa sauti mbili na alama (ng') lingali laendelea. Upungufu mwingine wa othografia ya Kiswahili unaoweza kutajwa hapa ni kule kukosa kutofautisha konsonanti za kipua (nazali) ambazo ni mizani kamili na zile ambazo huambatana na irabu ili ziunde mizani kamili. (Taz. Mkude 1982). Mifano ya konsonanti za kipua (nazali) ambazo ni mizani kamili ni m na n za kwanza katika maneno mmea na nne. Sauti n ya neno nguruwe ni sawa na sauti ya n yenye mkia. Kwa hivyo, kama tungefuata othografia sanifu kikamilifu badala ya nguruwe tungeandika ng'guruwe. Othografia ya Kiswahili sanifu haikukosa malalamiko. Kulikuwa na upinzani na kutoelewana hata kati ya misheni. Kasisi Roehl katika makala yake "Hali ya lugha katika Afrika Mashariki" (Africa Vol.3, Na.2, 1930), anaeleza masikitiko yake kwamba Idara ya Elimu huko Dar-es-Salaam ilikuwa imeanzisha othografia kinyume cha mapendekezo ya wataalamu wa isimu wa misheni. Roehl analalamika kwamba, kati ya makosa mengine, othografia inazipa nafasi za kipekee sauti za Kiarabu na kulazimisha zitumike babala ya kuwapa wazungumzaji wa Kiswahili uhuru wa kuzitamka kutegemea vile wanavyotamka sauti za lugha yao na kuziandika sauti hizo vile wanavyozitamka. Roehl 19* anaeleza kwamba othografia ya Kiswahili yatakikana iwe ya Kiswahili wala si ya Kiarabu au ya Kiingereza. Kasisi Roehl anaeleza zaidi kwamba katika kuunda othografia ambayo inafaa Kiswahili zaidi, isiwe ni Tanganyika pekee ambayo inatoa uamuzi. Anapendekeza Kenya, Uganda na Congo (Zaire) zihusike ili kuunda othografia sanifu kwa watu wote wanaotumia Kiswahili. Kama tunavyojua sasa upungufu mkubwa uliofanywa na nchi za Afrika Mashariki katika kusanifisha Kiswahili ulikuwa ni kushindwa kushirikisha Zaire katika shughuli za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kama alivyo- pendekeza Kasisi Roehl. Upungufu huo, licha ya jitihada za Ronald Snoxall, unaeleza kuwepo kwa tofauti kadha kati ya Kiswahili cha Zaire na Kiswahili sanifu. Kama inavyofahamika na kuelezwa wazi na wasomi kama vile John Williamson katika uchambuzi wake wa Kingwana cha maandishi (I.L.C. --- 19* Roehl hakutaja sauti za Kiarabu alizokuwa akimaanisha. Yawezekana alimaanisha sauti kama vile dh katika fedheha dhulumu na adhibu au gh katika ghadhabu gharika na lugha ambazo hazipatikani kwingine ila katika maneno yaliyoazimwa kutoka Kiarabu. 31 Bulletin Na. 21, 1951: 15-16), lahaja ya Kingwana haifuati upatano maalum kwa sababu ya kukosa kusanifishwa. Williamson alipata kwamba, katika makala moja herufi y na j zilitumiwa moja badala ya nyingine. Kwa hivyo maneno kama vile miji, jina, pamoja na kijana yalitumiwa katika sehemu moja ya makala, na kwingine katika makala hiyo hiyo maneno hayo yangeandikwa kama muyi, yina, pamoya na kiyana. Herufi r na l pia zilitumiwa moja badala ya nyingine. Habari, mara na hubiri yaliweza kupatikana katika makala moja na habali, mala na hubili. Herufi k na g zilichanganywa hivi kwamba maneno miziko na mizigo, ukonjwa na ugonjwa pia yalipatikana katika makala moja. Kupatikana kwa maneno kama vile muyi, habali, miziko, ukonjwa katika makala moja na mji, habari, mizigo na ugonjwa katika othografia ya Kingwana yaonyesha kwamba ni rahisi kusanifisha. Iligunduliwa kwamba ilikuwa rahisi kusoma na kuelewa maandishi ya Kiswahili sanifu cha Afrika Mashariki kwa kutujia ujuzi wa Kingwana: Snoxall 20* anaeleza kwamba alijaribu mara mbili kukifanya Kingwana kifuate taratibu za Kiswahili sanifu cha Afrika Mashariki. Kwanza alimtuma C. G. Richards aliyekuwa mkurugenzi wa East African Literature Bureau kwenda Belgian Congo (Zaire) kuwahimiza wasanifishe Kingwana. Richards alienda huko lakini hakufanikiwa. Snoxall alitamani kusambaza Kiswahili sanifu cha Afrika Mashariki ambacho chatumiwa na watu wengi zaidi. Maoni yake ni kwamba, Kingwana chatumiwa katika sehemu moja ya nchi moja, na kwa kuwa wanaokizungumza wanafahamu Kiswahili sanifu, ingekuwa rahisi kuwaleta pamoja na wale wanaotumia Kiswahili sanifu cha Afrika Mashariki: "Ingekuwa kazi rahisi ikifanywa kwa bidii". (Snoxall ibid.) Jaribio la pili alilofanya Snoxall lilikuwa ni kuwaalika Wabelgiji wawili kutoka Kongo (Zaire) kuhudhuria mkutano wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki mjini Nairobi. Wabelgiji hao waliitikia mwaliko lakini walishangaa kuona kwamba kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilikuwa na wajumbe Waafrika. Wabelgiji hawakufikiria kwamba wajumbe wa Kiafrika kama vile Shaaban Robert wangeweza kuwa wataalam wa lugha yao. Kwa hivyo Wabelgiji hawakutaka kujiunga na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Hawakuona kama ingekuwa vizuri kufanya hivyo. Ingawaje, Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, iliweza kuwajulisha watawala wa Kongo ya Ubelgiji kwamba tofauti kati ya Kingwana na Kiswahili sanifu ilikuwa ni matamshi yasiyofuata kanuni za safuri. Maoni -- 20* Mahojiano na mwandishi February 10 1984. Hali imebadilika sasa kwa kuwa Kiswahili cha Zaire kimesanifishwa. 32 hayo ya Kamati yalipelekewa watawala wa Kongo na Bwana Sandrart wa kutoka Rwanda aliyetumwa na Kongo ya Ubelgiji kuhudhuria mkutano wa kumi na tatu (13) wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki mnamo 1950. Bwana Sandrart aliweza kuifahamisha Kamati mambo kadha kuhusu Kingwana. Tofauti za kimatamshi hazikutatiza kueleweka kwa Kiswahili katika kukisanifisha ndiko kulikopendekezwa na Roehl katika Zaire, Rwanda na Burundi. Iwapo Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ingefaulu kuwashawishi watawala wa Kibelgiji kutumia Kiswahili sanifu, hali hiyo ingewezesha kutumiwa kwa vitabu vya Kiswahili sanifu katika eneo kubwa zaidi. Kiswahili kingepata matumizi mapya ya kuwaunganisha Wazungu wenye asili za Uingereza na Ubelgiji mbali na kuwaunganisha Waafrika wa makabila na mataifa mbalimbali, kwa kuwa kungekuwa na lugha moja ya mawasiliano katika Afrika Mashariki na Kati. Pia Wakongo wangekuwa na Kiswahili sanifu. Kushirikishwa kwa Kongo na nchi zingine zinazotumia Kiswahili katika kukisanifisha ndiko kulikopendekezwa na Roehl katika makala yake ya 1930. Canon G. W. Broomfield alijibu makala ya Kasisi Roehl kwa haraka alipoiandika makala yake "Kukifanya Kiswahili kiwe cha Kibantu" (Africa Vol.4 Na. 1,1931). Broomfield anaanza kwa kumfahamisha Roehl kwamba othografia ambayo Roehl anaizungumzia ilifanywa na kamati mjini Dar es Salaam mwezi Oktoba 1925. Kwa hivyo, anaeleza kwamba othografia hiyo haikubuniwa na Idara ya Elimu kama alivyodai Roehl. Anasema kwamba Tanganyika pamoja na Zanzibar zilihudhuria na kwamba Kenya haikuhudhuria kutokana na kutoelewana hata ingawa ilikuwa imealikwa. Anaendelea kueleza kwamba othografia iliyoidhinishwa ni ile ambayo ilikuwa ikitumiwa kwa miaka mingi na UMCA isipokuwa kutokutumiwa kwa kh. Maneno ambayo hapo awali yalikuwa yakiandikwa kwa kutumia konsonanti mbili zikifuatana kama vile hatta, milla na marra ingebidi yatumie konsonanti moja: hata, mila na mara. Kutumiwa kwa kh katika maneno kama vile khabari, khatia na khalisi, ilibidi yatumie h pekee: habari, hatia na halisi. Katika makala hiyo Broomfield anataja pia kwamba mmishonari mmoja alipinga othografia hiyo katika mkutano wa Dar es Salaamu wa 1925, lakini wanachama watano waliiunga mkono. Maelezo haya yana- onyesha kwamba ni watu wachache sana waliohusika katika kuamua suala la othografia. Yawezekana kwamba kanisa la Roehl, misheni ya Lutheran, haikualikwa kutoa maoni yao au kuhudhuria mkutano huo wa 1925. Kuhusu msamiati wa Kiarabu katika Kiswahili ambao unasababisha 33 kuwepo na konsonanti za Kiarabu katika othografia ya Kiswahili, Broomfield anaeleza kwamba maneno yenye asili ya Kiarabu ni maneno ya Kiswahili. Anadai kwamba maneno yenye asili ya Kiarabu ni maneno ya Kiswahili hivi kwamba Kiswahili hakijawahi kuwepo bila ya maneno ya Kiarabu na kwamba hakiwezi kuyaondoa. Kwa hivyo hakubaliani na maoni ya Roehl, ya ukweli kwamba hapo mwanzo Kiswahili kilikuwa lugha safi ya Kibantu na kwamba maneno ya Kiarabu yaliazimwa. Ukweli kwamba Kiswahili kilikuwepo kabla ya kuja kwa Waarabu hauwezi kubishaniwa. Hii ndiyo sababu mhariri wa jarida la Africa alisahihisha maoni ya kupotosha ya Broomfield katika maoni ya mhariri yaliyotangulia makala hiyo. Majadiliano ya othografia yaliendelea wakati wa vita vya pili vya dunia. Mjadala huo wa wanakamati ulihusu mageuko ya irabu yaliyosababishwa na mfuatano wa irabu mbili katika neno moja. Mageuko hayo ni kama vile kuenda na tuataka kuwa kwenda na twataka. Kasisi A. R. Pittway kutoka Kenya, aliyefanya uchunguzi wake katika lahaja ya Kimvita, aliuanzisha mjadala katika jarida la Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki Bulletin Na. 13 la 1939. Pittway anaeleza kwamba kwa kuwa usanifishaji unahusu lahaja tofauti kusiwe na lahaja yoyote muhimu itakayopuuzwa. Anasema kwamba maneno ambayo si ya Kiunguja, semi, na miundo ya kisarufi, yastahili kukubaliwa kutumiwa sambamba na Kiswahili sanifu ili kutajirisha lugha. Kwa maoni yake, kukubaliwa kwa matumizi hayo ya kilahaja kutasaidia kufanya Kiswahili kipendwe sana na watu. Pittway anaendelea kupendekeza kwamba mw inayotangulia u igeuzwe kuwa mu. Anaeleza kwamba ni kawaida mu kugeuka kuwa mw inapo- tangulia a,i,e na o, lakini kifonetiki si jambo la kawaida kwa mu kugeuka kuwa mw inapotangulia u. Pittway alitaka mabadiliko hayo kwa sababu dhehebu lake la C.M.S. Iililokuwa limeamua kusanifisha Biblia na Kitabu cha Maombi lilihitaji muongozo. Alisema kwamba mabadiliko hayo yalikuwa muhimu kwa sababu matumizi ya mu na mw katika vitabu vilivyopitishwa na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki yaelekea hayakufuata kanuni yoyote. Kama ilivyotarajiwa, makala ya Pittway iliyoandikwa mara tu baada ya kuchapishwa kwa kamusi za Kiingereza-Kiswahili na Kiswahili-Kiingereza, ilipingwa mara moja. Katika jarida, Bulletin Na. 14 la 1948, Ronald Snoxall anatahadharisha dhidi ya othografia inayokwenda kinyume cha kamusi sanifu iliyoichukua kamati miaka mingi kutayarisha. Kwa hivyo pendekezo la Pittway halipaswi kukubaliwa kuvuruga othografia iliyo- kubaliwa. Snoxall anapendekeza othografia iliyotumika katika kamusi ikubaliwe vile ilivyo. 34 Maoni mengi kuhusu pendekezo la Pittway yalitolewa na Kasisi Fr. Alfons Loogman wa Bagamoyo aliyetahadharisha dhidi ya kukubali kanuni za lugha zibadilishe othografia iliyokubaliwa. Loogman anaeleza kwamba kusanifishwa kwa Kiswahili kuna maana kwamba lahaja moja ilichaguliwa kuwa msingi wake na kwamba inabidi lahaja zingine ziwe tayari kupoteza baadhi ya miundo na kanuni za sarufi zao licha ya umuhimu wa lahaja hizo. Hata hivyo Loogman anaunga mkono kanuni ya mgeuko wa sauti uliotajwa na kusema kwamba hakuna mtu angependa kusema yaitu, waivi au maino badala ya yetu, wevi na meno. Katika kukomesha mjadala huu, katibu wa kamati Kasisi B. J. Ratcliffe anakiri kwamba hakuna othografia inayoweza kutosheleza mahitaji yote ya lahaja zote. Anatoa msimamo rasmi kueleza hivi: "'M' ya Kiswahili kwa kawaida husimamia 'm', 'u' hutoweka kabla ya konsonanti, na mara nyingi huwa 'w' inapotangulia irabu ila wakati inapotangulia kiini cha neno linaloanzia kwa 'u' au kabla ya 'w' au hugeuka kuwa 'w' wakati mwingine iwapo maneno yanahitaji kugeuka huko." (ibid. uk. 6). Ni jambo zuri kwamba Kamati ilipinga mabadiliko ya othografia. Kama watu wangekuwa huru kurekebisha othografia katika siku hizo, hatungejiepusha na makosa. Tungekumbwa na othografia ya kizamani kama ile ya Kiingereza ambapo maneno yanaandikwa kwa njia tofauti sana na vile yanavyotamkwa. Nikitoa mifano miwili tu, neno Leicester hutamkwa Lesta, na Gloucester hutamkwa Glosta. 2.3 Maoni kuhusu usanifishaji Kumbukumbu iliyojulikana kwa jina "Kiswahili cha Kisasa", I.L.C. Bulletin Na. 7 1934, iliandikwa na afisa wa Idara ya Elimu nchini Kenya. Kumbukumbu hiyo ilipelekewa katibu wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na Mkurugenzi wa Elimu ili ijadiliwe katika mkutano wa Kamati. Mwandishi ambaye hakutaja jina lake alitahadharisha Kamati kwamba Kiswahili walichokuwa wakishughulikia kilikuwa kikiendelea kuwa lugha ngeni kwa Waswahili wenyewe kwa kutengenezewa kanuni mpya na wageni. Sehemu moja ya kumbukumbu hiyo ilisema hivi:- "Tumesanifisha Kiswahili, na katika shughuli za kufanya hivyo yaonekana Kiswahili kimekuwa lugha mpya. Bila shaka sote tunakiri kwamba kama lugha zingine Kiswahili kitaendelea na kitapanuka 35 katika nyanja za muundo, semi na msamiati kwa kuathiriwa na ustaarabu wa walowezi. Lakini maendeleo hayo yafaa yatokane na mawazo ya Waswahili; haifai kuwalazimisha kuyapokea. Lakini hivyo ndivyo ilivyo; tuko katika harakati za kuwafunza Waswahili Iugha yao kupitia vitabuni, vingi ambavyo si vya Kiswahili kimuundo au kimawazo, na ambavyo lugha yake inafanana kidogo sana na lugha inayozungumzwa. Labda tuna haraka sana kuhepa ukweli kwamba Waswahili wenyewe wana uwezo wa kurekebisha lugha yao kufaa mahitaji ya siku hizi na kwamba tayari wanafanya hivyo kwa haraka ya kustaajabisha. Hivi ndivyo hali ilivyo huko Mombasa na inaweza kudhihirishwa na wachunguzi wengi. Jambo muhimu sana ni kwamba jitihada zetu hizi za kupata mwana haramu huyu, Kiswahili cha Kiingereza, zina matokeo ya kututenganisha na jamii tunaojaribu kuelimisha. Au tukieleza kwa maneno mengi, tunafikiria kwa Kiingereza hadi wao wanafikiria kwa Kiswahili na hatuwezi kuziba pengo hili." (I.L.C. Bulletin Na. 7 1934: 4). Mwandishi anafikiri kwamba sifa nyingi zisizo na kifani zilitolewa kuwasifu wachunguzi wakuu wa Kiswahili kama vile Krapf, Steere, Sacleux, Taylor, Veltten na Beech bila ya kujali kazi zao ambazo zingetumiwa shuleni. Anafikiri kwamba kamati ilikuwa na haraka sana ya kuandika vitabu na kutafsiri vingine na kwamba katika kufanya hivyo wakaguzi wasiokuwa na ujuzi waliajiriwa. Anaendelea kusema kwamba wale wanaoitetea hii lugha mpya wanasema kwamba ndiyo ya pekee inayoweza kueleweka na makabila yasiyokuwa ya Waswahili. Anakanusha wazo hili kwa kusema kwamba ni rahisi kwa Waafrika kujifunza Kiswahili kuliko Kiswahili hiki kilichochanganywa na muundo wa Kiingereza. Ili kuthibitisha kwamba Waswahili walipinga mtindo huu mpya wa Kiswahili na othografia yake, mwandishi wa "Kiswahili cha Kisasa" aliambatisha makala kutoka gazeti la 'Al-lslah' la Mombasa. Makala hiyo ilikuwa ya Juni 20, 1932 ambayo mwandishi aliishambulia othografia mpya ya Kiswhili. Othografia iliyokubaliwa kama tulivyoeleza haikuwa na baadhi ya herufi kama vile kh inayopatikana tu katika maneno yaliyoazimwa kutoka kwa Kiarabu. Othografia iliyokubaliwa ingekuwa na h badala ya kh na hii ni mojawapo ya sababu zilizomfanya mwandishi wa makala ya Al-lslah alalamike. Makala hiyo inasema hivi: "Ni madhara makubwa tupatayo kwa Kiswahili hiki kilichoharibiwa ni Wazungu. Kiswahili ni lugha ya watu wa Pwani, nacho hakiwi safi ella kitanganyikapo na Kiarabu. Tangu kufika Wazungu, wame- kigeuza na kukiharibu kwa wapendavyo wao; wamepunguza baadhi 36 ya harufu ambazo ni lazima ziwemo katika baadhi ya maneno, na pengine hubadilika maana kwa kukosekana harufu hizo. Wameitungia vitabu vya nahau, na pengine hao watungao vitabu hivyo ni Wazungu wageni hawajui sana lugha hii, na ambao wavitowa makosa ni Wazungu wa bara, wasiojuwa Kiswahili. Na wakiambiwa ni mtu wa Pwani kuwa ni makosa, hawakubali ella kile kile chao ..." (I.L.C. Bulletin Na. 7, 1934: 8). Mwandishi wa "Kiswahili cha Kisasa" anaendelea kutilia nguvu mambo aliyoyataja kwa kusema kwamba baadhi ya vitabu vilivyochapishwa hivi karibuni vilikuwa tafsiri ya neno kwa neno ya vitabu vya Kiingereza. Anasema kwamba matumizi ya kanuni za sarufi yalikuwa yakihimishwa sana jambo ambalo lilifanya vitabu vilivyochapishwa kuwa sahihi kisarufi, lakini vilikuwa mbali sana na Kiswahili halisi kwa kuwa sarufi peke yake haiundi lugha. Anataja upungufu mkubwa wa Kiswahili "kipya". Upungu- fu huo ni, tafsiri ya neno kwa neno, kuzingatia matumizi ya kanuni za sarufi bila ya kujali methali na semi pamoja na kutojali tabia ya kishairi ya Kiswahili. Mwishowe anatoa mifano ya sentensi ambazo zina upungufu kutokana na vitabu vilivyoandikwa kwa Kiswahili sanifu vilivyokuwa vikitumika shuleni wakati huo. Katika jarida hilo hilo la Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, kufuatia makala hiyo ya "Kiswahili cha Kisasa" kuna jibu lake lililo- andikwa na Kasisi Canon Broomfield mwandishi wa kitabu kijulikanacho kama Sarufi ya Kiswahili, ambaye kwa wakati huo alikuwa mhariri kutoka Zanzibar. Canon Broomfield alikuwa ameombwa na katibu wa Kamati kumjibu mwandishi wa "Kiswahili cha Kisasa" kwa manufaa ya wasomaji wa jarida. Katika jibu lake Canon Broomfield anaonelea kwamba mwandishi wa "Kiswahili cha Kisasa" ametia chumvi suala la kugeuka kwa Kiswahili kuwa lugha mpya. Anasema kwamba marekebisho yaliyokuwa yakitokea yalikuwa hayana budi kuwepo kwa kuwa lahaja moja ndiyo ilichaguliwa kuwa msingi wa kusanifisha Kiswahili. Kwa hiyo marekebisho yalifanywa ili kusaidia kutumiwa kwa lahaja hiyo kama lugha ya mawasiliano kote. Usanifishaji ulihitaji kusomesha Kiswahili hicho ambacho chaonekana kuwa kipwa. Anaeleza zaidi kwamba Kiswahili sanifu chaonekana kuwa lugha mpya zaidi katika lahaja zinazotofautiana sana na Kiunguja, ambacho ndicho msingi wa usanifishaji. Kuhusu athari za Kiingereza katika Kiswahili, Broomfield anaeleza kwamba hilo ni jambo lisiloweza kuepukika kwa sababu lugha mbili zinapotumika katika eneo moja hazina budi kuathiriana na haziwezi kubaki kuwa safi, pia matokeo ya kuazima huenda yakatajirisha lugha 37 inayoazima. Anatoa mifano ya semi za Kiebrania zilizoingia katika Kiingereza kupitia tafsiri ya Biblia. Sasa semi hizo zimekuwa Kiingereza. Anatetea kile kinachoonekana kama tafsiri za neno kwa neno au tafsiri za semi za Kiingereza kwa kusema kwamba Kiingereza kinaathiri Kiswahili cha mazungumzo cha Waafrika wanaozijua lugha zote mbili. Anasema kwamba mabadiliko kama hayo ni ya kawaida kwa kuwa lugha hubadilika kila mara na kwamba Kiswahili cha wakati huo hakikuwa sawa na Kiswahili cha wakati wa Krapf. Haoni kama Kiswahili kinaweza kujiepu- sha na kuazima kwa istilahi za ufundi na teknolojia. Broomfield anaandika hivi: "Maendeleo yoyote ya kielimu huhitaji kuwa na mabadiliko na maendeleo ya lugha itakayotumika kueleza elimu hiyo. Tupende tusipende, Kiswahili kitabadilika na kuendelea kwa haraka, kwa sababu hizi. Katika wakati huu kuna maandishi machache sana na tunaanza kusanifisha lugha hii, pia Waafrika wanaojua kusoma na kaundika ni wachache sana. Tena Afrika inawasiliana na ustaarabu wa Uropa; elimu mpya na utaalamu mpya wa kila aina unawafikia Waafrika. Kiswahili cha miaka ishirini tu iliyopita hakifai siku hizi. Ni lazima lugha ibadilike na itabadilika, tupende tusipende..." (Broomfield I.L.C. Bulletin Na 7, 1934: 4). Njia za kukuza lugha zitakuwa ni pamoja na kuazima maneno kutoka lugha za kigeni hasa Kiingereza na kuunda maneno mapya. Broomfield anaonya kwamba lazima watu wajifunze maneno hayo na vile yanavyo- tumika. Anatoa mfano wa maneno kumi na tisa (19) yaliyoundwa kutokana na neno vote aliloliazima kutoka kwa Kiingereza, ambayo anasema, kwamba yanaweza kueleweka vizuri baada ya kujifunza maana ya neno vote. Broomfield anasema kwamba mwandishi wa kumbukumbu hakuzi- shughulikia lahaja tofauti za Kiswahili ambazo zatofautiana kimsamiati, kimatamshi, sarufi na semi ambazo zaifanya kazi ya wahariri wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kuwa ngumu. Anasema kwamba wahariri hawatarajiwi kuandika upya miswada wanayopelekewa. Anaeleza kwamba, Kiunguja kinapotumiwa kama msingi wa usanifishaji jitihada zinafanywa kuzihusisha lahaja zingine kwa kuwa lahaja zote kubwa zitakichangia Kiswahili katika siku za baadaye. Broomfield anakanusha madai ya mwandishi wa kumbukumbu kwamba kuna chochote katika kazi za Meinhof, Werner, Madan, Torrend, Domet, Stigand na kadhalika ambacho chaweza kufaa shuleni. "Yako wapi maandishi hayo; je, twapata chochote kinachoweza kutumika kama vitabu vya shule vya jiografia, historia, hesabu, 38 afya, elimu ya viumbe, kilimo au uraia? Mbali na uchunguzi wa kiisimu unaokusudiwa kusomwa na Wazungu, maandishi mengine mengi, zaidi ni mkusanyiko wa mila, ngano na hadithi. Nyingi kati ya hizi ni za lugha isiyo na adabu na nyingi hazina umuhimu wowote wa kielimu." (Broomfield, I.L.C. Bulletin Na. 7, 1934: 19). Anakiri kwamba uandishi wa vitabu umefanywa kwa haraka na kwamba baadhi ya vitabu hivyo havikosi upungufu lakini kuchaguliwa kwa Kiswahili na kule kupenda kwa nchi zote za Afrika Mashariki kutumia Kiswahili wastani kumesabibisha hali kuwa hivyo. Wale walio- andika vitabu walifanya hivyo kwa sababu hapo awali hakukuwa na vitabu kama hivyo na ni juu ya wale wanaotoa lawama kuandika vitabu bora zaidi. Mwisho kabisa Broomfield anataja kwamba kusanifisha na kuunganisha lugha ni kazi ngumu sana na kwamba wale wanaoishughulikia hawata- pendwa. Makala iliyoandikwa katika gazeti la Al-Islah imeandikwa kwa Kimvita na wale ambao hawatumii lahaja hiyo hawataisifu kamwe. Pia Broomfield anasema kwamba, katibu wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki alijibu makala ya Al-Islah lakini gazeti hilo halikuichapisha. Huko kuonekana kwa Kiswahili kuwa ni lugha ngeni kwa sababu ya kutafsiri wakati wa usanifishaji, kwa maoni yangu, hakungeepukika. Hiyo ilikuwa deni ambayo ilibidi Kiswahili kilipe kwa maendeleo yake ya haraka. Kiswahili ambacho hapo awali kilikuwa tu lugha ya biashara, kilianza kutumika kwa haraka kama lugha ya elimu siyo tu Uswahilini bali kote katika Afrika Mashariki. Kwa hivyo Kiswahili hakikuwa tena lugha ya Waswahili tu kama vile mwandishi wa "Kiswahili cha Kisasa" alivyosema bali kilikuwa lugha ya halaiki kubwa ya watu wa Afrika Mashariki nzima. Ili kukiwezesha Kiswahili kiumudu wadhifa huo, ilibidi vitabu vitayarishwe kwa muda mfupi. Siku hizo hakukuwa na Waafrika wa kutosha ambao wangeweza ama kuandika vitabu vilivyohitajika au kutafsiri vya Kiingereza kwa Kiswahili. Maoni kwamba Kiswahili kilikuwa kikichafuliwa kwa kusanifishwa na kwa kutumiwa kwa kuandikia na kutafsiria vitabu vya shule hayakuwa Kenya pekee. Nchini Zanzibar, kilikotoka Kiunguja, kulikuwa na hofu kwamba lahaja ya Kiunguja itachafuliwa na jitihada za usanifishaji. Akitoa ripoti yake kuhusu vitabu vya shule ya mwaka 1927, Mkaguzi wa Shule wa Zanzibar, Bwana G. B. Johnson alieleza masikitiko yake kwamba ni sharti vitabu vinavyotumiwa Zanzibar vikubalike huko Tanganyika. Alisema kwamba ni sharti vitabu hivyo viwe vya "Kiswahili kilichorekebishwa kuambatana na maagizo ya Kamati ya Uchapishaji ya Tanganyika". Ilibidi vitabu vya Zanzibar vikubalike Tanganyika kwa 39 sababu Zanzibar ilikuwa ikihitaji vitabu vichache sana na gharama ya kuchapisha vitabu vya shule za Zanzibar pekee ilikuwa kubwa. Zanzibar ilifurahia uamuzi wa kutumiwa kwa Kiunguja kuwa msingi wa kusanifisha Kiswahili. Lakini kulikuwa na hofu kwamba ingewabidi Wazanzibari kutumia maneno na miundo kutoka Tanganyika. Jambo hili liliwakera sana kama inavyodhihirishwa na maneno ya Johnson. "Yaonekana wazi kwamba hatimaye Zanzibar italazimika kutumia vitabu vya shule vilivyoandikwa kwa lugha yao iliyochafuliwa. Hili ni jambo la kusikitisha hata ingawa yaonekana haliepukiki. Hii ni gharama kubwa ya kulipa dhidi ya usanifishaji wa Kiswahili. Watu wa Zanzibar wanaojiona kwamba wanakitumia Kiswahili safi wanachukizwa na kutumiwa kwa Kiswahili cha bara ambacho kwao wanakiona kwamba ni lugha iliyoharibiwa. Kuhakikisha kwamba shule zetu zinatumia Kiswahili sanifu kutakuwa kazi ngumu isiyo- pendeza na itachukua muda kabla matumizi ya bara hayajakuba- lika." 21* Kutumiwa kwa Kiswahili kama lugha ya vitabu vya shule kulikuwa ni matumizi mapya ya lugha hiyo. Lugha ya vitabu vya shule ni tofauti na lugha ya mazungumzo. Katika Kiswahili, tofauti hiyo ilionekana kuwa kubwa sana kwa sababu ya maendeleo ya haraka yaliyochukua muda mfupi na kwa kuwa Waafrika hawakutumiwa kuyatekeleza maendeleo hayo. Jambo muhimu lililosababisha masikitiko ni kule kutumika shuleni kwa vitabu vilivyotafsiriwa vibaya vikiwa na ithibati ya Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Matumizi ya semi na miundo ya Kiingereza katika vitabu hivyo vilivyotafsiriwa neno kwa neno hayakukanushwa na Broomfield kama nilivyotaja. Baadhi ya wanakamati pia waliyapigia makelele matumizi hayo. Alipokuwa akiandika kuhusu siku hizo za mwanzo wa usanifishaji wa Kiswahili, Snoxall anatukumbusha kwamba kulikuwa na vitabu vichache sana na kwamba kamati ilitegemea sana tafsiri za Kiingereza zilizokuwa zikitafsiriwa na wanakamati wenyewe. Vitabu vya waandishi kama vile Rivers-Smith, Mkurugenzi wa Elimu Tanganyika, vilifaa sana. Snoxall anasema kwamba baadhi ya tafsiri hizo zilikuwa za neno kwa neno na anashangaa iwapo wanafunzi walizielewa. (Snoxall 1982: 3) 22*. -- 21* Zanzibar Protectorate Administrative Reports for the Year 1927 - Iliyochapishwa 1928. Sehemu iliyonakiliwa inagusia mkutano wa Mombasa wa 1928. 22* Mfano mmoja ambao Snoxall anaukumbuka sana kutoka kitabu cha Uraia ambacho kilikuwa tafsiri ya A Manual of Citizenship na Rivers-Smith ni: "Watu wa Taifa hilo wamekwisha panda kipawa kingine katika ngazi ya ustaarabu". Wanafunzi walitaka kujua ni nini "Ngazi ya ustaarabu" na ilikuwa wapi? 40 Sura ya Tatu 3.0 Miaka ya mwanzo ya usanifishaji 3.1 Kabla ya vita Kipindi cha kuanzia 1930 hadi 1938 kilikuwa muhimu sana kwa historia ya usanifishaji wa Kiswahili. Katika kipindi hicho, msingi imara sana uliwekwa na kukaanzishwa kiwango cha juu cha kufanya kazi. Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilihitaji msingi imara hivyo ili kuiwezesha kufanya kazi wakati wa vita. Sifa nyingi za mafanikio ya Kamati zatokana na kazi nyingi na ya kuchosha iliyofanywa na Frederick Johnson aliyekuwa katibu wa kwanza wa Kamati hiyo. Mbali na kutafsiri vitabu vingi, Johnson alifanya kazi nyingi ya kutunga kamusi za Kiswahili-Kiswahili, Kiswahili-Kiingereza na Kiingereza-Kiswahili. Nitaanza sehemu hii kwa kujadili hali nzuri ya wakati huo iliyoisadia kamati kufanikiwa. Hasa sera ya lugha ya nchi za Afrika Mashariki wakati huo, iliwataka maafisa waliozifanyia kazi nchi hizo, wapite mitihani ya lazima ya Kiswahili. Kisha tutaijadili kazi yenyewe ambayo Kamati ilikuwa ikifanya. Serikali zote za Afrika Mashariki, Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar ziliunga mkono Kamati kwa kuwa zote ziliwakilishwa katika Kamati. Sera ya lugha za nchi zote zilikisaidia Kiswahili kama tutakavyo- endelea kufafanua. Wafanyakazi Wazungu wa nchi hizi zote ilibidi wajifunze Kiswahili na waipite mitihani. Walioshindwa kufauli mitihani hiyo walibaki kuwa wafanyakazi wa muda wala si wa kudumu. Kwa hivyo iliwabidi maafisa wa serikali Wazungu wajifunze Kiswahili. lli kupandi- shwa cheo kazini iliwabidi wapite mitihani ya juu ya Kiswahili. Sera hii ilikipa Kiswahili hadhi. Mitihani hiyo ya Kiswahili ilisababisha mahitaji ya kuchapisha vitabu vitakavyowasaidia maafisa hao kujitayarisha kufanya mitihani hiyo. Pia vitabu hivyo vilinunuliwa kwa wingi kwa kuwa maafisa hao walitamani kupita mitihani ili wazihifadhi kazi zao. Kwa hivyo mitihani hiyo ilisaidia kukuza na kueneza Kiswahili pamoja na kuongeza idadi ya vitabu vilivyochapishwa wakati huo. Sasa tutajadili vile sera ya lugha ilivyokuwa katika kila nchi. 23* -- 23* Maagizo haya yapatikana katika kitabu cha Ratcliffe na Elphinstone kiitwacho Modern Swahili 1932: 295-310. 41 Nchini Kenya, kulingana na barua ya Katibu Mkuu namba 40 ya Juni, 1, 1931, mbali na mitihani ya Wazungu waliokuwa wafanyakazi wa Jeshi la King's African Rifles ambayo ilikuwa na maagizo yake tofauti, maafisa wengine wote Wazungu waliokuwa wakifanya kazi katika Koloni iliwabidi wafanye mitihani ifuatayo ambayo ilikuwa ya lazima. Mtihani uliotangulia ulikuwa, mtihani wa kwanza wa mahojiano kwa Kiswahili ambao ilibidi ufanywe kabla ya mwaka mmoja kwisha tangu kuajiriwa kwa kazi isiyokuwa ya kibarua. Iwapo afisa aliyehusika hangepita mtihani huo ilimaanisha kwamba hangepata nyongeza ya mshahara ya kila mwaka na pia ingesababisha kushushwa cheo na kuwa mfanyakazi wa kibarua. Kiwango cha Kiswahili kilichohitajika ni cha kumwezesha afisa huyo kufanya kazi kwa kutumia Kiswahili pasipo mahitaji ya mkalimani. Mtihani wa pili ulikuwa wa Kiswahili sanifu kiwango cha chini. Mtihani huu ulitahiniwa baada ya mwaka mmoja kwisha na kabla ya miaka miwili na nusu kwisha tangu afisa aajiriwe. Wale ambao hawakupita mtihani huo walichukuliwa hatua sawa na wale ambao hawakupita mtihani wa kwanza. Ili mtu aweze kupita mtihani huo ilibidi awe amefikia kiwango cha kuelewa na kuzungumza Kiswahili kwa ufasaha na ujasiri. Mtihani wa Kiswahili sanifu kiwango cha juu ndio uliokuwa wa tatu na wa juu sana kati ya hiyo mitihani ya lazima. Mtihani huo ulikuwa wa mahojiano pamoja na wa kuandika. Ulikuwa wa Wazungu wenye vyeo vikubwa na ulifanywa baada ya miaka mitatu na kabla miaka kumi haijakwisha tangu waajiriwe. Kukosa kupita mtihani huo kwa muda uliowekwa kuliathiri cheo cha afisa aliyehusika na kumaanisha kwamba hangeendelea kupewa nyongeza za mshahara. Ili mtu aweze kupita mtihani huo ilibidi aijue vizuri sarufi ya Kiswahili na aweze kuzungumza Kiswahili kwa ufasaha. Maagizo yaliyoihusu Uganda yapatikana katika tangazo la barua namba 40 ya Disemba 29, 1928 kutoka afisini mwa Katibu Mkuu. Maagizo hayo ni sawa na ya Kenya isipokuwa kwamba kuna tofauti chache nitakazoeleza. Kuhusu mtihani wa kiwango cha kwanza wa mahojiano, maafisa waliokuwa wakifanya kazi Buganda, waliruhusiwa kufanya mtihani wa Kiluganda kwa kiwango hicho, lakini maafisa waliokuwa wakifanya kazi katika sehemu zingine za Uganda ilibidi wafanye mtihani wa Kiswahili. Maafisa waliokuwa wakifanya kazi katika tawala za mikoa na wa Idara ya Elimu ilibidi wapite mtihani wa Kiswahili sanifu, kiwango cha chini kabla hawajathibitishwa kazini. Maafisa wengine wote wangethibitishwa kabla hawajapita mtihani huo, lakini baada ya kufanya kazi kwa muda wa miaka minne hawangepata tena nyongeza ya mshahara mpaka kwanza 42 wapite mtihani huo. Mtihani wa Kiswahili sanifu, kiwango cha juu nchini Uganda ulikuwa ukifanywa na maafisa wa tawala za mikoa, na idara za elimu, kilimo, mifugo, misitu na polisi. Maafisa wote wa idara hizi ilibidi wapite mtihani huo, la sivyo, mshahara wao haungezidi pauni 720. Nchini Uganda, maafisa wa serikali wangefanya mitihani ya kiwango cha chini na cha juu ya lugaha zingine za Uganda badala ya Kiswahili. Nchini Zanzibar, dondoo kutoka maagizo ya serikali ya Zanzibar yanaeleza kwamba ni lazima maafisa wote wa Kizungu wapite mtihani wa Kiswahili sanifu, kiwango cha chini kabla mwaka mmoja haujakwisha tangu waingie nchini. Wale ambao hawangepita mtihani huo ama hawangeendelea kuwa waajiriwa wa kudumu au hawangepata nyongeza ya mshahara ya kila mwaka. Wauguzi ambao hawangepita mtihani huo, ingebidi wasimamishwe kazi. Wale waliokuwa wakifanya mtihani wa Kiswahili sanifu kiwango cha juu walikuwa maafisa Wazungu ambao walikuwa wafanyakazi wa kudumu. Baada ya kupita mtihani huo walipewa kiinua mgongo cha pauni hamsini (50). Mbali ya huu mtihani wa Kiswahili kiwango cha juu maafisa Wazungu wa Zanzibar walikuwa huru kufanya mtihani wa Kiarabu au Kigujerati wa kiwango hicho. Watahiniwa wa mtihani wa kiwango cha juu wa Kiswahili, Kiarabu au Kigujerati ilibidi waweke amana ya rupia arobaini na tano (45), pesa ambazo wangerudishwa wapitapo mtihani. Maagizo yaliyoihusu Tanganyika yapatikana katika 'Maagizo kwa watu wote kutoka Afisi ya Katibu Mkuu, Dar es Salaam, Juni 15, 1931'. Kulingana na Maagizo hayo ilibidi maafisa wa Kizungu wapite mtihani wa Kiswahili sanifu, kiwango cha chini kabla mwaka mmoja haujakwisha tangu waajiriwe nchini. Wale ambao hawangepita mtihani huo hawa- ngeendelea kuwa waajiriwa wa kudumu. Mtihani wa Kiswahili sanifu, kiwango cha juu ulikuwa ukitahini ujuzi kamili wa Kiswahili, sarufi na muundo wa lugha kwa jumla. Watahiniwa waliofaulu walitakikana waweze kueleza maagizo, sheria na kanuni za serikali vizuri kwa Kiswahili. Pia walitakikana waweze kutafsiri kwa ufasaha maandishi ya Kiswahili kwa Kiingereza na ya Kiingereza kwa Kiswahili. Maagizo haya yote yaonyesha wazi kwamba sera ya lugha katika Afrika Mashariki wakati wa ukoloni ilikiunga Kiswahili mkono hasa wakati huo wa siku za mwanzo za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Sera hiyo ilikusudiwa kuwawezesha Wazungu kuwaelewa Waafrika wanapofanya kazi zao. Sera hii iliwaridhisha wanakamati ambao walijivunia kazi zao kwa kuona kwamba zilitambuliwa na serikali. Juhudi za Kamati ya 43 Kiswahili ya Afrika Mashariki hazikuzinufaisha shule tu, bali ziliwafaidi maafisa wa Kizungu ambao ilibidi wajitayarishe kufanya mitihani hiyo ya lazima. Ufafanuzi huu unatusaidia kuelewa ni sababu gani iliyowafanya wanakamati wawe na moyo thabiti wa kufanya kazi nyingi ngumu ya kusanifisha Kiswahili kwa kujitolea. Sasa tutaigeukia "warsha" ili tuone machache kati ya mambo muhimu yaliyokuwa yakifanywa na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kabla ya vita vya pili vya dunia. Kwa kifupi kazi nyingi na ngumu ilifanywa na maafisa wa serikali na misheni kutoka Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar waliojitolea kusanifisha Kiswahili. Hawakuwa na vitabu vya kutosha vya Kiswahili ambavyo wangetegemea kuwasaidia katika kazi zao. Mjadala mfupi unaofuata watokana na Jarida la Kamati - ILC Bulletin Na. 1 ya 1930. Waonyesha baadhi ya matatizo yaliyoikumba Kamati. Kabla ya kufikia uamuzi kuhusu msamiati sanifu, orodha za maneno zilipelekewa wahariri wa Kamati pamoja na kuchapishwa kwenye Jarida la ILC Bulletin ili kuwapa wahariri pamoja na raia nafasi ya kuyajadili. Maoni na mapendekezo tofauti yalijadiliwa na Kamati kabla orodha iliyokubaliwa haijachapishwa kama msamiati sanifu. Maoni na mapende- kezo yaliyotolewa na wahariri kabla uamuzi haujafikiwa yalitofautiana sana kama inavyodhihirishwa hapa chini. Kasisi B. J. Ratcliffe, mhariri wa Kenya, anapendekeza kwamba 'irabu' na 'herufi' zitumiwe badala ya kuazima 'vokali' na 'konsonanti' kutoka Kiingere- za. 'Herufi' ilipendekezwa badala ya 'harufu' ambalo lilikuwa likitumiwa kwa wingi na Waswahili wa Mombasa ili kulitofautisha na neno harufu la kawaida. Naye katibu wa Kamati, Frederick Johnson anashuku iwapo neno irabu latumiwa na watu wengi au latumiwa na Waswahili wachache wanaoandika kwa kutumia hati za Kiarabu. Kwa maoni ya Johnson neno herufi au harufu lilimaanisha hati yoyote ya maandishi iwe vokali au konsonanti. Kisha anafikia uamuzi kwamba neno lenye kumaanisha konsonanti lilikuwa lahitajika. Hivyo ndivyo neno konsonanti lilivyoazimwa. Mengi kati ya maneno tunayoyaona kuwa ya kawaida siku hizi, ilibidi yatolewe uamuzi. Mfano mmoja ni neno shule. Kasisi A. B. Hellier, mhariri wa Tanganyika alipendekeza neno shule lililoazimwa kutoka Kijerumani badala ya neno skuli lililoazimwa kutoka lugha ya Kiingereza. Naye Canon Broomfield alikuwa na maoni kwamba maneno yote mawili yangetumiwa kumaanisha vituo tofauti vya elimu. Broomfield aliyekuwa mhariri wa Zanzibar alipendekeza neno skuli litumiwe kumaanisha vituo na vyuo vya kufunzia walimu nalo neno shule limaanishe shule za vijijini tu. 44 Maoni yalitofautiana sana hivi kwamba inashangaza iliwezekanaje kamati ikaweza kutimiza mambo mengi hivyo. Tukitazama mifano ya maneno lindi na kina, twaona kwamba wahariri wote wanne walikuwa na maoni tofauti. Bwana Morris, mhariri wa Uganda alipendekeza kwamba neno lindi litumiwe badala ya kina. Kasisi Ratcliffe wa Kenya alisema kwamba neno sahihi ingekuwa kwina wala si kina. Canon Broomfield kutoka Zanzibar alisema kwamba neno kimo lilitumiwa kumaanisha urefu wa kwenda juu na wa kwenda chini, na kwamba neno kina lilikuwa halijulikani Zanzibar. Naye Kasisi Hellier alijaribu kutoa suluhisho kwa kusema kwamba "tukitumia kimo kumaanisha kwenda juu na kina kumaanisha kwenda chini tutakuwa tumepiga hatua mbele" (ILC Bulletin Na. 1 1930: 5). Baada ya kusoma aya za hapo juu mtu anaweza kushawishiwa kushuku ujuzi wa kamati na wahariri wake. Maoni kama hayo yangekuwa ya haraka na yasiyo ya kweli kwa sababu watu hao walikuwa wakishughulikia karibu kila kitu, kuanzia maneno ya kawaida ya kila siku ambayo yalihitajika hadi sarufi ya Kiswahili. Wewe unayesoma kitabu hiki, jihisi u mmoja kati ya wanakamati, naye Kasisi A. B. Hillier anakufahamisha kama alivyoifahamisha Kamati kwamba: "Sarafu za senti hamsini, senti kumi, na senti tano kwa sasa hazina majina. Ni muhimu zipewe majina ya kutumiwa shuleni na ya kutumiwa na umma." (ILC Bulletin Na. 1, 1930: 10). Je, kama mwanakamati ungetoa mapendekezo gani, hasa unapojua kwamba baadhi ya wasemaji wa Kiswahili walikuwa wakitumia maneno mengi kama vile "peni la senti kumi" na "peni la senti tano"? Maneno nusu shilingi kumaanisha senti hamsini, peni kumaanisha senti kumi na nusu peni kumaanisha senti tano yalikuwa ni afadhali kuliko deka na pente kutoka Kigiriki na ashara na hamsa kutoka Kiarabu ambayo yalipendeke- zwa kumaanisha senti kumi na senti tano. Maelezo ya hapo juu yanaonyesha baadhi ya shida zilizowakumba wasanifishaji wa Kiswahili mapema katika shughuli za usanifishaji. Kufanikiwa kwao kulitokana na jitihada za pamoja za misheni wa madhehebu mbalimbali pamoja na msaada na ushirikiano wa serikali za kikoloni za Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar. Mashauriano mengine mengi kama hayo yaliyojadiliwa hapo juu yalifanywa na matokeo yake yalikuwa ni kusanifishwa kwa maneno mengi ya Kiswahili. Kamati ilitoa orodha za maneno ya Kiswahili, ikayajadili, kisha ikachapisha yale yaliyokubaliwa kama Kiswahili sanifu. Katika jarida la ILC Bulletin Na. 9 la Oktoba 1935, Kamati inajadili orodha ya maneno ya Kiswahili yenye asili ya Kibantu na kutoa maelezo ya chanzo 45 chake. Orodha hiyo inayo maneno kama vile kanzu, shamba na kizibao. Katika Jarida hilo Johnson pia anajadili chanzo cha baadhi ya maneno naye Kasisi Hellier anayo orodha ya msamiati anaoupendekeza wa vipimo na mizani. Katika Jarida la mwaka uliofuata, I.L.C. Bulletin Na. 10 ya 1936 kumbukumbu tatu za J. W. T. Allen, Broomfield na F. Johnson zimechapishwa. Kumbukumbu hizo ni maoni ya Kamati kumjibu Clement M. Doke aliyetoa mapendekezo kuhusu jinsi ya kugawanya maneno katika kitabu cha Bantu Linguistic Terminology. Mapendekezo ya Doke yangesababisha kuwe na maandishi ya maneno kama vile waSwahili, muIngereza, mUngu, waDaudi na kwamtu badala ya Waswahili, Mwi- ngereza, Mungu, wa Daudi na kwa mtu. Kamati ilikataa mapendekezo ya Doke katika makala hayo na mengine yaliyochapishwa katika jarida la 1937. Masuala ya kisarufi pia yalijadiliwa na kuchapishwa katika jarida la Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Kwa mfano matumizi ya KA na KI yalijadiliwa na A. B. Hellier katika jarida la 1931 naye F. Johnson alijadili kinyume cha kiambishi "kuto-" katika jarida la 1933. Katika makala yake, Johnson anatoa rai kwamba neno kutoenda latokana na maneno kutoa na kwenda. Naye mwanakamati Ronald Snoxall anapinga maelezo ya Johnson na kumsahihisha kwa kueleza kwamba to katika neno kutoenda ndicho kiungo cha kinyume. Masuala mengine kuhusu kusanifishwa kwa Kiswahili yalishughulikiwa na Kamati pia, na matokeo yake yakachapishwa kwenye jarida. Masuala hayo yalikuwa ni pamoja na kutoa sababu za kutumiwa kwa irabu zikifuatana kulikoelezwa na Broomfield mnamo 1931; kuhesabu katika Kiswahili na A. B. Hellier 1932; alfabeti za Kiswahili na A. B. Hellier 1934; mjadala kuhusu alama za kuwakifisha; pamoja na kukadiriwa kwa vitabu vya shule vya wakati huo, kulikofanywa na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Mnamo mwaka 1934 ilibidi Kamati ipime kazi yake. Jambo hili lilisababishwa na kumbukumbu "Kiswahili cha Kisasa" iliyoandikwa na afisa mmoja wa Idara ya Elimu, Kenya. Baada ya kuipokea kumbukumbu hiyo, katibu alimuomba Broomfield aijibu. Kumbukumbu hiyo, majibu yake, pamoja na dondoo la gazeti Al-Islah la Mombasa zilizochapishwa katika Jarida, ILC Bulletin la 1934 tayari zimejadiliwa katika sura ya pili. Baadhi ya makala zilirudiwa katika matoleo ya Jarida ya hapo mwanzo. Kwa mfano, makala ya Snoxall kuhusu kitendo kutoa, ilichapishwa katika Jarida namba 6 la 1933 na kurudiwa tena katika Jarida namba 8 la 1935. Makala iliyojadilia suala la a mbili katika maandishi ya Kiswahili katika 46 Jarida namba 2 la 1931, ilichapishwa tena katika jarida Bulletin namba 6, la 1933. Kuna sababu mbili za kuchapisha upya makala hayo. Sababu ya kwanza ni kuwa ILC Bulletin lilikuwa jarida changa lililokuwa likitoa nakala chache, na lilikuwa na wasomaji wachache na waandishi wa makala za kuchapishwa hawakuwa wengi pia. 24* Inawezekana kwamba watu ambao wangeandika makala ya kuchapishwa kwenye jarida walikuwa na kazi nyingi ya kuandika na kutafsiri vitabu vya Kiswahili ili kutosheleza mahitaji ya vitabu hivyo. Sababu ya pili ni kwamba matolea machache ya kwanza hayakuchapishwa kama vitabu bali yalipigwa taipu na kutolewa nakala. Jarida la kwanza lililochapishwa kama kitabu lilikuwa toleo namba 6 la Oktoba 1933. Kupigwa chapa huko kulipoanza, ndipo baadhi ya makala zilipoanza kuchapishwa upya ili ziweze kuwafikia wasomaji wengi zaidi. Yale yaliyojadiliwa hapo juu ni baadhi ya mambo muhimu ya kupanga lugha kitaaluma, ambayo hujulikana pia kama "uhandisi wa lugha", uliofanywa na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Jarida hali- kuchapishwa katika mwaka 1937 kutokana na kifo cha Frederic Johnson aliyekuwa katibu wa kwanza wa Kamati. Johnson alifariki akiwa Aden mnamo mwezi Machi, 1937. 3.2 Wakati wa vita Wazungu wengi, baadhi yao wakiwa misheni waliondoka Afrika Mashariki kwenda nchi zao mbalimbali za Ulaya kujiunga najeshi wakati wa vita vya pili vya dunia. Kwa sababu hizo hizo na kwa kuwa ilikuwa hatari kusafiri wakati wa vita, Wazungu wengi waliotarajiwa kujiunga na misheni kadha hawakuwasili. Kulikuwa na ukosefu wa pesa kwa sababu ya kugharamia vita. Wanafunzi wa Afrika Mashariki waliopevuka pamoja na wengi wa walimu wao walijiunga na jeshi lililokuwa likilinda Afrika Mashariki. Kwa sababu hiyo shuguli zote za kielimu zilififia kama inavyodhihirishwa na maelezo yafuatayo ya Mkurugenzi wa Elimu, Kenya mnamo 1942. "Mahitaji ya viongozi wa jeshi, ya Waafrika ambao walijua kusoma na kuandika, yalikuwa mengi kama yalivyokuwa katika miaka ya vita iliyotangulia. Idadi ya vijana walioacha shule za misheni na za serikali kabla hawajamaliza masomo yao ilikuwa kubwa. Mshahara mkubwa unaolipwa na jeshi pia umesababisha walimu wa Kiafrika wengi wa shule za msingi kuacha kazi za kufundisha." 25* -- 24* Hapo mwanzo bila shaka nakala zilikuwa chache sana. Kufikia 1953 nakala zilizokuwa zikichapishwa zilikuwa kati ya 500 na 600. 25* Kenya Education Department Annual Report 1942, Government Printer - Nairobi, (pia tazama Lugumba na Ssekamwa 1973: 19). 47 Hali katika nchi zingine za Afrika Mashariki ilikuwa mbaya pia. Nchini Uganda, kwa mfano, vijana wa kiskauti wa shule walitumiwa kusaidia askari polisi katika kulinda mji mkuu Kampala. Baadhi ya shule, kama vile shule ya kilimo ya Gulu ilibidi ifungwe baada ya Mzungu aliyekuwa akiisimamia kuambiwa arudi kwao Ulaya. (Lugumba na Ssekamwa 1973: 65). Kuhusu Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki Whiteley 1969, anadai kwamba hakukuwa na kazi nyingi iliyofanywa na Kamati. Hata hivyo maoni ya Whiteley yanapingwa vikali na mafanikio ya Kamati ya wakati huo. Jarida la Kamati ILC Bulletin lilichapishwa kila mwaka wakati wa vita, vitabu vingi vilichapishwa, miswada ilipokewa na kushughulikiwa, ku- likuwa na mashindano ya uandishi wa Kiswahili na vitabu kadha vilitafsiriwa. Pia jitihada zilifanywa kukisanifisha Kiswahili cha Zaire ili kiwe sawa na Kiswahili cha Afrika Mashariki. Baadhi ya mikutano ya Kamati haikuweza kuitishwa wakati wa vita na bila shaka kama haku- ngekuwa na vita Kamati ingefanikiwa zaidi kati ya 1939 na 1945. Maelezo yafuatayo yanaonyesha kwamba hatuwezi kudunisha mafanikio ya Kamati katika miaka hiyo ya hatari. Jarida la lLC Bulletin Na. 13 la 1959 linatoa orodha ya maneno na mapendekezo ya matumizi yake ili wasomaji wa jarida watoe maoni yao. Ni muhimu kutaja kwamba kamati inapendekeza majina kama vile kabila, chupa na jumba yatumiwe katika ngeli za 9/10 (Ngeli ya N, kwa mfano: Kabila hii badala ya kabila hili). Kamati ilifikiria kwamba, endapo majina hayo yangetumiwa kama majina ya ngeli za 5/6 JI-MA), yangevuja sifa ya maana kwa kuleta hisia mbaya hivi kwamba neno makabila lingeleta maana ya ushenzi, hali neno majumba lingeonyesha maana ya nyumba kubwa zisizo na umbo zuri lililolingana. Katika maelezo hayo kamati ilitilia maanani sana uwezo wa ngeli za 5/6 wa kuleta hisia mbaya ya jina ambalo si muhimu likilinganishwa na maana ya kuonyesha ukubwa wa jina. Maoni haya ya kamati kuhusu sarufi ya Kiswahili yalipingwa. Bwana E. B. Huddon aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mashariki nchini Uganda, katika I.L.C. Bulletin Na. 14 ya 1940 anata- hadharisha kwamba, Wazungu wanaweza kupendekeza kutumia kwa kabila hii (ngeli ya 9) badala ya kabila hili (ngeli ya 6), Dachi-Madachi badala ya Dachi-Wadachi nk. lakini itachukua muda kujua ni matumizi gani yatakayoshika. Anatoa mfano wa vile mabibi na mabwana yanavyo- tumiwa kama wingi wa bibi na bwana na wala maneno ambayo tungetarajia, ambayo ni, wabibi na wabwana hayatumiki kamwe. Pia tamko wake zake ni matumizi sahihi hata ingawa hayafuati kanuni za viambishi vya ngeli. Majadiliano haya pamoja na ya matumizi ya viambishi m-wa kuonyesha 48 wingi yanaendelea katika matoleo kadha yajarida la I.L.C. Bulletin. Kasisi Canon A. B. Hellier katika jarida la 1941 kwa mfano, anasisitiza kwamba kamati inao wajibu wa kukomesha matumizi yasiyokuwa sanifu katika shule licha ya matumizi ya watu. "Ikiwa baadhi ya watu wataamua kusema Mataliana badala ya Waitaliano inasikitisha, lakini hatuwezi kuwazuia; lakini tunaweza kuzuia matumizi kama hayo yasiingie katika vitabu vya shule". Vile vile Hellier anasema kwamba, Kamati haitashawishiwa kuandika Waingereza na Waitaliano kama Wengereza na Wetaliano ati kwa sababu baadhi ya ai huwa e. 26* Hellier anasema kwamba maneno kama vile rafiki adui na mke ni baadhi ya maneno ambayo hayafuati kanuni za viambisho vya ngeli katika hali ya wingi. Anajadili neno mbona kwa kirefu na kudai kwamba ni sawa na tamko 'kwa nini?'. Hakubaliani na maelezo ya Bull na Snoxall ya hapo awali kwamba neno mbona, chanzo chake ni navona. Anasema kwamba nivona ni chanzo kinachofaa zaidi na kwamba ndilo neno lililotangulia mbona. Katika jarida namba 14 mapendekezo ya maneno ya Kiswahili ya msamiati uliochapishwa katika jarida namba 13 yanatolewa; kisha maneno yaliyokubaliwa ambayo yamesanifishwa yamechapishwa katika jarida I.L.C. Bulletin Na. 14 la 1941. Ningependa kutaja kwamba Kamati iliona ni muhimu maneno mlangobahari na pembemraba yaandikwe hivyo badala ya kuyagawa pembe mraba na mlango bahari. Kamati pia ilipendekeza maneno ya lugha zingine za Kiafrika yatumiwe walipokosa maneno ya Kiswahili yanayofaa. Kwa mfano, neno lililo- sanifishwa la ugonjwa wa ngombe 'ndigano' latokana na neno la Kimasai 'oldikana'. Pia neno ugonjwa mwingine wa ngombe 'kimeta' ni la Kihehe kinachozungumzwa katika Wilaya ya Malangani, Tanzania. Labda neno la homa mbaya ya matumbo lililosanifishwa 'entereki' ni la Kimasai pia. Jarida la I.L.C. Bulletin Na. 16 la 1942 lilichapisha matokeo ya uchunguzi pamoja na mapendekezo ya Kamati kuhusu mambo kadha ya sarufi, matumizi na msamiati. Jarida namba 17 la 1943 pia lilichapisha matokeo ya uchunguzi wa sarufi, matumizi, msamiati na othografia. 27* Jarida namba 18 la 1944 lilimkumbuka Dkt. Ludwig Krapf na kumsifu kwa kazi zake za uchunguzi wa Kiswahili na uandishi wake aliouanza miaka mia moja iliyopita. Mwaka 1944 uliadhimisha miaka 100 tangu Krapf afike Afrika Mashariki. Mbali na orodha za maneno ya Kiswahili na Kiingereza, maana, na matumizi yake, makala fupi pia zilichapishwa. Mwisho kabisa Kamati inawashukuru wanafunzi wa Chuo cha Serekali -- 26* Tazama sehemu ya othografia, sura ya pili. 27* Ili kupata mengi kuhusu othografia soma sura ya pili. 49 cha Uchapishaji cha Dar es Salaam pamoja na mwalimu wao kwa kuchapisha Jarida la I.L.C. Bulletin kwa miaka mingi. Makao makuu ya Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki yalihami- shwa kutoka Dar es Salaam kuenda Nairobi mnamo mwaka 1942. Wasomaji wa Jarida walijulishwa anwani mpya ya Kamati katika toleo namba 16 la mwaka huo. Katika jarida namba 17 la 1943 katibu wa Kamati anawashukuru wasomaji wa jarida kwa kutoa maoni na mape- ndekezo yao kwa wingi kuhusu Kiswahili. Alisema kwamba maoni na mapendekezo hayo yalikuwa mengi sana hivi kwamba hayangechapishwa yote au kujibiwa moja moja. Yaonekana kwamba labda vita viliwafanya wananchi wa Afrika Mashariki watambue kwamba walikuwa ni jamii moja na kwamba Kiswahili ndicho kingewaunganisha na kuwawezesha kujitambua. Inaripotiwa kwamba katika mwaka uliotangulia (1942), Kamati iliende- lea kuwasiliana na idara za utangazaji za Kenya na Tanganyika pamoja na jeshi kuhusu uchapishaji wa vitabu pamoja na mafunzo ya Kiswahili kwa wanajeshi. Katibu aliendelea kuwasiliana na nchi zingine kwa kuandikiana barua kwa kuwa vizuizi vya wakati wa vita havikumruhusu kusafiri. Anarekodi mwamko mpya wa kukipenda Kiswahili uliothibitishwa na barua nyingi alizozipokea kutoka kote katika Afrika Mashariki. Katibu Ratcliffe anaandika hivi: "Usafiri wa wanajeshi na kuongezeka kwa njia za usafiri kumeongeza sana mahitaji ya othografia sanifu." (I.L.C. Bulletin Na.17 la 1943: 14). Moja kati ya shughuli kubwa sana za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilikuwa ni kuhakikisha kwamba wanajeshi wamefunzwa Kiswahili. Jeshi liliwaendea Kamati, nayo Kamati iliwashauri vilivyo. Sera ilinuia kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya wanajeshi kote katika Afrika Mashariki. Baadhi ya maafisa vijana wa Kiingereza ilisemekana hawakupenda kujifunza Kiswahili kwa kuwa hawakuona umuhimu wa lugha hiyo baada ya vita (Snoxall: mahojiano na mwandishi). Waafrika wote waliojiunga na jeshi ilibidi wajifunze Kiswahili, ili waweze kuwasiliana na wanajeshi wenzao waliokuwa wakitumia lugha tofauti. Kwa hivyo, Kiswahili kikawa lugha ya wanajeshi. Shule zilizokuwa zikisomesha watoto wa wanajeshi pia zilitumia Kiswahili. (Kwa maelezo zaidi, tazama Sura ya Tano). Kimoja kati ya vitabu vilivyotumika sana ni Upcountry Swahili Exercises kilichoandikwa na Breton. Lakini kitabu kilichotayarishwa na kuchapishwa na sehemu ya Elimu ya Jeshi la Afrika Mashariki ili kusomesha wanajeshi Kiswahili kiliitwa A Kiswahili Instruction Book for the East African Command. 50 Kiswahili walichofunzwa wanajeshi kilikuwa cha mwanzo tu. Hata baadhi ya wanajeshi waliokijua Kiswahili vizuri hawakukifikiria kuwa ni Kiswahili safi. Mmoja wao ni C. A. R. Savage aliyekuwa mwanajeshi huko Jinja, Uganda. Bwana Savage aliyekijua Kijaluo, Kiacholi na Kiswahili vizuri alikuwa mwanakamati wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kutoka Uganda. Siku moja mabwana Savage na Snoxall wakiwa safarini kwenda Nairobi kwa gari la moshi kuhudhuria mkutano wa Kamati, Bwana Savage alitunga ubeti ufuatao wa Kiingereza kukieleza Kiswahili cha bara kama kile walichofunzwa wanajeshi: "Natives who speak Swahili here Have never heard of Bishop Steere Their primitive upcountry speech No rules of Grammar serves to teach Sometimes really zealous learner Some concords may pick up from Werner But "Safi" stuff is heard alone When Ratcliffe talks to Elphinstone." 28* Tafsiri: Wenyeji wanaoongea Kiswahili huku Hawajamsikia Askofu Steere Lugha yao ya bara isiyostaarabika Haifuati kanuni za sarufi Mara nyingine mwanafunzi mwenye bidii Hujifunza viambisho vitabuni vya Werner Lakini lugha iliyo safi husikika tu Ratcliffe azungumzapo na Elphinstone. Kamati ilianzisha ushirikiano na Belgian Congo (Zaire) katika shughuli za kuleta pamoja maendeleo ya Kingwana na ya Kiswahili sanifu (tazama Sura ya Pili). Vitabu vinane vipya vilichapishwa mnamo 1942. Vitabu vingi vilipigwa chapa na misheni za Afrika Mashariki. Pia miswada ishirini na tano ilipelekwa Kamati, ikiwa ni ya masomo mbalimbali kama vile kilimo, mazoezi ya viungo na mbinu za kusomeshea. Baadhi ya miswada ilipelekewa Kamati ili kamati iikague na ithibitishe kwamba othografia ilikuwa sanifu, nayo miswada mingine ilipelekewa Kamati ili Kamati iisanifishe na kuichapisha ikiamua kufanya hivyo. Kwa sababu ya vita, katibu anaeleza kwamba kulikuwa na upungufu wa karatasi na kwamba ilichukua muda -- 28* Snoxall, mahojiano na mwandishi, Februari 10, 1984. Sehemu moja ya ubeti huo pia yapatikana katika Whiteley, 1969: 79). 51 mrefu kutuma miswada Uingereza ili ichapishwe. Kama vile nilivyotaja katika mwanzo wa sehemu hii, mashindano ya uandishi wa Kiswahili yaliiendelea wakati wa vita. Zawadi mbili za kwanza za uandishi wa insha ya kuelekezwa zilishindwa na Wakenya wawili kutoka shule za wavulana za Alliance na Mangu. Zawadi ya tatu ilishindwa na mtu mmoja kutoka Masasi, Tanganyika. Katika shindano la uandishi wa insha ambapo mwandishi hakuelekezwa, zawadi ya kwanza na ya tatu zilishindwa na waandishi kutoka Makerere, Uganda, nayo zawadi ya pili ilishindwa na mwandishi kutoka Dar es Salaam, Tanganyika. Mashindano mengine yalikuwa ni mashindano ya uandishi na mashindano ya insha ya wanafunzi wa shule za Wazungu. Akizungumzia ufasaha wa lugha mhariri wa jarida anasema kwamba Kiswahili kilichotumiwa chaonyesha kwamba waandishi walikuwa wanaimudu lugha, na walijieleza vizuri. (I.L.C. Bulletin Na. 17, 1943: 16). Katika jarida, I.L.C. Bulletin Na. 18 la 1944, ripoti ya mwaka uliotangulia inaonyesha kwamba mnamo 1943 kulikuwa na mawasiliano na makundi ya Afrika Mashariki na ya kimataifa ambayo yangesaidia katika utoaji wa vitabu vya fasihi ya Kiswahili. Katibu alitembelea mikoa ya Mashariki, Kati na Kaskazini ya Tanganyika kukadiria mahitaji ya vitabu vya Kiswahili katika shule na vituo vingine vya elimu. Vitabu kumi vya Kiswahili vilichapishwa na kamati ilipokea miswada ishirini na nane kuichunguza. Kamati yenyewe iliongezea orodha hii kwa kutafsiri vitabu vinne. Mnamo 1943 Waafrika walioshiriki kwenye mashindano ya uandishi wa Kiswahili, wakiwa ni pamoja na askari jeshi walikuwa 215, lakini hakukuwa na yeyote aliyeshiriki kutoka shule za serikali za watoto wa Kizungu. Kitengo cha Kamati kilichokagua mashindano hayo kiliridhika kwamba mashindano hayo yalisaidia katika kueneza ujuzi wa kusoma na kuandika. Miswada iliyopokelewa ilionyesha kukua kwa vipawa vya uandishi ambao ulihitajika sana kwa kuwa kulikuwa na upungufu wa fasihi ya Kiswahili iliyoandikwa na Waafrika. Kati ya wale walioshinda zawadi katika mashindano ya 1943 wali- kuwemo Maurice Otunga wa Holy Ghost College, Mangu, Kenya na Josiah Muli wa Alliance High School, Kikuyu, Kenya. Katika mashindano ya 1944, Robert Matano wa Alliance High School, Kikuyu, na Moses Kinyanjui wa Holy Ghost College, Mangu, pia walishinda zawadi. Ripoti ya 1944 ilichapishwa katika I.L.C. Bulletin Na. 19 ya 1945. Ripoti hiyo inataja kwamba Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilikumbwa na matatizo. Hata hivyo jarida halikueleza aina ya matatizo hayo. Labda kamati ilikuwa na wasiwasi kuhusu pendekezo la Waku- rugenzi wa Elimu wa Serikali za Afrika Mashariki kwamba Kamati 52 iunganishwe na halmashauri ya uchapishaji - East African Literature Bureau - iliyonuiwa kuanzishwa. Miswada iliyoendelea kupokewa na Kamati iliwapa ofisi ya katibu pamoja na wahariri wa Kamati kazi za kutosha za kufanya mwaka huo. Wahariri hao walipongezwa kwa kufanya kazi kwa bidii, licha ya upungufu wa wafanyakazi wakati wa vita. Vitabu kumi vipya vilichapishwa mnamo 1944 na miswada kumi na tisa ilipokelewa. Kwa upande wake kamati ilitafsiri vitabu kumi na vinne. Kazi iliyofanywa na Kamati wakati huu wa vita, kulipokuwa na upungufu wa pesa na wafanyakazi ilikuwa nyingi na ya kushangaza. Kati ya 1942 na 1944, kipindi kifupi cha miaka mitatu Kamati iliripoti kwamba ilichapisha jumla ya vitabu ishirini na vinane (28). Ilikuwa imetafsiri vitabu kumi na vinane (18), pamoja na kushughulikia miswada sabini na miwili (72). Vita havikupunguza usomaji wa vitabu, bali vitabu viliuzwa kwa wingi zaidi. Ratcliffe anaandika kwamba "ingawaje ni wakati wa vita, vitabu vya Kiswahili havijawahi kununuliwa kwa wingi jinsi hii". (Ratcliffe I.L.C. Bulletin Na. 18, 1944: 4). Mnamo 1943 pekee, Ratcliffe anaripoti kwamba zaidi ya vitabu 330,000 vya Kiswahili vilivyochapishwa huko Uingereza viliuzwa katika Afrika Mashariki, mbali na nakala 70,000 za vitabu vilivyochapishwa Afrika Mashariki. Kamati inapendekeza Kiswahili kitu- miwe katika kuelimisha watu kwa wingi badala ya kutumia lugha za kwanza zilizokuwa zikipendekezwa, ambazo zilitumiwa na idadi ndogo ya watu wa kabila moja moja. Jarida la I.L.C. Na. 19 la 1945, lilichapishwa mwezi Novemba wa mwaka ambao vita vya pili vya dunia vilimalizika. Jarida linashangilia kukomeshwa kwa uhasama huko Ulaya. Kumalizika kwa vita kulileta mabadiliko mengi. Yasemakana kwamba Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilipewa miradi mipya na kwamba mambo yaliyokuwa yakitiliwa mkazo kuliko hapo awali yalikuwa ni kusoma na kuandika pamoja na ukuzaji wa lugha za kwanza. Mhariri wa Jarida anasema hivi - "Mengi yamesemwa na yangali yanasemwa kuhusu kuhitajika kwa Kiingereza kama lugha ya kusomesha masomo mengine, lakini itachukua muda mrefu kabla Kiingereza hakijakuwa tiba ya Waafrika ya kutojua kusoma na kuandika". (I.L.C. Bulletin Na. 19, 1945: makala ya mhariri). Kutiliwa mkazo huku kwa Kiingereza na lugha za kwanza mara tu baada ya vita, kulikuwa ndiyo mwanzo wa kudhoofika kwa shughuli za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Usanifishaji wa Kiswahili ulikuwa umeanza kushuka kutoka upeo wake. Kamati ilitambua hivyo na ikajaribu kuonyensha kwamba Kiingereza hakingeweza kutumiwa ku- pigana na hali ya kutojua kusoma na kuandika. Ilibidi lugha za Kiafrika zitumiwe. Kwa kuwa ingekuwa ghali sana kukuza lugha nyingi za kwanza, 53 ingekuwa bora Kiswahili kitumiwe. Kiswahili kilikuwa kimejitambulisha kama lugha sanifu iliyotumika kote katika Afrika Mashariki. Kilikuwa na maandishi mengi yaliyokuwa yakiongezeka kwa wingi, na hiyo ndiyo sababu Kamati ikaonelea kwamba Kiswahili pekee ndicho kinachofaa kwa elimu ya watu wengi. Afisi ya Kikoloni haikufuata mapendekezo ya Kamati. Kwao lilikuwa suala la kisiasa. Ilibidi Wakoloni watumie mbinu mpya kuwatawala Waafrika ambao walikuwa wamepevuka kisiasa baada ya kushiriki katika vita. Waafrika walikuwa wameutambua udhaifu wa Wazungu wakati wa vita. Ilikuwa wazi kwao kwamba iwapo wangeshirikiana wangeweza kupinga utawala wa kikoloni. Watawala wa kikoloni walikuwa na hamu ya kutumia mgawanyiko wa lugha za kwanza ili kuwatenganisha Waafrika. Kuendelea kutumiwa kwa lugha moja ya Kiswahili kungeleta matokeo yaliyo kinyume cha yale yaliyotarajiwa, kwa kuwa kungewaunganisha Waafrika. Kiingereza haki- ngekuwa na matokeo kama hayo kwa kuwa kingewaunganisha Waafrika wachache walioelimika, ambao hawangekuwa tisho kubwa kwa serikali ya kikoloni. Sera hii mpya ya kupunguza mkazo wa Kiswahili ilijitokeza na kuiudhi Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na bila shaka ndiyo Jarida linayoigusia linapotaja kwamba Kamati ilikumbwa na matatizo fulani. 54 Sura ya Nne 4.0 Kamati baada ya vita 4.1 Kipindi cha Nairobi (1946-1952) Tayari tumetaja kwamba kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (I.T.L.C.) ilihamisha makao yake makuu kutoka Dar es Salaam hadi Nairobi mnamo mwaka wa 1942. Sehemu hii inahusu maisha ya kamati jijini Nairobi baada ya vita vikuu vya pili vya dunia kuanzia mwaka 1946 hadi 1952. Baada ya kukaa Nairobi, makao makuu ya kamati yalihamishwa hadi Kampala. Jarida la I.L.C Bulletin halikuchapishwa mnamo mwaka wa 1946. Mkutano wa kwanza wa Kamati yote, tangu vita vianze mwaka 1939, ulikuwa mjini Nairobi tarehe 4 na 5 Machi mwaka 1946. Kama ilivyo- jadiliwa katika Sura ya Tatu hakukuwa na mikutano ya kamati yote wakati wa vita. Mikutano iliyokubaliwa ilikuwa ni ile kitengo cha kamati ambacho kilihudhuriwa na wasomaji, mwenyekiti na katibu. Kitengo kilifanya uchunguzi wa lugha na kazi zingine kama vile ukaguzi wa mashindano ya uandishi. Kama ilivyotarajiwa mabadiliko kadha yalikuwepo hasa kuhusu uanachama wa kamati baada ya vita. Kamati ilipokutana mwaka 1942 Wakurugenzi wote wa Elimu kutoka Tanganyika, Uganda, Kenya na Zanzibar walikuwa wapya. Kwa hivyo walikuwa wakihudhuria kikao cha kamati kwa mara yao ya kwanza. Wasaidizi wa wahariri wa Kiafrika kutoka nchi zote nne, pia walihudhuria kikao cha Kamati kwa mara yao ya kwanza. Mbali na mabadiliko haya, pia kulikuwa na mabadiliko katika ajenda ya mkutano ambayo ilihusu zaidi masuala ya lugha zingine za Kiafrika kuliko Kiswahili. Kama itakavyojadiliwa kwa kirefu katika Sura ya Tano, Kipindi hiki cha Kamati, baada ya vita kilikuwa na mabadiliko mengi kuhusu sera ya lugha ambapo Kiingereza na lugha kadha za Kiafrika zilianza kutiliwa mkazo badala ya Kiswahili. Jarida la I.L.C. Bulletin Na. 20 lilichapishwa mwaka 1947. Kama ilivyokuwa kawaida, jarida lilikuwa na maoni mengi kuhusu lugha kutoka kwa wasomaji. Mwandishi mmoja ambaye makala yake yametokea katika majarida ni A. N. Tucker kutoka School of Oriental and African Studies, Chuo Kikuu cha London. Katika maandishi yake yanayohusu mtindo wa kuandika lugha, anasema kwamba lugha zingine za Kibantu zatakikana zitumie mtindo wa kuandika Kiswahili kama kielekezo. Hata hivyo 55 anatahadharisha kuhusu miundo tofauti ya baadhi ya lugha za Kibantu kama vile kuwepo na irabu saba badala ya tano za Kiswahili na hali ya kuwa na irabu mbili zilizofuata katika neno moja (ambapo irabu hizo zinasababisha neno liwe na maana tofauti). Tucker anatahadharisha kwamba tofauti kama hizo zitiliwe maanani wakati wa kuunda mtindo wa kuziandika lugha za Kibantu. Katika mwaka wa 1946 uliotangulia, jumla ya miswada ishirini na mbili ilikabidhiwa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ili iishughulikie. Vitabu kumi na moja vya Kiswahili vilichapishwa na vitabu vingine vitano vikatafsiriwa na wafanyakazi wa afisi ya katibu mtendaji. Mashindano ya uandishi wa Kiswahili yaliendelea kuwavutia washiriki wengi kutoka shule za Kiafrika hata ingawa hakukuwa na walioshiriki kutoka shule za Wazungu. Jarida la I.L.C. Bulletin halikuchapishwa katika miaka ya 1948, 1949 na 1950 ambapo mabadiliko kadha yalikuwa yakitendeka. Licha ya hivyo, jumla ya vitabu vipya ishirini na sita vya Kiswahili vilichapishwa wakati huo. Pia wahariri wa Kamati pamoja na katibu walikabidhiwa miswada 156 (mia moja hamsini na sita) kuishughulikia. Mnamo mwezi wa Disemba mwaka wa 1949 Rev. B. J. Ratcliffe katibu wa Kamati alistaafu. Rev. Ratcliffe alifika Afrika ya Mashariki kwa mara ya kwanza mwaka 1899 alipoanza kazi za kidini katika wilaya ya Tana River nchini Kenya. Uhusiano wake na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ulianza hapo mwaka 1930 alipochaguliwa kuwa mhariri kuwakilisha Kenya. Alishikilia wadhifa huo hadi mwaka 1937 alipo- ajiriwa kuwa katibu baada ya kifo cha Frederick Johnson aliyekuwa katibu wa kwanza wa Kamati. Shughuli kubwa aliyoifanya Ratcliffe kama katibu ilikuwa ni kuha- kikisha kwamba kamusi mbili Standard Swahili-English na English- Swahili zimechapishwa. Kamusi hizo zilikuwa zimehaririwa na Frederick Johnson kutegemea msingi uliowekwa katika kamusi za Madan. Ratcliffe aliweza kutetea vilivyo, matumizi ya msamiati wa lahaja tofauti za Kiswahili. Kufuatia juhudi zake, msamiati wa lahaja za Kenya, hasa Kimvita uliweza kuingizwa kwenye kamusi - jambo ambalo halinge- dhaniwa kwamba lawezekana mwaka 1928. Baada ya Ratcliffe kustaafu, mkurugenzi wa East African Literature Bureau, Bwana C. G. Richards alishikilia wadhifa wa katibu kwa muda. Baada ya Richards, Bwana H. E. Lambert alichaguliwa kuwa kaimu wa katibu hadi mwezi wa Agosti 1952 wakati W. H. Whiteley alipouchukua uwadhifa wa katibu. Wakati jarida la I.L.C. Bulletin la mwaka wa 1951 lilipochapishwa, tayari Kamati ilikuwa imeundwa upya. Kamati ilibadilisha jina kutoka 56 lnter-Territorial Languages (Swahili) committee (I.L.C.), likawa East African Inter-Territorial Language (Swahili) Committee (E.A.I.L.C.). Tangu Kamati hii ya Kiswahili ya Afrika Mashariki iundwe mwaka 1930, ilikuwa chini ya (mamlaka ya ) halmashauri ya Magavana wa Afrika ya Mashariki. Kwanzia Januari moja mwaka 1948 Kamati ilianza kuwa chini ya tume ya East African High Commission. Katika mwaka wa 1950 kulikuwa na mkutano uliohudhuriwa na maafisa wakuu wa Kamati kutoka nchi zote za Afrika ya Mashariki pamoja na Bwana C. G. Richards aliyewakilisha halmashauri ya uchapi- shaji wa vitabu - East African Literature Bureau. Mwenyekiti wa mkutano huo alikuwa ni afisa tawala wa East African High Commission. Mkutano huo uliitishwa kujadili kazi za Kamati tangu kuanzishwa kwa East African Literature Bureau. Ilikubaliwa kwamba Kamati ingeendelea kuwepo kama chombo cha lugha ambacho ni tofauti na East African Literature Bureau. Ilikubaliwa kwamba Kamati ingeendelea kujihusisha zaidi na uchunguzi wa lugha na somo la Kiswahili. Kamati pia ingebakia kuwa mamlaka ya juu kuhusu uandishi na uchapishaji wa vitabu vya Kiswahili. Nayo halmashauri ya East African Literature Bureau ilipewa mamlaka ya utoaji na uchapishaji wa vitabu. Kazi hiyo hapo awali ilikuwa ikifanywa na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Pia kazi ya upangaji wa mashindano ya uandishi wa Kiswahili ilikabidhiwa East African Literature Bureau hata ingawa usomaji na utoaji uamuzi wa maandishi hayo ulikuwa ukifanywa na Kamati. Kwa sababu ya ushirikiano huu wa kufanya kazi kati ya Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na halmashauri ya uchapishaji, naonelea ni bora nieleze machache kuhusu East African Literature Bureau. East African Literature Bureau iliundwa mwezi Januari, 1948 kama mojawapo ya huduma zilizotolewa na East African High Commission. Iliundwa baada ya kufanywa uchunguzi ulioagizwa na mkutano wa Magavana wa Afrika Mashariki. Uchunguzi huo ulifanywa kuanzia Julai 1945 hadi 1947. Kwa maoni ya J. W. Chege (1978: 128) East African Literature Bureau ilirithi kampuni ya uchapishaji ya C.M.S. iliyojulikana kama Ndia Kuu Press (Highway Press). Meneja wa kampuni hiyo C. G. Richards, pia ndiye aliyechaguliwa kuwa mkurugenzi wa kwanza wa East African Literature Bureau. Kazi za uchapishaji za Ndia Kuu Press zilichukuliwa na East African Literature Bureau. Makao makuu ya East African Literature Bureau yalikuwa mjini Nairobi, lakini pia kulikuwa na matawi madogo huko Kampala na Dar es Salaam. Tawi la Kampala lilikuwa likihudumia Uganda nalo tawi la Dar es Salaam lilihudumia Tanganyika na Zanzibar. Pia halmashauri hii 57 ilitoa huduma za maktaba kwa kutumia magari yaliyozitembelea shule na miji ya Afrika Mashariki. Huduma hii ya maktaba pia ilitolewa kupitia njia ya posta. East African Literature Bureau ilianzishwa ili kutosheleza mahitaji ya vitabu yaliyokuwa yakiongezeka kwa haraka kati ya Waafrika walio- elimika. Kwa hivyo ilitarajiwa kuchapisha na kutawanya "vitabu vya fasihi kwa watu wa kawaida, vitabu vya lazima vya shule, vitabu vya kilimo na ufundi vya watu wazima, magazeti au majarida, kuwasaidia waandishi wa Kiafrika na kutoa huduma za maktaba. Mahitaji ya Waafrika yangehudumiwa kwanza, lakini pia, halmashauri hiyo ilitakikana ichapishe vitabu vya fasihi kwa Wahindi". 29* Kazi ya uandishi wa vitabu vya lazima vya shule uligawanywa katika sehemu nne. (i) Kuandika na kuhariri miswada ya vitabu vya walimu na wanafunzi ili kutosheleza mahitaji ya ratiba za Idara za Elimu. (ii) Kufanya vivyo hivyo kwa vitabu vya ziada. (iii) Kutafsiri au kukagua tafsiri za Kiswahili, Kiluganda, Kijaluo na Kikikuyu na kufanya mpango wa tafsiri kama hizo nje ya halmashauri kwa lugha zingine zinazohitajika katika elimu. (iv) Kushughulikia miswada ya vitabu vya lazima na maswali kutoka kwa wachapishaji. Sehemu ya uchapishaji wa magazeti ya East African Literature Bureau ilichapisha gazeti la kila wiki lijulikanalo kama Tazama. Gazeti hilo lilikuwa likitolewa zaidi ya nakala 17,000. Tazama lilianza kuchapishwa na East African Standard mwaka 1956. Tafsiri ya Tazama kwa Kiluganda ilikuwa ikichapisha nakala chache sana. J. W. Chege (1978: 30) anayo maoni kwamba vitabu vya East African Literature Bureau vilinuiwa kutosheleza "mahitaji ya kikoloni ya kuko- mesha kutoridhika na ukoloni na kwamba vilichapishwa kufuatia mashauri na kibali cha Baraza la Ushauri". Ushirikiano wa East African Literature Bureau na mashirika ya uchapishaji ya Uingereza kama vile MacMillan, Longman na Thomas Nelson n.k, kwa maoni ya Chege ilikuwa ni hila ya wakoloni ya kumiliki biashara za uchapishaji. Anatoa mifano na tarakimu kuthibitisha dai lake kwamba vitabu vilivyokuwa vikinunulika kwa wingi zaidi vilipewa wachapishaji hao baada ya East African Literature Bureau kuhakikisha kwamba vingenunuliwa kwa wingi katika matoleo ya kwanza. 'Mkurugenzi mkoloni' (C. G. Richards) alifaulu sana kwa hila hii hivi kwamba wakati wa kustaafu 'alipendekeza kwamba East African Literature -- 29* East African Literature Bureau, Annual Report for 1950: 2. 58 Bureau ivunjiliwe mbali kwa kuwa ilikuwa tayari imetimiza kazi zake na kwamba makampuni yaliyomiliki uchapishaji yalikuwa na uwezo wa uchapishaji'. (Chege 1978: 131). Kamati iliyoundwa upya ilikuwa na watu tisa, wawili kutoka kila nchi pamoja na katibu. Idadi hii ilikuwa ndogo sana ikilinganishwa na wanakamati kumi na saba - wanne kutoka kila nchi na katibu. Snoxall hufikiria kwamba kupunguzwa kwa wanakamati ilikuwa ni hatua ya maendeleo. "Ni maendeleo mazuri kwamba uwanachama wa kamati umepunguzwa kuwa kundi dogo la wataalamu wenye bidii na kwamba mashindano ya uandishi na kazi za uchapishaji wa vitabu vya shule zimechukuliwa na East African Literature Bureau" (Snoxall E.A.I.L.C. Bulletin Na. 22, 1952:3). Orodha mpya ya shughuli za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki iliyoundwa upya ilikubaliwa katika kikao cha kumi na tatu (13) cha kamati. Shughuli hizo zilizoorodheshwa hapa chini zilitilia mkazo uchunguzi katika maeneo kama vile fasihi ya Kiswahili na lahaja. Shughuli zifuatazo za Kamati zilikubaliwa: a) Kuandaa vifaa vya kutosha vya kusomesha Kiswahili. b) Kurekebisha na kuchapisha upya makamusi ya Kiswahili kutegemea matokeo ya utafiti. c) Kushirikiana na mabaraza ya lugha kuhusu mitihani. d) Kuwajulisha watu wa Afrika Mashariki mambo yanayohusu hadhi, umuhimu na maendeleo ya Kiswahili kupitia vyombo vya kutawanya habari. e) Kufanya uchunguzi juu ya historia ya Waswahili, lugha, lahaja, uhifadhi na ufafanuzi wa fasihi ya jadi ya Waswahili. f) Kuendelea kuwa na mawasiliano kati ya nchi zinazotumia Kiswahili - Tanganyika, Zanzibar, Kenya, Uganda, Rhodesia ya Kaskazini (Zambia), Nyasaland (Malawi), Somaliland (Somalia), Kongo ya Ubelgiji (Zaire) na Visiwa vya Komoro. g) Kuendelea kuwa na mawasiliano kati ya kamati na mashirika ya kielimu, vyuo, na vyuo vikuu vinavyoshughulikia Kiswahili kama vile Chuo Kikuu cha London, Chuo Kikuu cha Afrika ya Kusini, Leyden, Lourain na Berlin, pamoja na kuvihimiza vyuo vikuu vingine vianzishe somo la Kiswahili. h) Kuhimiza kuanzishwa kwa somo la Kiswahili katika shule za Wazungu na za Wahindi katika Afrika Mashariki ili kuwe na ushirikiano wa kijamii; na ili kuwezesha kupata wanaisimu watakaoweza kufanya uchunguzi wa somo hili katika siku za baadaye. 59 i) Kudondoa makala muhimu kuhusu somo la Kiswahili kutoka kwenye majarida ya vyuo na mashirika yanayohusika na Kiswahili. j) Kuongoza au kukagua usomeshaji wa Kiswahili katika vituo vilivyokubaliwa ili kurekebisha mitindo isiyofaa ya kufunza somo la Kiswahili. k) Kufanya kazi za ukatibu wa kamati za lugha zisizo za Serikali. Orodha ya shughuli za Kamati inayo mambo mengi sana. Kama katibu Whiteley alivyokiri baadaye "Kamati ingeweza kutekeleza michache kati ya miradi iliyoorodheshwa, zaidi kwa kuwa, katibu atakuwa na kazi zingine mbali na ukatibu". (E.A.I.L.C. Bulletin Na. 23, 1953: 7). Taarifa ya mhariri ya Bulletin Na. 21 inatangaza kuajiriwa kwa Bi. D. V. Perrott wa U.M.C.A. ambaye pia ni mwandishi wa kitabu kiitwacho Teach Yourself Swahili, kuwa mhariri wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki huko London. Kazi hii mpya ingemwezesha muajiriwa kuiwakilisha Kamati huko London, hasa katika kuisoma miswada inayochapishwa huko Uingereza. Hapo awali miswada hiyo ilikuwa ikitumwa katika ofisi ya katibu kusomwa. Kuwa na mhariri huko London kulinuiwa kupunguza gharama za kutuma miswada kati ya London na Afrika Mashariki. Toleo la E.A.I.L.C. Bulletin Na. 22 la 1952 lilikuwa na makala muhimu ya somo la Kiswahili. Makala hayo ni pamoja na jinsi ya kusomesha Kiswahili kama lugha ya kigeni iliyoandikwa na Ali Ahmed Jahadhmy, viambishi KA na U iliyoandikwa na J. Williamson pamoja na makala ya H. E. Lambert kuhusu vile tafsiri inavyoathiri Kiswahili. Katika mkutano wa kumi na nne (14) wa kila mwaka uliokuwepo Nairobi Oktoba 17, 1951, Kamati ilijadili mambo kadha kuhusu lugha na katiba pia. Pamoja na hayo kamati ilijadiliana kuhusu uwezekano wa kuyapeleka makao makuu yake huko Kampala katika Chuo cha Makerere. Pendekezo la kuishirikisha Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na Makerere liliwasilishwa kwa mkuu wa Chuo cha Makerere na afisa tawala wa East African High Commission mwezi Januari 1952. Baraza la Chuo lilijadili pendekezo hilo na kulipitisha mwezi Aprili mwaka huo huo. Mapatano hayakuchukua muda mrefu kufikiwa kwa sababu Taasisi ya Ucunguzi wa Shughuli za Jamii ya Afrika Mashariki ya huko Chuoni tayari ilikuwa imeanzisha uchunguzi wa lugha. Katibu mpya Bwana Wilfred Howard Whiteley alikuwa tayari ameajiri- wa kama mchunguzi mwandamizi wa isimu na lugha za Kibantu na Taasisi ya Uchunguzi wa Shughuli za Jamii. Whiteley alijifunza Kiswahili katika School of Oriental and African Studies, Chuo Kikuu cha London 60 kwa miaka miwili. Pia alikuwa amefanya kazi kwa muda wa karibu miaka mitatu kama afisa wa shughuli za jamii huko Tanganyika. Akiwa huko Makerere, Whiteley angeendelea na uchunguzi wake kwa lugha kadha za Kibantu huko Tanganyika mbali na kazi zake za kutoa mihadhara. Mwezi Septemba 1952 katibu mpya, W. H. Whiteley, alishika usukani kutoka kwa katibu wa muda, H. E. Lambert mjini Nairobi. Whiteley aliyahamisha makao makuu ya Kamati hadi Chuo cha Makerere Kampala ambapo kamati iliambatanishwa na chuo hicho mwaka huo huo wa 1952. Whiteley aliposhika usukani kazi nyingi za Kamati zilihusu kutoa idhini ya kuchapishwa kwa miswada baada ya kuisoma na kuirekebisha vilivyo. Mradi mwingine uliokuwa shughuli kubwa ya Kamati, hasa katibu, ni ule wa kuchapisha jarida la E.A.I.L.C. Bulletin ambalo lilikuwa jukwaa la kujadili masuala muhimu yanayohusu Kiswahili. Akiwa Makerere, Whiteley alijikuta na shida ya kufanya kazi zote za ukatibu kwa kuwa, kama tulivyotaja, alikuwa na kazi za uchunguzi na kusomesha pia. Ilikuwa vigumu kwake kufanya kazi hizi zote pamoja na kusoma miswada ipatayo minne kila mwezi ambayo ilipelekewa kamati kuishughulikia. Kwa hivyo Whiteley aliwaajiri wahariri watatu wa muda, kumsaidia. Mmoja alitoka Makerere na wawili walitoka Dar es Salaam. Afisa tawala wa muda pia aliajiriwa ili kuvipanga vizuri vitabu vya maktaba ya Kamati na kufanya mambo mengine kama vile kupanga vizuri faili za Kamati. Shughuli za uchapishaji wa vitabu hazikuwa tena mikononi mwa Kamati, kama tulivyoeleza. Kwa hivyo, kufikia mwaka 1953 waandishi wengi walikuwa wakiipeleka miswada yao moja kwa moja kwa East African Literature Bureau bila ya kupata ithibati ya Kamati. Isipokuwa miswada hiyo iwe ni ya vitabu vya shule, East African Literature Bureau haikutakikana isisitize kuwepo kwa kibali cha Kamati kabla ya kuvichapi- sha vitabu. Kwa hivyo Kamati ililifikiria jambo hili na kuamua kutoa idhini kwa vitabu vichache vilivyochaguliwa kama vile, vitabu vya sarufi na vitabu vya lazima vya kutumiwa shuleni. Kusomwa na Kamati kwa miswada mingine kulikomeshwa. Uamuzi huu uliipatia afisi ya katibu nafasi ya kupumua kwa kuwa uliiondolea kazi ya kuchosha ya kuisoma miswada mingi ambayo baadhi yake haikuambatana na shughuli za kamati mbali na kuwa imeandikwa kwa Kiswahili. Mwaka uliofuata, 30* Whiteley, alijaribu kutoa sababu za msimamo wake mpya kuhusu ithibati kwa kusema kwamba, kusisitiza Kiswahili kiwe na umbo maalum kulisababisha lugha ionekane kama iliyobuniwa kwa kukosa uhalisi wake. -- 30* Tazama E.A.I.L.C. Bulletin Na. 23 ya 1953. 61 4.2 Kipindi cha Makerere (1952-1960) Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilikuwa na makao yake makuu Makerere, Kampala kuanzia mwaka 1952 hadi mwaka 1962. Katika sehemu hii nitajadili shughuli za kamati kufikia mwaka 1960 kwa kuwa shughuli za kati ya mwaka 1960 na 1962 zinahusu zaidi sura ya sita inayojadili kubadilika kwa kamati kuwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Jarida la E.A.I.L.C. Bulletin Na. 23 la 1953 linayo makala ya kurasa ishirini iliyoandikwa na H. E. Lambert kuhusu lahaja ya Kivumba cha kisiwa cha Wasini na jimbo karibu na Vanga katika kusini mwa pwani ya Kenya. Lambert pia anajadili utenzi wa kutekwa kwa mji wa Tumbe na Waswahili (Wavumba) kutoka Vanga pamoja na shairi la kumsifu Mwana Mnga. Maandishi haya yalikuwa ni matokeo ya uchunguzi uliofanywa na Lambert huko Vanga ambacho ni kijiji cha Waswahili cha kusini zaidi nchini Kenya. Shairi hilo la mwisho lasemekana kwamba lilitungwa na mshairi mashuhuri Muyaka, lakini kama Lambert anavyoeleza, hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha au kukanusha dai hili. Kufikia wakati huu, Kamati ilikuwa tayari imeanza kuchunguza zaidi lahaja za Kiswahili. Makala ya Lambert yalikuwa ni mfano tu wa matokeo ya uchunguzi huo. Baadhi ya matokeo ya uchunguzi huo wa lahaja yalichapishwa katika Jarida la E.A.I.L.C. Bulletin lakini mengine yali- chapishwa kama vitabu kama tutakavyoendelea kujadili. Mnamo mwaka wa 1954 jarida lilibadilishwa jina kutoka Bulletin hadi Journal. Pia jina la Kamati lilibadilishwa kutoka jina refu la East African Inter-Territorial Language (Swahili) Committee, hadi East African Swahili Committee. Katika makala ya mhariri jarida la EASC Journal Na. 24 la 1954, Whiteley anaeleza kwamba hapo awali jarida lilikuwa likichapisha taarifa rasmi fupi za habari kwa raia ambayo ni maana halisi ya neno Bulletin. Anasema kwamba neno Journal linafaa zaidi kwa jarida jipya litakalokuwa kubwa kuliko Bulletin na litakalochapisha makala ndefu zaidi zenye kuamsha msisimko wa wasomi ili kuwafanya watoe mchango wao kwa kuandika makala. Kuanzia na toleo la 1954 Whiteley alitarajia matoleo yote ya jarida yawe kielelezo katika makala yote yanayochapishwa. Toleo la 1954 ni mfano bora wa aina ya jarida alilolitaka Whiteley. Lilikuwa na makala ndefu kuhusu vimiliki katika Kiswahili sanifu iliyoandikwa na O. B. Kopoka. Baada ya kupata makala ya Kopoka, katibu ambaye pia ni mhariri wa jarida, alimwuliza H. E. Lambert aandike kuhusu vimiliki katika lahaja huku akitoa mifano kutoka lahaja kadha za Kiswahili. Mwishowe anaongeza makala inayojadili vimiliki katika Kidigo kutokana na maandishi ya Z.M.S. Zani ili kulinganisha na 62 Kiswahili na kukamilisha mjadala huu wa vimiliki. Mbali na vimiliki, jarida hili linayo makala kadha ya uchambuzi wa vitabu. Katika jarida hili la 1954 pia tunafahamishwa kwamba tayari Kamati imeanzisha uchunguzi wa lahaja za Kiswahili pamoja na uchambuzi wa matumizi ya Kiswahili katika magazeti. Katika mkutano wa kumi na saba (17) wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki uliokuwepo kati ya Februari 10 na 12 1954 ilikubaliwa kwamba nakala zote za Jarida la EASC Journal zitakuwa zikiuzwa kuanzia wakati huo. Kabla ya hapo nakala za E.A.I.L.C. Bulletin zilikuwa zikitolewa bure. Jarida la EASC Journal Na. 25 la 1955 limechapisha makala nyingi kuhusu Kiswahili. Makala hizo ni pamoja na ya W. H. Whiteley kuhusu lahaja ya Kimvita, makala ya O. B. Kopoka inayohusu maneno yanayoishia kwa irabu yenye kuonyesha nia inayotazamia na vile yanavyotumiwa katika mashairi ya zamani ya Kiswahili. E. B. Haddon pia anaijadili hiyo nia ya kutazamia katika makala yake. Kurasa zilizobaki za jarida zinazo makala za uhakiki au uchambuzi wa vitabu pamoja na barua za wasomaji. Kujadiliwa kwa undani kwa nia inayotazamia kunatokana na utaratibu mpya wa jarida ulioanzishwa na Whiteley wa kuandika makala ya kitaaluma ya Kiswahili. Matoleo mengine ya jarida yaliyochapishwa wakati Whiteley akiwa katibu wa Kamati yalifanana na hayo yaliyojadiliwa hapo juu. Yaelekea hakukuwa na kiwango kilichowekwa cha urefu wa makala zilizochapishwa. Kati ya zile ndefu sana ni Habari za Wakilindi makala (kitabu) yenye karibu kurasa 50 iliyoandikwa na Abdallah bin Hamed bin Ali Liajjemi na kuchapishwa na EASC Journal Na. 27 1957. Orodha za istilahi au msamiati wa kitaaluma zimechapishwa katika matoleo kadha ya jarida. Kwa mfano, istilahi za uchaguzi zimechapishwa katika EASC Journal Na. 27 la 1957 na istilahi za ujenzi zimechapishwa katika EASC Journal Na. 28/1 la 1958. Katika mwaka wa 1956, mbali na kuchapisha jarida kamati ilianza kutayarisha vitabu vya ziada ambavyo vingechapishwa kama nyongeza kwa jarida. Karibu vitabu hivyo vyote vilikuwa tenzi. Utenzi wa Vita vya Wadachi kilichohaririwa na J. W. T. Allen kilikuwa tayari kimechapishwa katika mwaka 1955 kama kitabu cha ziada ya EASC Journal Na. 25. Miaka miwili baadaye Utenzi wa Vita vya Majimaji kilichoandikwa na Abdul Karim bin Jamaliddini kilichohaririwa na W. H. Whiteley kili- chapishwa kama kitabu cha ziada ya EASC Journal Na. 27 la 1957. Vitabu vingine vya ziada vilichapishwa mwaka wa 1958. Vitabu hivyo ni Maisha ya Siti Binti Saad cha Shaaban Robert EASC Journal Na. 28/1 na Maisha ya Hemed bin Mohammed, Yaani Tippu Tip Kwa Maneno Yake Mwenyewe kilichoandikwa utangulizi wa kihistoria na kufasiriwa na Bi 63 Alison Smith. Kitabu hiki kilikuwa cha ziada ya Jarida la EASC Journal Na. 28/2 la 1958. Nyongeza ya kamusi ambayo ilitarajiwa kuchapishwa kama kijitabu ilichapishwa katika jarida la EASC Na. 26 la 1956. Wazo la kuchapisha nyongeza ya kamusi lilijadiliwa katika mikutano kadha ambayo ni pamoja na mkutano wa kumi na tisa (19) wa kila mwaka wa Kamati wa Desemba 1955. Maneno yaliyokusudiwa kuchapishwa katika nyongeza hiyo ya kamusi yalichapishwa katika matoleo kadha ya jarida. Wazo la kuchapisha nyongeza ya kamusi ya Kiswahili-Kiingereza na Kiingereza-Kiswahili yaonekana lilikuwa limetupiliwa mbali kufikia mwaka 1959 ambapo katibu aliulizwa atafute njia za kupata pesa za kuchapisha kamusi timilifu ya Kiswahili-Kiingereza. Wazo la kamusi mpya lilizuka baada ya kulinganisha kamusi sanifu ya Kiswahili-Kiingereza na kamusi kubwa zaidi za lugha "ndogo" kuliko Kiswahili. Kamati ilionelea kwamba ikiwa ushirikiano wa watawala wa Kibelgiji huko Kongo ungepatikana, kamusi za Kiswahili-Kiingereza na Kiswahili- Kifaransa zingechapishwa wakati mmoja. Kwa kufanya hivyo gharama ingepunguzwa na pengo kati ya Kiswahili sanifu na lahaja ya Kingwana ingepunguzwa. 3l* Makala kubwa za jarida la EASC Journal la 1956 zilikuwa ni pamoja na mchangio wa Wajerumani katika somo la Kiswahili katika miongo ya hivi karibuni iliyoandikwa na Prof. E. Dammann na utafiti wa istilahi za ukoo wa Waswahili iliyoandikwa na A. H. J. Prinns. Pia jarida hilo lilichapisha makala fupi iliyoitwa "Halmashauri ya Kiswahili ya Afrika Mashariki" iliyoandikwa na Shaaban Robert wa Tanganyika. Mwandishi anasema kwamba Kiswahili kiliondolewa katika vyuo vya Uganda. Pia anatoa hoja kwamba Wakenya walikuwa wakisomesha Kilatini badala ya Kiswahili katika vyuo vyao. Ni wazi, hata ingawa Shaaban Robert hakuthibitisha hoja yake, kwamba watawala wa kikoloni walikuwa tayari wameanza kupunguza matumizi ya Kiswahili katika vituo vya elimu. Kwa mara ya kwanza, tunafahamishwa kwamba kamati ilikuwa ikikadiria mitihani ya Kiswahili ya watahini wa Chuo Kikuu cha Cambridge. Kamati ilikuwa ikiwashauri kuhusu muundo na kupendekeza vitabu vya lazima. Katika Jarida, EASC Journal Na. 27 la 1957, katibu, W. H. Whiteley, anaalika maoni na mchangio kwa nyongeza ya kamusi ya Kiswahili sanifu. Yaonekana hamu ya wanakamati kuendelea na shughuli zao ilikuwa imeanza kufifia kwa kuwa tawala za kikoloni za Afrika Mashariki -- 31* Mabadiliko ya sera ya lugha yaliyojadiliwa katika sura ya nne hayakuiwezesha Kamati kutimiza lengo hili. 64 hazikuonyesha shukrani bali ziliipuuza Kamati. Alipokuwa akiwapa moyo na kuwahimiza waandike kamusi, Whiteley aliongeza kusema yafuatayo: "Hata ingawa kazi ya kutayarisha kamusi ya Kiswahili-Kiingereza imekaribia kwisha idadi ya maoni tuliyoyapata ni ndogo kuliko ilivyotumainiwa. Je, yawezekana wazungumzaji wa Kiswahili wakose mapenzi kwa lugha yao kiasi cha kwamba kazi muhimu kama hii inapita bila wao kujali? Ama ni wanakamati - ambao Kamati yote hutegemea - ambao wamekosa hamu ambayo wanatarajiwa kuo- nyesha? Yeyote mwenye ulegevu huu wa kutojali asijiliwaze kwa kuamini kwamba hii ni kazi ya kitaaluma tu ambayo haina umuhimu wa kufaa. Mahitaji ya kuwasiliana vya kutosha tayari yamedhihirishwa kwa ukatili nchini Kenya kwa muda wa miaka minne iliyopita, na ni ujinga kudhania kwamba Kiswahili hakina matatizo kama hayo." 32* (EASC Journal Na. 27, 1957: 6). Tabia ya kutojali Kiswahili ya serikali za kikoloni za Afrika Mashariki na ulegevu wa wanakamati ulianza kudhuru moyo wa kufanya kazi wa maafisa wa Kamati. Pia katika jarida hilo hilo la 1957, mchunguzi msaidizi Bwana O. B. Kopoka anaripotiwa kuwa amehuzunishwa sana kwa kuwa wanakamati hawaonyeshi kupendezwa na kazi yake kuhusu sarufi ya Kiswahili. Kutokana na uchunguzi wa Bwana Kopoka tayari vitabu viwili vya sarufi - Miao na Matendo vilikuwa vimechapishwa. Baadaye, mwaka 1959 Bwana Kopoka alijiuzulu kazi ya mchunguzi msaidizi na akaanza kufanya kazi na Kampuni ya Shell. Baada ya kujiuzulu huko, Kamati ilisimamisha kazi za uchunguzi wa sarufi. Pia, katika jarida la Kamati Na. 30 la 1959, tunajulishwa kwamba kamati imesikitishwa kwa kufahamishwa kwamba serikali ya Tanganyika haihitaji tena sarufi na kwamba haitaki kazi aliyoifanya Bwana Kopoka (uk. 19). Katika mwaka 1958, kamati ilieleza kusikitishwa kwake na idadi ndogo ya Waafrika waliokuwa wakinunua jarida. Huku kukiwa na wanunuzi kutoka sehemu kadha za Ulaya, hakukuwa hata na mtu mmoja aliye- linunua kutoka Zanzibar. Ingawa hivyo, kwa jumla, idadi ya wanunuzi ilikuwa ikiongezeka kutoka 350 mwaka 1952, kufikia 600 mwaka 1958. Kuanzia mwaka 1958 ilikatwa shauri kuchapisha jarida mara mbili kwa mwaka kwa sababu ya kuongezeka kwa makala za kuchapishwa. Suala la ununuzi wa majarida lilizuka tena mwaka mmoja baadaye. -- 32* Ni dhahiri kwamba sentensi ya mwisho inazungumzia juu ya hali ya hatari nchini Kenya. Serikali ya kikoloni ya Kenya iliona wazi kwamba haikuwa na ujuzi wa lugha wa kutosha kupenya njama za Mau Mau kwa kutumia Kikikuyu, Kimeru au Kiembu. 65 Katika maoni ya mwandishi wa Jarida la Kamati - EASC Journal Na. 29/1 la 1959, Whiteley alitaja kwamba hakukuwa na Mhindi au Mwafrika yeyote aliyekuwa akilinunua hata ingawa makala kadha katika kila toleo pamoja na vitabu vyote vya ziada vilikuwa vikitarajiwa kusomwa na Waafrika. Whiteley analaumu ukosefu wa njia bora za usambazaji majarida. Ni wazi pia kwamba, tatizo hili pia lilisababishwa na kutotangazwa vyema kwa shughuli za Kamati na Kamati yenyewe haiwezi kujiepusha na lawama hii. Katika kurasa zingine za jarida hilo imetajwa kwamba, wakiwa katika shughuli za kufanya uchunguzi wa Kihadimu, Kitumbatu na Kipemba huko Zanzibar na Pemba, Kamati ilisikitika kuona kwamba watu wa Zanzibar na Pemba hawakujua kuwepo kwa Kamati hii. Katika mkutano wa kila mwaka wa 1957, Kamati ilionyesha wasiwasi na masikitiko yake kuhusu kiwango cha chini cha Kiswahili kilichokuwa kikitumika katika vipindi vya idhaa mpya ya Kiswahili ya B.B.C. Jarida la 1958 - EASC Journal Na. 28 limechapisha makala ya mfululizo wa mihadhara mitano ya kila mwezi iliyotolewa Tanga kwa kudhaminiwa na "Jumuia ya Taaluma ya Kiswahili" ya Tanga. Sehemu ya pili ya makala ya Prinns kuhusu istilahi za ukoo wa Waswahili pamoja na majina ya Kiswahili ya samaki wa baharini pia yamechapishwa katika toleo hilo. Kwenye mkutano wa kila mwaka wa Septemba 1958, wazo la kuanzishwa kwa kamati ya ukusanyaji, uhariri na uchapishaji wa makala za kihistoria ulijadiliwa. Iliripotiwa katika mkutano huo kwamba Liwali wa Pwani, Kenya, Sheikh Mbarak Ali El Hinawy angekuwa radhi kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo. Hata hivyo Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilikuwa na wasiwasi. Whiteley anatahadharisha kwamba "bila shaka familia nyingi zinashuku kwamba Wazungu wataitumia miswada yao kwa njia mbaya". Hofu za Waswahili zilikuwa na msingi kwa sababu hata ingawa Wazungu walihifadhi miswada hiyo, wengine, kama vile Jan Knappert, wameichapisha baadhi ya miswada hiyo kuwa vitabu ghali sana huko Ulaya. Vitabu hivyo havipatikani Afrika Mashariki na hata vikipatikana ni ghali sana hivi kwamba wenye miswada hawawezi kupata pesa za kuvinunua licha ya kuwa baadhi yao walilipwa pesa kidogo na wengine hawakulipwa chochote kwa miswada yao. 33* -- 33* Mifano ya vitabu vya Jan Knappert ambavyo Mswahili wa kawaida hawezi kuvigharamia ni pamoja na vitabu vya mashairi ya kiislamu Swahili Islamic Poetry vilivyochapishwa na E. J. Brill, huko Leiden, Netherlands mwaka 1971, na kitabu chenye tenzi za karne nne: Four Centuries of Swahili Verse: A Literary History and Anthology chenye kurasa 323 kilicho- chapishwa London na Heinemann mwaka 1979. 66 Mpango ungefanywa ili miswada kama hiyo ichapishwe na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Pesa ambazo zingepatikana kutokana na kuuzwa kwa vitabu vilivyochapisha zingewekwa kwenye wakfu ambao ungetumiwa kuwanufaisha Waswahili kwa njia kama vile kugharamia masomo ya juu ya watoto wao, kugharamia uchunguzi zaidi, au kwa huduma za jamii. Kamati ilijua wazi kwamba Waswahili hawakuwa tayari kupeana miswada yao, na hiyo ndiyo sababu walihitaji msaada wa watu mashuhuri wa pwani kama vile Liwali Sheikh Mbarak Ali el Hinawy. Kamati ya kihistoria iliundwa. Ilikutana kwa mara ya kwanza tarehe 27 Juni 1959. Wafuatao walihudhuria: 1) Sheikh Mbarak Ali El Hinawy. 2) Bwana J. S. Kirkman wa Mombasa. 3) Bwana J. W. T. Allen - Katibu mtendaji wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. 4) Bwana Shihabuddin Chiraghdin - wa Mombasa. 5) Sheikh Hyder Mohammed El Kindy - wa Mombasa ambaye alikuwa katibu wa hii kamati ndogo. Wanachama wafuatao wa hiyo kamati waliomba radhi kwa kutoweza kuhudhuria. 1) Sir John Grey wa Zanzibar. 2) Sir Said bin Ali Mugheiry wa Pemba. 3) Dkt. G. S. P. Freeman-Grenville wa Mafia. 4) Sheikh Muhammad Kassim Mazrui wa Malindi. 5) Sheikh Mohammed bin Ali bin Hamed Buhry wa Tanga. Kamati hiyo ilipewa jukumu la kukusanya miswada mingi ya kihistoria iwezekanavyo. Ilikubaliwa kwamba makala na miswada yote itakayo- kusanywa atapelekewa katibu katika chuo cha Makerere. Katibu ali- takikana kuiorodhesha na kuipa nambari miswada hiyo na ikiwezekana angeinakili na kuipeleka nakala moja kwa mwenyekiti na nyingine kwa mwenye mswada kama shukrani kwa ushirikiano wake - (Tazama: EASC Journal Na. 30, 1959: 13). Yaonekana kwamba suala la mwenye haki za kunakili na kuchapisha miswada na makala hayo halikushughu- likiwa. Zaidi ya hayo, Kamati iliamua kuchunguza uwezekano wa kupiga picha ndogo (microfilm) maandishi ya kale yaliyokuwa katika hifadhi za Makerere na Mombasa. Katibu aliombwa kutafuta msaada wa pesa kutoka kwa mashirika ya kutoa misaada ili kuwezesha ukusanyaji wa miswada. Kiasi fulani cha pesa kilitumiwa kununua miswada kutoka kwa watu ambao hawakuwa tayari kuitoa bure. Ripoti ya mkutano wa 21 wa kila mwaka uliokuwepo kati ya tarehe 10 na 13 Septemba 1958 huko Tanga, Tanganyika, imechapishwa katika 67 jarida Na. 28/1 la 1958. Kamati ilijadili hali ya baadaye ya Kamati kwa vile kushirikishwa kwake kwenye Taasisi ya Uchunguzi wa Shughuli za Jamii ya Afrika Mashariki katika Chuo cha Makerere kwa kipindi cha miaka mitano kungemalizika mwisho wa mwaka wa masomo wa 1959/60. Wakati huo Taasisi ilikuwa ikigharamia nusu ya mshahara wa katibu na hakukuwa na uhakika ikiwa pesa zingepatikana na kuigharamia kamati baada ya hapo. Wanachama wa Kamati walikubaliana kuonyesha umuhimu wa Kamati kwa serikali zao ili kuiwezesha Kamati kupata pesa baada ya kwisha kwa muda wa kuwa kwenye Taasisi. Makisio mapya ya kuigharamia kamati yalipelekewa serikali (zote) ili kufikiriwa. Kufikia wakati wa mkutano uliofuata wa kila mwaka kati ya tarehe 9 na 11 Septemba huko Mombasa, serikali za Afrika Mashariki zilikuwa bado hazijajibu ombi la Kamati. Kwa hivyo Kamati haikuwa na uhakika iwapo wangepata pesa ambazo walikuwa wameomba. Ilionekana kwamba Kamati zaidi ilikuwa chombo cha uchunguzi ambacho kingegharamiwa na serikali mpaka kitakapojiunga vizuri na Chuo Kikuu. Katika ripoti ya kila mwaka ya 1958 - 1959 iliyochapishwa kwenye EASC Journal Na. 30 la 1959, katibu mpya J. W. T. Allen anaeleza kwamba Kamati ilipata shida kubwa za kiidara kwa sababu ya kuondoka kwa katibu W. H. Whiteley, msaidizi wake Bi. Fawler na Bwana O. B. Kopoka. Pia anaripoti kwamba hakukuwa na matumaini ya kupata pesa zingine kutoka kwa serikali. Ilibidi Kamati ipunguze gharama zake kwa kuajiri makarani wa muda inapowezekana na kwa kuhamisha ofisi za Kamati hadi University Hall ambapo Allen alikuwa akifanya kazi ya mlinzi. Ilibidi maktaba ya Kamati iwekwe amana katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Makerere kwa sababu ya kukosa chumba kulikosababishwa na ukosefu wa pesa. Uamuzi wa kupunguza matumizi zaidi. ulifikiwa katika mkutano wa kila mwaka uliokuwepo kati va tarehe 4 na 5 Septemba 1959. Katika mkutano huo, Kamati ilikata shauri kutochapisha vitabu vya ziada tena kwa sababu ya gharama kubwa ya uchapishaji. Kwa bahati nzuri Kamati ilikuwa na ushirikiano bora na East African Literature Bureau na mkurugenzi wake, C. G. Richards, alikuwa amehudhuria mkutano huo. Badala ya vitabu hivyo vya ziada ya majarida, East African Literature Bureau ilikubali kuanza kuchapisha mfululizo wa vitabu wenye kujulikana kama Johari za Kiswahili. Wangeanza kuchapisha vitabu viwili viwili kila mwaka. Ilikubaliwa pia kwamba vitabu vya kwanza vya Johari za Kiswahili ambavyo vingechapishwa na Kamati kama vitabu vya ziada ya majarida vitakuwa: 1) Utenzi wa Vita vya Wadachi. 2) Utenzi wa Abdirrahmani na Sufiyani. 68 3) Utenzi wa Uhud. 4) Utenzi wa Seyyida Hussein bin Ali. 34* Mkurugenzi wa East African Literature Bureau pia alikubali kuchapisha toleo jipya la kitabu kilichosahihishwa cha Tippu Tip. Kufikia mwaka 1959 vitabu vifuatavyo vya uchunguzi wa lahaja za Kiswahili vilikuwa tayari vimechapishwa na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki: 1) Ki-Mtang'ata - A Dialect of Mrima Coast na W. H. Whiteley, 1956. 2) Ki- Vumba - A Dialect of the Southern Kenya Coast na H. E. Lambert, 1957. 3) Chi-Jomvu and Ki-Ngare - Sub dialects of the Mombasa Area na H. E. Lambert, 1958. 4) The Dialects and Verse of Pemba - An Introduction na W. H. Whiteley 1958. 5) Chi-Chifundi - A Dialect of The Southern Kenya Coast na H. E. Lambert 1958. Kwa sababu ya matatizo ya kipesa ya Kamati, Allen aliandika maoni ya mhariri ya EASC Journal Na. 30 la 1959 na kutishia kwamba Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki haingeweza kuendelea kufanya kazi yake kikatiba. "Ni lazima ipanuke, iwe kitu kikubwa au ikomeshe jitihada za kuendelea", akaandika. Anailaumu nia mbaya ya kikoloni ya kupuuza na kutojali Kiswahili kwa kusababisha mashaka hayo ya Kamati. 35* Allen anaeleza kwamba Kamati ni kama mji uliozingirwa. Ikikoma kujitahidi itapoteza kile kilichochukua miaka mingi ya kazi ngumu kukipata. Lingine la kufanya ni kwa kamati kuvumilia kuendelea na kutumaini kwamba watapata mwokozi. Kamati ilikuwa katika hali ya kukata tamaa, na Allen alijitahidi juu chini kutafuta msaada wa pesa kutoka kwa mashirika ya kutoa misaada. Kwenye mkutano wa Kamati wa kila mwaka uliokuwepo mwezi Septemba 1959 Kamati ilijulishwa kwamba Chuo Kikuu cha Makerere kilikuwa kimependekeza kuundwa kwa kamati ya chuo ya kushughulikia somo la Kiswahili. Kamati hiyo ingetoa mapendekezo yake kwa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Kamati ilikubali pendekezo la kamati ya chuo kikuu la kuanzishwa kwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilikubali pendekezo hilo hata ingawa ilielewa wazi kwamba kuendelea kwa "Kamati kungeishia -- 34* Majina kamili, pamoja na watunzi au waandishi na wahariri yapatikana katika bibliografia. 35* Tazama sehemu ya kubadili sera dhidi ya Kiswahili katika sura ya Tano ambapo Allen amenukuliwa kwa kireru. 69 kwenye mwanzo wa kipindi kipya cha miaka mitano (au mapema zaidi)". Kamati vilevile ilipendekeza kwamba, kamati ya chuo ihakikishe kwamba washauri wenye ujuzi wa isimu, elimu jamii na historia wanashirikishwa katika kuanzishwa kwa taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Kamati vile vile ilitaraji kwamba, serikali za Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar zitaendelea kuisaidia Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili kifedha ikiwa Makerere au ikihamia katika chuo kikuu kingine. Makala kuu zilizochapishwa mwakawa 1960 (EASC Journal Na. 31) ni pamoja na sehemu ya pili ya makala ya Sir John Gray kuhusu historia ya Zanzibar, sehemu ya pili ya makala ya W. H. Whiteley kuhusu lahaja ya Zanzibar mashambani na makala ya Mwidani bin Mwidadi iliyohaririwa na Lyndon Harries kuhusu kuanzishwa kwa mji wa Rabai. (Sehemu za kwanza za makala ya Sir John Gray na W. H. Whiteley zilichapishwa katika EASC Journal Na. 30 la 1959.) Mjadala wa matumizi ya Kiswahili nchini Zaire, Rwanda na Burundi ulioandikwa na Hamis Kitumboy na makala ya B. Lecoste kuhusu sarufi ya Kiswahili cha Kongo ya Ubelgiji (Zaire) yalichapishwa pia katika jarida hilo la 1960. Mnamo tarehe 23 Mei 1961 ilitangazwa huko Makerere kwamba Wakfu wa Calouste Gulbenkian ya Lisbon umetoa msaada wa pauni elfu tisa (?9000) na kwamba kiasi kama hicho kitatolewa na Hazina ya Maendeleo ya Makoloni. Pesa hizo zilitolewa kugharamia mchunguzi mmoja na wasaidizi wake kwa miaka mitatu pamoja na usafiri na gharama zingine ili kukiwezesha Chuo Kikuu cha Makerere kianzishe Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Ripoti hiyo iliyotolewa kwa magazeti pia inaeleza kwamba Afrika Mashariki pamoja na Kongo (Zaire), wana lugha moja kuu ya mawasiliano ambayo hueleweka kwa urahisi na Waafrika wa eneo hilo, kwa sababu imefanana sana na lugha zao. Inapendekezwa kwamba chuo au taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili ianzishwe kwa kupanua kazi za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ili kukuza uchunguzi katika lugha ya Kiswahili. Pia inaelezwa kwamba serikali za Afrika Mashariki zingeendelea kugharamia shughuli za kiidara ili pesa zilizotolewa zitumike zaidi katika shughuli za uchunguzi. 70 Sura ya Tano 5.0 Kiswahili na sera ya lugha 5.1 Kiswahili na sera ya lugha nchini Uganda Historia ya maendeleo na usanifishaji wa Kiswahili pamoja na shughuli za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki hugusia zaidi vile hali ilivyokuwa Tanzania na Kenya kuliko Uganda. Labda sababu yake ni kwamba Kiswahili hakikupewa nafasi ya kuenea huko kama kilivyoenea Kenya na Tanzania. Wabaganda walipinga kusomeshwa kwa Kiswahili katika shule zao wakati ambapo serikali ya kikoloni ilikuwa tayari kukuza Kiswahili. Wakati sera ya lugha ilipobadilika dhidi ya Kiswahili kote katika Afrika Mashariki kuanzia muongo wa 1950 Kiswahili kiliondolewa shuleni kwa kuwa hakikuwa tena lugha iliyotambulika kusomeshwa nchini Uganda. Kabla sijayajadili mabadiliko ya sera ya lugha dhidi ya Kiswahili, kwanza nitaijadili sera ya lugha nchini Uganda, na vile ilivyokuwa ikibadilikabadilika, kufikia wakati Kiswahili kilipoondolewa shuleni. Kuanzia mwaka wa 1925 suala la ni lugha zipi za Kiafrika zitakazo- tumika kusomesha katika madarasa ya mwanzo ya shule za msingi kote nchini Uganda, lilijadiliwa na serikali ya kikoloni. Kwanza uamuzi ulitolewa kwamba Kiluganda itumike katika eneo lote lililokuwa likitumia lugha za Kibantu. Kisha kamati ikaundwa kuchagua lugha muafaka ya kutumia katika eneo la Kinailoti la Mikoa ya Kaskazini na Mashariki. Kamati hiyo pia ilitakikana kutayarisha tafsiri ya vitabu vya shule katika lugha zilizochaguliwa. Kiingereza kingetumika kuanzia madarasa ya juu ya shule za msingi na kuendelea. Mwaka 1926 Idara ya Elimu iliamua kutumia lugha tatu za Kiafrika katika shule za msingi. Lugha hizo ni: 1) Kiluganda - iliyotumiwa Buganda na sehemu ya kaskazini ya Mkoa wa Mashariki. 2) Kiacholi - iliyotumiwa katika Mkoa wa Kaskazini. 3) Kiateso - lugha iliyotumiwa katika shule za eneo la kati la Mkoa wa Kati. Lugha zingine zote za Kiafrika zilitambuliwa kuwa "lahaja ndogo" ambazo hazingetumiwa ila katika shule za malezi. Kiwango hicho cha 71 elimu kilisemekana kwamba hakikuhitaji vitabu na kwamba wanafunzi wengi hawakuendelea na masomo huko kwa kuwa walijiunga na shule za msingi ambako wangetumia moja kati ya lugha tatu zilizochaguliwa. 36* Kufikia 1927 vitabu kadha vilikuwa vimeandikwa kwa Kiluganda lakini kulikuwa na matatizo katika zile lugha zingine mbili. Gavana aliandika kumbukumbu kuhusu jambo hili, nalo baraza la kutoa mashauri kuhusu elimu ya Waafrika likaijadili kwa kirefu. Matokeo yake ni kwamba ilionekana muafaka Kiacholi na Kiateso zitumiwe kama lugha za kusomesha katika shule za msingi zilizokuwa katika maeneo hayo tu (ya Acholi na Teso). Ilikubaliwa kwamba Kiswahili kisomeshwe kama somo katika shule za msingi na kwamba vitabu vya masomo kama vile afya, jiografia na kilimo viandikwe kwa Kiswahili. 37* Uamuzi wa kusomesha Kiswahili ulifikiwa kwa sababu ya matatizo ambayo hayakuweza kutatuliwa wakati huo ya kutafsiri vitabu kwa lugha za Kiateso na Kiacholi. Sababu nyingine kubwa pia ni ile athari iliyotokana na kutumiwa kwa Kiswahili katika nchi jirani za Kenya, Tanganyika na Zanzibar. Ripoti ya Idara ya Elimu ya Mwaka wa 1927 inaongeza kwamba "Aidha lugha hizi mbili si lugha za kwanza za watu wengi walioko katika maeneo hayo, na kwao Kiswahili hakitakuwa shida kukielewa kuliko Kiateso na Kiacholi" (uk. 10). Kwa hivyo sera ya lugha iliruhusu kutumiwa kwa lugha za kwanza kusomesha wanafunzi wote katika miaka miwili ya kwanza ya masomo kiwango ambacho vitabu havikuhitajika sana. Baada ya kiwango hicho, wanafunzi walianza kujifunza Kiswahili, lugha ambayo iliwawezesha kusoma idadi kubwa ya vitabu ambavyo vilikuwa vikiongezeka kwa wingi. Kiswahili kilitambuliwa kuwa lugha ya pekee ambayo ingerahisisha mawasiliano katika nchi za Afrika Mashariki. Kilitambuliwa kuwa lugha ya watu wengi ambayo ingetumiwa katika kuvichapisha vitabu vingi vya shule na vya fasihi. Gavana Gowers aliyekuwa Gavana wa Uganda wakati huo alikiunga mkono Kiswahili. Katika mwaka 1928 alipendekeza Kiswahili kitumiwe badala ya Kiluganda kama lugha ya elimu na utawala nchini Uganda (Ladefoged et. al. 1971: 88). Sera hii ya kufunza lugha za kwanza zikifuatiwa na Kiswahili ilifuatwa katika mikoa yote ya Uganda isipokuwa mkoa wa Buganda. Hapo mwanzoni Kiswahili kilipingwa katika Mkoa wa Mashariki, lakini baadaye kilikubalika kuliko Kiluganda ambayo ingetumiwa ikiwa Kiswahili hakingetumika. Katika Mikoa ya Kaskazini na Magharibi mabadiliko ya kuanza kutumia Kiswahili yalitajwa kuwa "yalipendwa -- 36* Education Department, Annual Report ya 1926 uk. 11. 37* Education Department, Annual Report ya 1927 uk. 10. 72 sana na watu wote". 38* Kwa sababu ya sera hii mpya ya lugha, vitabu vya shule vilivyokuwa vikitumiwa Tanganyika vilianza kutumika katika shule za Uganda kuanzia mwaka 1928. Pia Mkurugenzi wa Elimu nchini Uganda alipendekeza kuanzishwa kwa shirika la kutafsiri vitabu vya Kiswahili ili kuhudumia nchi za Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar. Mwaka 1928 Ronald Snoxall alihamishwa kutoka Tanganyika kwenda Uganda kama Msimamizi wa Elimu ya Msingi. Snoxall alikuwa na ujuzi wa nchi ambayo ilikuwa ikitumia Kiswahili kama lugha ya kufunza katika shule za msingi. Idara ya Elimu ya Uganda ilihitaji msaada wake katika jaribio la kufuata sera ya lugha ya Tanganyika. 39* Vituo vya elimu vilivyokuwa vikihudumia nchi nzima yaonekana viliunga mkono kwa dhati sera mpya kuhusu Kiswahili. Shule ya Ufundi ya Kampala, kwa mfano, iliamua kutofundisha Kiingereza. Badala ya Kiingereza, Kiswahili kilifundishwa kwa kuwa ndicho lugha ya mawasiliano kote Afrika Mashariki. Kama alivyosema mkuu wa shule hiyo, Bwana Savile, shule hiyo ilikuwa ikihudumia nchi nzima pamoja na watu wenye kuzungumza lugha zisizo za Kibantu ambao hawangeielewa Kiluganda. Mwezi Januari 1928 chuo cha serikali cha kufunza walimu wa shule za msingi kilianzishwa. Katika chuo hiki, Kiswahili kilitumiwa kama lugha ya kusomeshea. Katika ripoti yake ya 1928 mkuu wa chuo hicho, Kampala Normal School, A. J. Lush, alisema kwamba mitihani ya Kiswahili ilionyesha maendeleo ya kuridhisha katika mazungumzo na maandishi. Mwalimu wa Kiswahili, Sheikh Abdul Rahman Mahomet, aliajiriwa kutoka Zanzibar mwaka huo wa 1928. Mwezi Februari 1929 mkuu wa chuo pamoja na wanafunzi wake sita walitembelea Mombasa ambako walijifunza Kiswahili kwa muda wa miezi mitatu. Matumizi ya Kiswahili yalikuwa yakienea vizuri kote nchini Uganda mwaka 1929 isipokuwa Buganda. Wanafunzi wa Uganda kutoka shule za serikali na za misheni walipelekwa Mombasa, Kabaa na Zanzibar ili kupewa mafunzo ya Kiswahili. Vilevile Kiswahili kilifunzwa kwa mafanikio katika chuo cha walimu cha misheni ya C.M.S. Mukono na chuo cha walimu cha misheni ya White Fathers, Bikira. Katika vyuo kadha Kiswahili kilifunzwa badala ya Kiingereza. Urahisi wa Mwafrika kujifunza lugha nyingine ya Kiafrika badala ya Kiingereza ulitambuliwa. Kiswahili kilionekana kwamba kinafaa kuliko lugha zingine za Kiafrika kwa sababu kulikuwa na vitabu vingi vilivyo- andikwa kwa Kiswahili. Haingewezekana kuchapisha vitabu vyote -- 38* Education Department, Annual Report 1928 uk. 9. 39* Education Department, Annual Report ya 1928 uk. 6. 73 vinavyohitajika shuleni katika lugha nyingi za Kiafrika kwa sababu ya gharama ya kuchapisha nakala chache kwa kila lugha. Vitabu vya Kiswahili viliuzwa kwa wingi nchini Uganda. Kuanzishwa kwa kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kulikuwa kunangojewa kwa hamu nchini Uganda kwa kuwa kungesaidia kuchapishwa kwa vitabu vingi vya Kiswahili. Ripoti ya maendeleo ya misheni ya C.M.S. ya Elgon inaonyesha kwamba walianza kufunza Kiswahili kwa mara ya kwanza mwaka 1929. Baadhi ya walimu na wanafunzi wa chuo cha walimu cha misheni hiyo walipelekwa Mombasa kufunzwa Kiswahili ili wasaidie katika kuanzishwa kwa somo la Kiswahili. 40* Wakati huo huo, Katibu wa Elimu wa shule za misheni Katoliki ya Mataliani, W. Gotta alitoa ripoti kwamba hata ingawa Kiswahili kilikuwa somo jipya, kilipokelewa vizuri katika madarasa ya shule za msingi na vyuo vya walimu katika eneo la Gulu. Baadhi ya shule za msingi za Gulu, Kitgum, Moyo, Ama na Ngal zilikuwa na matatizo ya kusomesha Kiswahili. Lakini iliripotiwa kwamba masista wote waliokuwa wakiongoza shule hizo walikuwa tayari wamekwenda Dar es Salaam ili kujifunza Kiswahili. Ripoti ya Koloni ya Uganda ya mwaka 1929 inasema yafuatayo kuhusu maendeleo ya Kiswahili: "Ufunzaji wa Kiswahili tayari umeanzishwa katika Mkoa wa Masha- riki na maendeleo mazuri yamepatikana. Lugha hii itasomeshwa kote katika vyuo vya kufunza walimu wa shule za vijijini isipokuwa Buganda. Vitabu vilivyoko, ambavyo vimekusudiwa kutumiwa na makabila ya Afrika Mashariki yanayojua Kiswahili havifai kwa makabila ya bara ambao wanaanza kujifunza lugha hiyo; utayarishaji wa vitabu vinavyofaa zaidi yafaa iwe kazi ya kwanza ya Kamati mpya ya Kiswahili ya Afrika Mashariki." 41* Juhudi za kueneza ufunzaji wa Kiswahili nchini Uganda zilivuma mwaka 1930 wakati mradi mahsusi wa kufunza walimu wa vijijini kwa miaka miwili ulipoanzisha vituo 29 kote katika Mikoa ya Mashariki, Kaskazini na Magharibi. Masomo yaliyokuwa yakifunzwa ni dini, kilimo, mbinu za kufunza, afya na Kiswahili. Ufunzaji wa Kiswahili ulinuiwa kuhakikisha kwamba walimu wa gredi C watakaofaulu watakuwa wame- jiandaa vya kutosha kusitawisha ufunzaji wa Kiswahili katika shule zao. Wawakilishi wawili wa serikali na wengine wawili wa misheni waliwakilisha Uganda kwenye mkutano wa kwanza wa kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki uliokuwepo Nairobi mwezi Aprili 1930. -- 40* Education Department, Annual Report ya 1929 uk. 31. 41* Uganda Annual Colonial Reports: Annual Report 1929, uk. 31, London, 1930. 74 Sera hii ya kueneza Kiswahili iliendelezwa na misheni mwaka wa 1930. Misheni ya C.M.S. iliripoti kuenea kwa matumizi ya Kiswahili bora. Misheni ya White Fathers iliwafunza Kiswahili walimu wa zamani kumi na watatu ili wahitimu kuwa walimu wa kudumu. Katibu wa Elimu wa misheni ya White Fathers, C. Robbiard alisema kwamba ni rahisi sana kwa Mwafrika kujifunza lugha nyingine ya Kiafrika hivi kwamba baadhi ya walimu wao walijifunza wenyewe. 42* Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilikutana Makerere Uganda mwezi Aprili 1931 kwa mara ya kwanza. Katika mkutano huo kazi muhimu ilikamilishwa kuhusu usanifishaji wa uandikaji wa maneno ya Kiswahili yaliyoazimwa kutoka lugha za kigeni. Mwezi Juni 1931 Baraza la Kutoa Mashauri Kuhusu Elimu ya Waafrika lilikutana na kutoa maoni kwamba Kiluganda iendelee kuwa lugha ya kusomesha masomo mengine katika Mkoa wa Buganda na kwamba Wabaganda wakipenda wanaweza kuanzisha somo la Kiswahili. Pia shauri ilikatwa kwamba walimu wa vyuo vya walimu vya serikali wafunzwe ili kusomesha Kiswahili katika shule ya King's African Rifles (KAR), shule za polisi, na shule zingine za msingi zilizoko kwenye maeneo yenye lugha tofauti. Baraza hilo la kutoa mashauri pia lilisema kwamba: "Vyuo vya walimu vya misheni vinavyopata ruzuku vya Nabumali, Ngora, Arua, na Gulu lazima vifunze Kiswahili kwa wanafunzi wanaosomea huko. Kwamba katika maeneo yenye mchanganyiko wa lugha, Kiswahili kisomeshwe kama somo la shule za msingi mara tu walimu wanapopatikana kutoka vyuo hivyo, lakini lugha za kwanza za maeneo hayo ziendelee kuwa lugha za kufundishia. Kwamba, Kiswahili kisomeshwe katika chuo cha ufundi cha serikali ambacho kitasomesha vijana kutoka kote nchini." 43* Pingamizi ya kwanza kubwa dhidi ya Kiswahili ilianza mwezi Septemba 1931 wakati maaskofu wa misheni nne za Church Missionary Societies, pamoja na Kabaka wa wakati huo, Sir Daudi Chwa, walipomkabidhi Waziri wa Nchi anayesimamia Makoloni (ya Uingereza) kumbukumbu kulalamika dhidi ya kutumiwa kwa Kiswahili kama lugha ya pekee ya kusomesha masomo mengine katika shule za msingi. Nilipomhoji Ronald Snoxall alikiri kwamba karibu wahubiri wote wa Church Missionary Society (C.M.S.) walikuwa Wabaganda waliotaka kueneza lugha yao ya Kiluganda. Walitoa madai ya uwongo kwamba watu wote nchini Uganda walifahamu Kiluganda. Katika kumbukumbu yao, maaskofu pamoja na Kabaka walidai kwamba watu walikuwa wakilazimishwa kujifunza -- 42* Uganda Annual Colonial Reports. Annual Report ya 1929 uk. 31, London, 1930. 43* Education Department, Annual Report ya 1931, uk. 6. 75 Kiswahili kinyume cha kupenda kwao. Dai hili halikuwa la kweli. Sera ya lugha ya Gavana Sir William Gowers ilihimiza Kiswahili katika maeneo yenye mchanganyiko wa lugha yaliyokuwa nje ya Buganda. Kwa sababu ya pingamizi hii dhidi ya Kiswahili wamisheni wengi walikosa hamu ya kujifunza lugha hii. Jibu la Idara ya Elimu lilisema kwamba kumbukumbu hiyo ilitokana na kutoielewa sera ya serikali ya kutumiwa kwa lugha za kwanza katika madarasa mawili ya kwanza ya shule za msingi na kutumiwa kwa lugha hizo za kwanza pamoja na Kiswahili kama lugha za kusomesha masomo mengine katika madarasa mawili yafuatiayo. Kumbukumbu haikutaka Uganda itumie Kiswahili kama lugha ya mawasiliano kama nchi zingine za Afrika Mashariki kwa kuwa walitaka lugha ya Uganda (bila shaka - Kiluganda), iwe lugha ya mawasiliano nchini Uganda. Waganda, na zaidi Wabaganda, waliogopa na kwa hivyo hawakutaka kuanzishwa kwa shirikisho la Afrika Mashariki (Tazama Ladefoged et al 1971: 89). Mwaka 1932 suala la lugha ya kusomesha masomo mengine lilitatuliwa na serikali iipoamua kwamba masomo yote isipokuwa hesabu (hisabati) yasomeshwe kwa kutumia lugha za kwanza za maeneo mbalimbali. Somo la hesabu lilisomeshwa kwa Kiswahili, lugha ambayo wakati huo ilikuwa ikisomeshwa kama somo katika shule zote za msingi nje ya eneo la ufalme wa Buganda na Wilaya ya Busoga. Ripoti ya mwaka ya Koloni, ya 1931, ilionyesha kwamba Kiswahili kilikuwa kikianzishwa kwa utaratibu kama lugha ya kusomesha masomo mengine katika madarasa mawili ya mwisho ya shule za msingi katika wilaya zinazotumia lugha za Kinailoti. Katika Wilaya za Kibantu, Kiswahili kilikuwa kikisomeshwa kama somo isipo- kuwa katika Mkoa wa Buganda na Wilayani Busoga ambapo Kiluganda ilikuwa ikitumiwa katika madarasa yote ya shule za msingi. Ripoti za koloni za kila mwaka zilirudia habari hizi kati ya 1931 na 1936. Katika mwaka 1937 Ripoti ya Mwaka ya Koloni ilitaja kwamba Kiswahili kilisomeshwa kama somo katika madarasa mawili ya mwisho ya shule za msingi. Haya yalikuwa mabadiliko, lakini mradi Kiswahili kiliendelea kuwa katika ratiba ya masomo ni hakikisho kwamba kilikuwa kikienea kama lugha ya mawasiliano nchini Uganda. Ubora wa Kiswahili kikilinganishwa na Kiingereza ulitiliwa mkazo tena na Bwana E. G. Morris, Mkurugenzi wa Elimu, katika Ripoti ya Mwaka 1932. Morris aliandika yafuatayo: "Huku inapomchukua kijana hodari Mwafrika muda wa miezi sita tu kujifunza lugha ili aweze kukisoma kitabu cha Kiswahili na kukielewa barabara, ingemchukua angalau miaka sita ya kujifunza Kiingereza kwa makini ili aweze kukielewa kitabu cha Kiingereza cha kiwango sawa. Ni vigumu kuelewa vile watetezi wa Kiingereza wanavyotaraji 76 kusitawisha elimu ya Waafrika kwa kutumia lugha ya Ulaya kama lugha ya kusomesha masomo mengine." 44* (Inasikitisha kwamba baada ya zaidi ya nusu ya karne moja tangu maneno hayo yaandikwe vile hali ilivyo siyo tu kwamba lugha hiyo ya Ulaya ndiyo inasomesha bali Kiswahili kilichokuwa kikitetewa hata hakisomeshwi kama somo katika shule za msingi nchini Uganda). Katika "shule za kati" (shule ambazo zilitoa mafunzo ya kazi) lugha ya kusomesha ilikuwa ama Kiluganda katika eneo la kifalme la Buganda na Wilaya ya Busoga au Kiswahili katika sehemu zingine za Uganda. Lugha ya kusomesha katika vyuo vya walimu vya serikali ilikuwa ni Kiswahili. Ili kuonyesha vile ilivyokuwa rahisi kwa Waafrika kujifunza Kiswahili E. G. Morris anatoa mfano wa Mwalimu Omwami Y. Kakoza aliyeanza kujifunza mwezi Januari 1932 na ilipofika Septemba mwaka huo alifaulu mtihani wa Lower Government Standard Examination kwa kupata alama za juu zaidi - asilimia 89 1/2. Mwaka 1934 Kamati Kuu ya Church Missionary Society ya Diocese ya Elgon iliamua kwamba kuanzia wakati huo, masomo yote katika Chuo cha Kidini na cha Walimu cha Bawalasi yatasomeshwa kwa Kiswahili. Pia Kamati Kuu iliamua kutumia Kiswahili katika shule za msingi za misheni zilizokuwa katika maeneo ya mchanganyiko wa lugha. Mwaka 1935 mabadiliko yalifanywa kuhusu majina ya viwango tofauti vya elimu. Badala ya shule za malezi, shule za msingi, shule za kati ya chini, kati ya juu na sekondari ya chini, zote zilijulikana kama shule za msingi au shule za sekondari. Kila kiwango kilikuwa cha miaka sita. Mkaguzi wa shule za msingi katika mwaka huo wa 1935 alilalamika kwamba kulikuwa na uhaba wa vitabu vya shule vilivyoandikwa kwa lugha za kwanza zilizokuwa zikitumiwa kusomesha. Wakati huo huo kulikuwa na ongezeko la vitabu vya Kiswahili, lugha ya mawasiliano nje ya Mkoa wa Baganda na Wilaya ya Busoga. Serikali ilionyesha wasiwasi kuhusu kushuka kwa kiwango cha Kiingereza mashuleni kwa sababu walimu waliotarajiwa kukifundisha walikosa mazoezi baada ya kupelekwa kufanya kazi vijijini. 45* Mkutano wa kila mwaka wa Wakurugenzi wa Elimu wa Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar ulikuwa Makerere katika Februari na Machi 1936. Kati ya mambo waliyoafikiana ni kwamba kulikuwa na umuhimu wa kuongeza vitabu vya Kiswahili. Hali ya Kiswahili nchini Uganda ilitiliwa nguvu na mkutano wa kila mwaka wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki uliokuwepo Makerere mwezi Februari -- 44* Education Department, Annual Report ya 1932 uk. 5. 45* Education Department, Annual Report ya 1935 uk. 43. 77 1936. Lugha ya kusomesha katika "shule za kati" zilizokuwa zikifunza taaluma mbalimbali, zilizokuwa zikipewa ruzuku ya serikali, ilikuwa Kiswahili, isipokuwa Buganda na Busoga. Katika kiwango hicho cha shule, walimu Waganda wapatao 50 walikuwa wakifundisha zaidi ya wanafunzi Waganda 700, kwa kutumia Kiswahili mwaka huo wa 1936. Kulikuwa na washiriki 14 wa mashindano ya uandishi wa Kiswahili kutoka Uganda. Saba kati yao walipata zawadi. Wanne kati ya wale waliopewa zawadi walikuwa Wabaganda. 46* Ripoti ya Koloni ya mwaka 1938 yaonyesha kwamba Kiswahili kiliendelea kusomeshwa katika miaka miwili ya mwisho wa shule za msingi katika Wilaya za Kinailoti. Pia Kiswahili kiliendelea kuwa somo katika shule za Wilaya ya Kibantu isipokuwa katika Mkoa wa Buganda na Wilaya ya Busoga. Katika miaka ya vita, 1939-1945 shule zilitumiwa kutawanya taarifa za vita zilizoandikwa katika lugha nne, ambazo ni Kiingereza, Kiswahili, Kiluganda na Kigujerati. Habari hizo zilikusudiwa kubatilisha uvumi na propaganda. Mwaka 1942 Halmashauri ya Elimu ya Wanajeshi ya Afrika Mashariki (East African Army Education Corps) ilianzishwa. Moja kati ya madhumuni yake ilikuwa ni kupunguza matatizo ya mawasiliano kwa kufunza wanajeshi Waafrika Kiingereza na kuwafunza wanajeshi Wazungu ama Kiswahili, Chinyanja au Kisomali. Mkutano uliitishwa Makerere mwezi Oktoba 1944 kujadili kumbu- kumbu ya lugha katika shule za kuelimisha Waafrika iliyotolewa na Kamati ya Kutoa Mashauri ya Elimu Katika Makoloni. Maoni ya mkutano huo yalikuwa kwamba "Kiingereza pekee ndicho kilistahili kutambuliwa kuwa lugha ya baadaye ya mawasiliano". 47* Hata hivyo mkutano huo haukutetea kutumiwa kwa Kiingereza katika shule za Buganda. Ulipendekeza kwamba muda wa kusomesha Kiingereza uonge- zwe na kwamba lugha za kwanza zilistahili kusomeshwa kwa makini zaidi kote katika vyuo na vituo mbalimbali. Lugha zilizochaguliwa kusomeshwa hivyo, zilikuwa Kiluganda, Kirunyoro-Rutooro, Kiacholi (Kijaluo cha Kaskazini), Kiateso na Kilugbara. Haya yalikuwa mabadiliko makubwa ya sera. Kufikia mwaka 1944 sera ya lugha ilikuwa ikihimiza Kiswahili na lugha za kwanza. Sera mpya ilihimiza Kiingereza na lugha za kwanza. Haikutoa nafasi ya kusomeshwa kwa Kiswahili katika elimu ya Uganda. 48* -- 46* Education Department, Annual Report ya 1937 uk. 6. 47* Education Department, Annual Report ya 1944, uk. 7. 48* Uganda iliendelea kuwakilishwa katika Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki katika miaka yake yote 1930-1964. Kati ya 1945 na 1946 Wakurugenzi wa Elimu wa Afrika Mashariki walikuwa na mikutano ya kujadili suala la kuanzishwa kwa kampuni ya uchapishaji wa vitabu katika chuo kikuu cha Halmashauri ya Fasihi na Lugha ya Afrika Mashariki ambayo baadaye ilikuwa East African Literature Bureau. 78 Kutiliwa mkazo kwa lugha za kwanza katika shule za msingi haku- kufurahiwa hasa huko Buganda. Afisa wa Elimu wa Mkoa alisema kwamba: "Labda jambo lililozusha ubishi mwingi sana kati ya walimu na shule za msingi lilikuwa ni kuondolewa kwa Kiingereza kuwa lugha ya kusomesha masomo mengine katika shule za msingi na kutahiniwa kwa mitihani yote ya mwisho wa mwaka kwa lugha za kwanza. Mabadiliko haya hayajatekelezwa vizuri." 49* Mwaka 1946 Kiswahili kiliendelea kusomeshwa katika shule za msingi za maeneo ambayo yalitaka kisomeshwe. 50* Ripoti ya mwaka 1948 inaonyesha kwamba lugha sita za Kiafrika zilikuwa zimekubaliwa kuwa lugha za kusomesha katika shule za msingi. Lugha hizo sita ni Kiluganda, Kirunyoro-Rutooro, Kijaluo cha Kaskazini, Kiateso, Kilugbara na Kiswahili (Ladefoged et. al. 1971: 91). Mwaka 1949 Kiswahili kilikuwa kikitumiwa kama lugha ya kusomesha masomo mengine katika shule mbili tu (za pekee) za serikali, za watoto wa askari polisi na askari wa magereza. Hii ni kwa sababu Kiswahili kiliendelea kuwa lugha ya mawasiliano ya majeshi. Katika shule zingine zote, watoto walisomeshwa kwa lugha zao za kwanza kufikia darasa la nne. Lugha zingine tano za Kiafrika zilizotambuliwa zilibaki Kiluganda, Kirunyoro-Rutooro, Kiacholi au Kijaluo cha Kaskazini, Kiateso na Kilugbara. Lugha zingine za kwanza zingetumika katika madarasa mawili ya kwanza ya shule za msingi. Kiingereza hakikutumiwa kama lugha ya kusomesha masomo mengine katika shule za msingi isipokuwa katika sehemu chache baada ya kibali maalum. Hata hivyo kilikuwa kikisomeshwa kama somo katika madarasa ya tano na sita na kingesomeshwa mapema zaidi mradi tu kisitatize kusomeshwa kwa masomo mengine. Shule za watu binafsi zilisomesha Kiingereza katika madarasa ya chini na kwa hivyo ziliwavutia wanafunzi wengi. 51* Vyuo vya kuwafunza walimu wa lugha za kwanza ambavyo viliwafunza walimu wa kusomesha madarasa ya kwanza hadi ya nne vilinuiwa kusomesha kwa lugha za kwanza tu pamoja na kusomesha somo la Kiingereza. Katika shule za Magoa lugha ya kusomesha ilikuwa ni Kiingereza kuanzia mapema katika muongo wa 1950. Katika shule zingine za Wahindi, Kihindi na Kigujerati zilitumiwa kusomesha masomo mengine. -- 49* Education Department, Annual Report ya 1945 na 1946 uk. 9. 50* Uganda Annual Colonial Report ya 1946 uk. 51. 51* Education Department, Annual Report ya 1949 uk. 8. 79 Katika shule chache za msingi za Kiafrika ambapo somo la Kiingereza lilianzishwa mapema, ilionekana kwamba hakikuathiri masomo mengine. Kufuatia pendekezo la kundi la Binns na Kamati ya de Bunsen ya 1952, ilikatwa shauri somo la Kiingereza lianzishwe katika madarasa ya chini ya shule za msingi. Kabla ya hapo, somo la Kiingereza halikupendekezwa katika madarasa manne ya kwanza katika shule za msingi. Ingechukua muda kabla walimu wa kutosha hawajafundishwa ili matokeo ya taratibu hii yapatikane. Pigo kubwa zaidi la Kiswahili nchini Uganda lilikuwa tangazo la 1952 kwamba Kiswahili hakitambuliwi tena kama somo katika shule za Uganda. 52* Shule ambazo hazikuhusika ni za polisi na watoto wao. Lugha tano za Kiafrika ambazo tumezitaja ziliendelea kuwa lugha za pekee za Kiafrika zilizotambuliwa katika elimu. Lugha zingine za Kiafrika zinge- tumika tu katika madarasa mawili ya kwanza kama tulivyotaja. Lugha za kusomesha masomo yote katika miaka yote sita ya shule za msingi zilibaki hizo lugha tano za Kiafrika, nacho Kiingereza hakikusomeshwa sana kabla ya darasa la tano. Lakini shule zilihimizwa zianze kukisomesha katika madarasa ya chini. Ripoti ya Idara ya Elimu ya mwaka 1953 inatambua kwamba hata ingawa msimamo wa elimu ni kwamba mtoto hujifunza vizuri anapotumia lugha ya mama yake, lugha za Kiafrika zinazotumiwa katika shule za Uganda si lugha za mama za watoto wengi nchini Uganda. Hii ni kwa sababu ni lugha tano tu zinazotumiwa kielimu katika nchi yenye lugha nyingi. Serikali haikuwa tayari kutumia lugha zote za Uganda mashuleni kwa sababu ya gharama kubwa. Kulikuwa na maoni kwamba ikiwa Kiingereza kingesomeshwa vizuri katika madarasa ya mwanzo ya shule za msingi, watoto wangeanza kukitumia kama lugha ya kusomesha masomo mengine badala ya kubadilisha kutoka lugha ya mama hadi lugha nyingine ya Kiafrika iliyotambulikana (moja kati ya zile lugha tano). Ili kuwafunza walimu wa kusomesha Kiingereza katika madarasa ya mwanzo ya shule za msingi, masomo maalum ya kuwafunza Kiingereza yalitayarishwa mwaka 1954. Mwaka huo huo mafunzo ya kuwafunza walimu wa kusomesha kwa kutumia lugha za kwanza yalikwisha. Baadhi ya vyuo vilivyokuwa vikifunza walimu hao vilifungwa, na vingine vilipanuliwa na kufanywa kuwa vyuo vikubwa. Kuanzia 1958 serikali ilihakikisha kwamba Kiingereza kilisomeshwa kama somo muhimu kuanzia darasa la tatu. Kiingereza kilitiliwa mkazo zaidi mwaka 1960 -- 52* Education Department, Annual Report ya 1952 uk. 8. Tangazo lasema hivi: "Kiswahili si lugha inayotambulika tena katika shule za Uganda, kwa sasa, kinatumika tu katika shule za polisi na watoto wao kwa kuwa kingali lugha rasmi ya jeshi la polisi". 80 baada ya kuunganishwa kwa shule ambazo hapo awali zilikuwa zimega- wanywa katika shule za Waafrika, Magoa, na Wazungu. Kama tulivyojadili katika sehemu hii, kutumiwa kwa Kiswahili katika elimu nchini Uganda kulianza vizuri kukiwa na msaada kamili wa serikali. Kiswahili hakikuungwa mkono na baadhi ya Waganda - hasa Waba- ganda. Kufuata mabadiliko ya siasa katika Afrika Mashariki, Kiswahili kiliondolewa katika shule za Uganda mwaka 1952. Hata baada ya uamuzi huo mkali Uganda iliendelea kuwa mwanachama na kutoa pesa za kuigrarimia Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki hadi 1964. Upinzani dhidi ya Kiswahili uliofanywa na Wabaganda wakati wa ukoloni labda ulitarajiwa kwa vile walivyokuwa na nafasi maalum katika nchi ya Uganda. Hali haiko hivyo tena katika Uganda huru. Uganda, sawa na majirani zake wa Afrika Mashariki na kati, inahitaji Kiswahili katika kujenga umoja wa taifa na kwa mawasiliano ya kimataifa. Kwa muda wa karibu karne moja Kiingereza kimeshindwa kuyatatua matatizo ya lugha ya Uganda. Si lugha ya mwananchi wa kawaida na kingechukua zaidi ya karne nyingine kuwa hivyo. Kiswahili chastahili kupewa nafasi ya kuwa- unganisha wananchi wa Uganda. Hatua ya kwanza ni kuanza kukisomesha katika shule nchini Uganda. Mzee alipotolewa nje alikuwa kama mtu mwenye wazimu. Alikuwa akitetemeka kwa woga. Alitembea kwa haraka kutoka nje. Moyo wangu ulivurugika kwa mchanganyiko wa hasira na huzuni nilipoona mzee akikimbia Serikali yake. Mzee alipokuwa akitoka nje sikuona kitu kingine isipokuwa kwamba wazee walikuwa wakitukimbia. Uhusiano kati yao nasi ulikuwa ukikatika. Niliona wazazi wakiwakimbia watoto wao ambao sasa walikuwa kama simba. Kwa kuwa mzee huyu alikuwa amevaa shati ambalo lilikuwa limepasuka mgongoni niliweza kuona mgongo wake vizuri sana. Kweli niliona wazee wakitupa migongo. Mgongo wa mzee huyu sasa ulikuwa kama ukurasa ambao haukuandikwa maneno; ulikuwa kama ubao mweusi uliofutwa upande mmoja. Maneno yaliyokuwa yameandikwa upande mwingine sikuweza kuyasoma. Mawazo haya yalikuwa bado yakinizu- nguka ndani ya bongo na damu yangu mata tu niliposikia Mkuu wa Wilaya akipiga kelele: "Mwingine aingie!" Yule msichana aliingia. Alipoingia tu Mkuu wa Wilaya alisikika akisema: "Aa! Pili karibu!" Mlango ulifungwa. Mwanzoni walikuwa wakizungumza kwa sauti ya chini, lakini baadaye walijisahau. Walianza kuzungumza kwa 7 sauti ya juu. Hata sisi tuliokuwa nje tuliweza kusikia maneno yaliyokuwa yakisemwa. "Pili, mpango huu unauonaje?" "Hata mimi nimechoka na sinema. Kila Jumapili sinema. Afadhali Jumapili hii twende Serengeti tukawaone wanyama." "Basi kama ni Serengeti inafaa twende Jumamosi ili tulale huko siku mbili maana ni mbali kidogo." "Haya, vizuri. Lakini mimi leo nimechoka sana; utakuja kunichukua jioni twende sinema?" "Tutakuja kama saa mbili hivi. Utamwambia shemeji pia twende naye." Waliendelea kuzungumza kwa muda mrefu. Mambo waliyosema yalikuwa mengi. Mara kucheka, mara "Mimi sitaki", na mara "Huniamini". Nilisikia mlio wa kiti kikibururwa chini. Nafikiri Mkuu wa Wilaya alikuwa akiinuka. "Lete kitambaa changu! Hakika mimi siwezi kutoka nje bila kitambaa kichwani!". Kwa muda mfupi uliofuata walizungumza tena kwa sauti ya chini. Ilikuwa baada ya muda huu msichana alipotoka nje. Nilipokuwa nikiingia ndani nilisikia watu nje wakimgunia. Kweli nilipoingia ndani sikuweza kuamini kwamba aliyekuwa mbele yangu ndiye alikuwa Mkuu wa Wilaya. Alikuwa kijana mwenye umri wa miaka thelathini hivi. Mara tu nilipoingia na kutazamana uso kwa uso kila mmoja aliweka matuta usoni, kwani tulifahamiana tangu zamani. "Habari ya asubuhi," nilimsabahi. "Asante, keti kitini." "Mimi nilikuwa na shida kidogo." "Ndiyo kusema sasa huna." "Nina shida," nilijisahihisha ili kumpendeza. "Natafuta 8 kazi ya muda. Miezi mitatu hivi." "Wewe nani?" Nilikasirika kidogo, lakini hasira yangu niliimeza kwa kuuma meno. "Mimi Kazimoto, mwanafunzi wa Chuo Kikuu - Dar es Salaam." "Huko ndiko mnakofunzwa jinsi ya kuwasabahi wakubwa namna hiyo." "Mimi ninatafuta kazi." "Hata mimi nilipokuwa Makerere nilikuwa nikiwaheshimu watu. Au labda kwa kuwa umesoma Chuo Kikuu unafikiri u mtu tofauti." "Kusoma Chuo Kikuu siyo dhambi," nilimjibu. "Lakini mimi hayo hayakunileta hapa. Mimi ninatafuta kazi." "Huna adabu! Kaa nje kwanza, unanichelewesha kazi bure. Utaingia humu mtu wa mwisho." Nilisimama. Kwa muda nilimtazama machoni. "Unasikia! T-o-k-a nn-nje!" Nilitoka. Msichana aliyekuwa akinifuata aliingia ndani. Kwa kuwa nilikuwa nimekwisha sikia kwamba kulikuwa na kazi nilikaa pale kwa muda; zaidi ya hayo watu walikuwa wamebaki wachache. Yule msichana hakukawia sana mle ndani. Alipotoka nje nilimwona anatembea kuelekea kwangu. Nilifikiri kwamba labda alikuwa ametumwa na Mkuu wa Wilaya kuja kuniambia jambo fulani. "Mwalimu, siku hizi uko wapi?" "Bado ninaendelea na masomo." Ingawa nilimjibu, nilikuwa sikumbuki mahali nilipopata kumfundisha. Nilikuwa nimekwisha fundisha shule nyingi kwa muda. Shule zingine sikumaliza hata miezi miwili. Niliona haya kidogo kuona kwamba kwa muda wote ule 9 nilikuwa nikijitahidi kugusa kiuno cha mwanafunzi wangu. "Kwa muda wote huu ulikuwa bado hujanitambua. Mimi nilipokuona tu nilikukumbuka mara moja." "Samahani, nimesahau jina lako." "Salima." "Siku hizi uko wapi? Habari za Jangwani?" "Jangwani nilimaliza mwaka jana. Siku hizi ninafanya kazi." "Kazi gani?" "Ninafundisha, lakini ninatarajia kuacha kazi hivi hivi karibuni." "Kwa nini?" "Kazi ngumu, pesa kidogo. Haya kwa heri." "Kwa heri, asante." Alipokuwa amekwenda nilikumbuka wazi kwamba Salima alikuwa mmoja kati ya wasichana waliokuwa wakisoma shule ya wasichana ya Jangwani huko Dar es Salaam. Ingawa wakati huo alionyesha mapenzi kwangu, mimi sikutaka, kwa kuogopa kwamba wanafunzi wengine wangetambua wange- fanya fujo na ingekuwa vigumu kuendesha darasa. Zaidi ya hayo ufundishaji wakati huo ulikuwa ni mtihani na mkaguzi alikuwa akikaa darasani. Salima alinifanya sasa nikumbuke tena wale wasichana waliokuwa wakikaa mbele. Wasichana hao, kwa vile walivyokuwa wamezoea kukaa walinifanya nifundishe nikitazama juu ya vichwa vya wanafunzi. Hili ndilo kosa ambalo mkaguzi alinikumbusha karibu kila siku. Wakati nilipokuwa nikifikiria mambo haya niliona mtu wa mwisho anaingia ofisini. Sura ya Mkuu wa Wilaya ilinijia tena kichwani. Nilijongea karibu ili nipate kuingia tena. Ilikuwa wakati huu nilipovumbua kwamba nilikuwa nimesahau kufunga kifungo kimoja cha suruali yangu. 10 Jambo hili lilinuidhi sana. Nilianza kufikiri mabarabara yote ya mjini niliyokuwa nimepita nikiwa katika hali hiyo; pia watu wote niliowaona. Lakini mara mlango ulifungu- liwa. Yule mtu alitoka. Niliingia. "Naam, Bwana mkubwa sana, nafikiri sasa kiburi kimekwisha. " "Mimi sina kiburi. Shida yangu kazi." "Keti." Nilikaa mbele yake, tukawa tunatazamana. Nilipotupa macho juu ya meza niliona visusu viwili. Kimoja kimeandikwa In kingine Out. Ilikuwa ndani ya kile kijikapu cha In nilimoona picha za wasichana watatu ambao sasa niliweza kuwafahamu - Vumilia, Pili na Salima. Ndani ya kijikapu cha Out niliona bahasha za kiserikali. Juu ya meza niliona barua ambayo ilikuwa bado kwisha kuandikwa. Niliweza kuona maneno machache: "Salima natumaini kwamba hutakasirika sana; wale wasichana sina uhusiano nao..." Haya yote niliyaona kwa haraka Mkuu wa Wilaya alipokuwa anafunga kabati, kwani nilipoketi tu juu ya kiti yeye aliinuka. Alipomaliza kufunga kabati nilimwona anachukua funguo zingine mfukoni mwake. Nafikiri zilikuwa funguo za gari lake. "Samahani, ninataka kufunga ofisi. Saa nane na nusu sasa. Utarudi kesho." Nilimtazama machoni kwa mshangao. "Kazimoto, fika kesho asubuhi." Mimi niliendelea kumkazia macho. "Bwana Manase," nilimwita. "Ndiyo, unanifahamu; lakini sasa nimo kazini." "Sasa umo kazini." "Ndiyo." 11 "Manase," nilimwita tena. "Kazimoto," aliniita. Nilisimama pale nikamtazama dakika chache, kisha nikatoka nje kwenda kutafuta chakula; njaa ilikuwa inaniuma. Naam, Mkuu wa Wilaya, Bwana Manase, tulikuwa tukiishi kijiji kimoja. Ukweli ni kwamba tulikuwa majirani. Tangu utoto tulikuwa tumezoeana. Manase alipokuwa bado mtoto mdogo tulikuwa tukimwita "Popo" kwa vile masikio yake yalivyokuwa makubwa. Kati ya wanafunzi tuliokuwa tukisoma darasa la kwanza Manase ndiye alikuwa akifikiriwa kuwa mjinga wa mwisho. Ninakumbuka kwamba siku moja Manase alilia sana darasani bila kupigwa. Sababu yenyewe ilikuwa kwamba mwalimu alimwekea zero kubwa yenye macho mawili na meno yakimcheka. Kwa kuwa alikuwa jirani yangu, mara nyingi alikuwa akishinda nyumbani kwetu na nikimsaidia katika hesabu. Uadui kati yangu na yeye ulianza tulipokuwa darasa la nne. Siku moja, pale shuleni nilichimba shimo dogo na fupi. Ndani ya shimo hili niliweka maji. Niliwaita wanafunzi kama kumi hivi. Walipojongea niliwaambia, "Shimo hili ni refu sana huwezi ukagusa mwisho wake." "Labda kuna nyoka?" wengine waliuliza. "Hapana," nilijibu. Manase alijitokeza. "Mimi ninaweza kugusa mwisho wake," alisema. "Haya jaribu," nilimwambia. Manase alitumbukiza mkono. "Mbona fupi," alisema. "Umegusa chini?" nilimwuliza. "Ndiyo." "Ebu tuzolee mchanga wa chini," nilimwambia. Manase alipotoa mkono, alikuwa amejaza mbolea ya ng'ombe mkononi mwake. Wanafunzi walimzomea, akalia. 12 Tangu siku hiyo Manase alinichukia na nyumbani kwetu hakufika tena kuja kuongea. Kama ilivyo kawaida ya watoto wadogo uadui huu haukuendelea, kwani wakati wa mavuno ulipowadia tulijikuta tunatega ndege pamoja. Baada ya mavuno tulizoea pia kupita mashambani tukitafuta yale mawele yaliyosahauliwa kuvunwa. Yale tuliyopata tulizoea kwenda kuuza kwa padri mmoja wa Kizungu wa misioni yetu. Nakumbuka siku moja baada ya kuuza mawele yetu tulipita kaburini ili kula mapera. Tulipokuwa tumepanda tulisikia viatu vya padri akizunguka kaburini akisoma kitabu kama ilivyo kawaida yao. Tulifikiri kwamba alikuwa hawezi kutuona. Tulikaa kimya mtini. Alipofika karibu na mti tuliokuwa tumeranda alisimama akawa anasoma kitabu chake hapo. Alisimama kwa muda mrefu; halafu tuliona kidevu chake kinainuliwa juu. "Shukeni, ee!" Tulishuka hali tukitetemeka. Alituongoza hadi chumbani mwake. Tulipofika chumbani tuliambiwa kwenda kuzoa mchanga nje. Tulifanya vile. Tulipoingia chumbani tuliambiwa kuumwaga juu ya sakafu, na juu ya mchanga huu tuliamrishwa kupiga magoti. Baada ya muda mfupi tulilia kwa maumivu. Hapo ndipo alipotwambia kulala chini. Tulipigwa fimbo tano tano. "Haya kaeni!" Tulikaa. "Baba zenu nani?" Tulimwambia. "Ninyi watoto wa Wakristo ndio mwaiba mali ya kanisa! Hamfahamu kwamba kuiba ni dhambi? Tajeni amri za Mungu!" Tulizitaja. "Rudieni amri ya saba mara nne!" Tulifanya hivyo. "Mnajua kusoma?" "Ndiyo," tulijibu pamoja. 13 Padri alitupa vijitabu viwili vya Katekesimu. "Haya nendeni nyumbani! " Tulitoka kwa haraka kwa mchanganyiko wa hasira na furaha. Tulikuwa darasa la nane uadui uliporudi tena, lakini mara hii kwa bahati mbaya. Wakati wa mavuno ulikuwa umekaribia, mimi nilikuwa nimesimama juu ya ulingongo katikati ya shamba la mawele la baba yangu; Manase alikuwa katika shamba la baba yake. Tulikuwa tukiwinga ndege. Tulianza mchezo wa kutupiana mawe kwa teo. Kwa bahati mbaya Manase alinipiga kichwani damu ikanitoka. Nilikimbilia nyumbani hali nikilia. Kwa muda hatukuonana tena na Manase. Tulikuwa marafiki tena tuliposhinda wote kuingia darasa la tisa kwani tulishinda kwenda shule moja. Urafiki ulirudi hasa siku niliyomwokoa kutoka mtoni. Tulikuwa tukioga mtoni Manase alipoanguka mahali ambapo maji yalikuwa marefu. Kwa kuwa alikuwa hajui kuogelea alianza kuzama. Wenzangu walikimbia. Mimi niliogelea mara kwenda kumchukua. Karibu nife naye, lakini kwa bahati nzuri niliweza kumvuta mpaka maji mafu. Macho yake yalikuwa mekundu. Jioni hiyo, baba yake aliposikia aliniletea kuku wawili kama zawadi. Wakati tukiwa darasa la kumi, kwa mshangao wa kila mtu, akili za Manase ziliongezeka sana, akawa akiongoza darasa. Mwaka huu mimi sikuumaliza. Nilipatwa na ugonjwa wa kifua kikuu. Nilikaa hospitalini kwa muda wa mwaka mmoja mzima. Nilipotoka hospitalini nilikuwa na nia ya kusoma kufa kupona, lakini mwaka huo baba akashindwa kulipa ada ya shule; shule nikaacha, nikatafuta kazi. Manase akawa sasa miaka miwili mbele yangu. Kazi nilifanya kwa muda wa mwaka mmoja ili kuhakikisha kwamba nilipata pesa za 14 kutosha kuweza kunifikisha darasa la kumi na mbili. Wakati huu wote Manase alikuwa rafiki na jirani mwema mpaka alipomaliza Makerere na kujinyakulia shahada ya B.A. Wakati huu uhuru ulikuwa umekwisha ingia. Jina la Nyerere likawa likiimbwa hata na watoto wadogo. Mwafrika akawa Mwafrika; Mzungu akawa Mzungu; Mhindi akawa Mhindi na Mwarabu akawa Mwarabu. Kwa ufupi kila mtu akaanza kuona ukweli wa hali yake. Aliyejiona tofauti alirudi kwao. Kina Manase wakawa watu waliohitajika sana ili kushika uongozi wa nchi. Manase akawa ofisa mkuu wa elimu, huko Tanga. Alifanya kazi vizuri sana. Akahamishwa hadi Dar es Salaam. Akawa ametolewa kwenye matawi na kuletwa kwenye shina. Ilikuwa wakati huu Manase aliponifanyia ujeuri mkubwa. Alifanya kosa ambalo nilikuwa siwezi kumsamehe. Kisasi kilianza kuukera moyo wangu. Kosa hili ndilo lililotufanya tuzungumze namna ile ofisini. Nilipoingia, kusema haki, nilikuwa sitegemei kumkuta yeye, kwani baada ya kosa hili nilikuwa sifahamu mahali alikokwenda. Baada ya kukumbuka maisha yetu haya ya zamani, na baada ya kulikumbuka kosa hili, nilijikuta nikisema moyoni: "Lazima nijilipize kisasi; nimezaliwa kama yeye; mimi mwanamume kama yeye. Haiwezekani. Lazima nijilipize kisasi." Mara nilistukia nagongana na mwanamke fulani njiani. "Kaka, mbona hivi!" alisema. "Siku hizi hamwoni watu?" "Samahani, dada yangu, mawazo yangu yalikuwa mbali," nilimjibu. "Mawazo gani, unataka kuua mtu?" Sikutaka kuzungumza naye zaidi. Niliendelea na njia yangu. "Sasa ninakwenda wapi?" nilijiuliza moyoni. "Ndiyo, njaa inaniuma, kwa hiyo nilikuwa na nia ya kutafuta hoteli." 15 Nilikumbuka kwamba hoteli niliyokuwa nikitafuta nilikuwa nimeiacha nyuma. Nilirudi. Nyuma kidogo niliona kibao kimeandikwa "Hoteli ya Wananchi". Niliingia ndani kuagiza wali na nyama ya kuku. Wakati nikila watu ambao walikuwa wameenea vumbi waliingia hotelini. Ilionekana kwamba wafanya kazi wa humo hotelini waliwatambua mara moja. Walikuwa wasafiri kutoka Dar es Salaam, kama nilivyokuja kuelewa baadaye. Chakula walicholetewa kilikuwa tofauti na kile walichoniletea mimi. Ingawa nilikuwa mbali kidogo niliweza kuona kwamba wali walioletewa ulikuwa mbaya. Lakini kwa kuwa walikuwa na njaa kubwa hawakuweza kutambua kwamba walipewa uporo. Sikushangaa sana. Mambo haya nilikuwa nimekwisha yaona yakitendeka katika sehemu nyingi za nchi yetu wakati nikiwa safarini. "Mwishowe tumefika, saa ishirini na saba," mmoja kati yao alianza kuzungumza. "Mimi mgongo unaniuma sana, sijui kwa nini?" "Sababu ya mabarabara mabaya." "Sijui serikali inafanya nini?" "Watajali nini wakati wao wanapita hewani?" Mazungumzo yao sikuyafuata zaidi, kwani karibu na meza niliyokuwa nimekaa walikuwa wamekaa wazee wawili wakisimuliana hadithi zao za miaka miwili mitatu iliyopita, na masikio yangu yalivutiwa upande huo. "Bwana we! Niulize mimi nikwambie!" mzee mwenye sharubu alimwambia mwenziwe huku akigonga meza kwa mfupa kusisitiza wazo lake. "Kwa muda wa miaka miwili nilikuwa dereva wa mkuu mmoja wa mkoa. Wewe fikiri mzee kama mimi, mkuu wa mkoa ananiambia 'kanitongozee msichana'. Ni jambo ambalo mara nyingi liliniudhi. Heshima 16 yangu yote kwenda kuipoteza mbele ya msichana mdogo! Na mvi zangu kichwani! Halafu nikishamleta nyumbani kwake au hoteli, anasemaje? 'Utakuja kumchukua saa kumi na moja asubuhi umrudishe.'Mimi usingizi napoteza, yeye analala vyema!" "Wewe unajua upande mmoja tu," mwenziwe alidakia. "Mimi nilikuwa nikishika faili zao za mishahara. Maofisa wote hawa usiwaone nje matumbo kuning'inia! Wengi kati yao wanapokea shilingi mia mbili kwa mwezi!" "Kwa nini?" "Madeni, ndugu yangu, madeni. Utakuta wengi wana mikopo ajabu! Magari yote mikopo; maredio makubwa, yote mikopo; majiko ya kupikia, yote mikopo; karibu kila kitu cha maana kiko chini ya mkopo!" Walipoona kwamba kila mtu alikuwa akiwatazama walimaliza chakula chao wakatoka. Kwa muda kulikuwa na hali ya unyamavu pale hoteli, hali hii ilinifanya nimkumbuke Manase. Niliinuka kwa hasira huku nikiuma meno. Bilauri ya maji iliyokuwa juu ya meza yangu ilianguka na kupasuka. Nilikuwa karibu nitoke nje niliposikia kelele. "Bado hujalipa!" "Samahani," nilisema. Nililipa. Kwa mara ya kwanza wazo la kumkata Manase vipande vipande lilinijia kichwani mwangu wakati nikirudi katika nyumba ya wageni nilimokua nimekodi chumba cha kulala. Jioni sikula. Jioni hiyo kulikuwa na mchezo wa kuigiza katika jumba la maendeleo. Mchezo huo ulikuwa ukichezwa na wanafunzi wa shule ya wavulana ya Nsumba. Nilikata shauri kwenda kuutazama ili kutuliza kichwa changu kidogo chenye kiburi. 17 Wanafunzi hawa walicheza michezo miwili. Mchezo wa kwanza ambao ulichekesha sana watu ulikuwa juu ya baba mmoja aliyekataa kupeleka mtoto wake mgonjwa hospitali. Mchezo wa pili ulikuwa mchezo wa mapenzi. Yule mchezaji aliyefungua mchezo huu alisimama katikati, na kwa sauti, hali akisambaza mikono yake alitamka maneno haya: "Ndugu zangu, katika mchezo huu mtaona kwamba chuki haina nguvu kama wale uwachukiao wanakupenda. Utawezaje kuwachukia wale wakupendao? Kweli, mwanadamu hawezi kumchukia mwanadamu mwenziwe isipokuwa matendo yake. Ndugu zangu, mtaona kwamba kujilipiza kisasi kwa watu wakupendao ndio mwanzo wa mapenzi. Ndugu zangu, mtaona kwamba mwisho wa mwanadamu ulianza alipoweza kutembelea miguu miwili. Pia mtaona ugonjwa utakaowama- liza akina mama wenye mabinti." Aliinama. Watazamaji walipiga makofi. Mchezo ulikwisha saa nne. Nilipotoka nje nilikuwa na nia ya kwenda kulala mara moja, lakini kwa kuwa katika nyumba ya wageni nilimokuwa nimekodi chumba kulikuwa na bar nilikata shauri kunywa kidogo. Mbele yangu alikuwa amekaa mwanamke mmoja aliyekuwa akinitazama mara mbili mbili. Mimi sikuonyesha alama yo yote ya kumhitaji; nilikunywa pombe yangu kimya. Mbwa abwekaye haumi, aumaye ni yule kimya. Hii ndiyo ilikuwa njia yangu kupata wanawake. Nilipoagiza chupa ya pili mwanamke huyu alikuwa amehamia karibu nami. "Unakunywa nini?" "Tusker," alijibu kwa haraka. Niliagiza chupa mbili za Tusker. Tulikunywa pamoja mpaka saa sita. Walipofunga bar nilinunua chupa moja ya Grenado. Chupa hii tuliinywa pamoja chumbani mwangu. "Unatoka wapi?" aliuliza. Nilimwambia. 18 "Jina lako nani?" Nilitafuta moja. "Kumbe unatoka sehemu moja na Manase." Nilikubali. "Mhuni huyo! Amemwachisha kazi mwalimu mmoja, sasa anaishi pamoja naye." "Salima?" niliuliza kwa mshangao. "Huyo huyo! Lakini siye huyo peke yake, ana msichana mwingine katika mtaa wa Uhuru." "Ndiyo kusema anataka kumwoa Salima?" "Inaonekana vile, lakini tena tunasikia baba yake amekwisha kumtafutia mchumba mwingine huko nyumbani kwao. Wanasema kwamba Bwana Manase amemkataa kwa sababu ni mshamba mno; wengine wanasema anataka kuwaoa wote wawili." Nilihisi kwamba huyo msichana wa shamba alikuwa Vumilia. Mawazo juu ya Manase yalianza tena kuvuruga akili zangu. Nilianza kunywa pombe nyingi ili nilewe upesi nisahau mambo. Chupa ilikuwa bado kwisha mawazo haya yalipopotea: mwanamke huyu aliweka kichwa chake juu ya miguu yangu. "Bwanangu, mimi usingizi umenipata, tukalale!" Hakuweza hata kusimama. Nilimbeba hadi kitandani. Hata nguo nilipaswa kumvua. Nilishangaa kukuta hirizi kiunoni mwake. Hirizi hii niliitoa na kuiweka juu ya meza. Baada ya kumvua nguo zote nilifunga mlango, nikazima taa. "Utakwenda lini nyumbani?" yule mwanamke aliniuliza asubuhi. "Kesho." "Utalala humu tena?" "Ndiyo." "Leo usiku usinipe pombe nyingi." "Kwa nini?" "Ninataka kukuonyesha mchezo halisi wa kwetu." 19 "Ahaa!" Wakati huo alikuwa akijaribu kuinuka kutoka kitandani. "Usinitazame!" aliniambia. Nilitazama pembeni. "Aa! Iko wapi?" alipiga kelele. "Nini?" "Hirizi yangu ! " "Hiyo hapo mezani." "Kwa nini uliitoa?" aliuliza kwa wasi wasi. "Kwa nini nisiitoe?" "Mimi siwezi kutunza mtoto wako." Alivaa nguo kwenda kuoga. Baada ya kuoga tulipeana kwa heri ya kuonana. Alipokuwa amekwenda nilikumbuka kwamba nilipaswa kumwona Manase asubuhi hiyo. "Jambo zuri ni kwamba nilipata usingizi," nilisema moyoni. Wazo la kufika tu ofisini nimchome Manase visu vya tumboni lilinijia tena kichwani. "Huenda nami nikanyongwa," nilisema moyoni. "Sitapata faida yo yote isipokuwa kuwaacha wazazi wangu taabuni. Jambo la maana ni kujaribu kumpa Manase maisha magumu hapa duniani. Nisipoweza basi nitajilipiza kisasi kwa njia ingine." Nilikata shauri kwenda kumwona Manase ofisini kila kisu. Siku ya kwanza nilipoingia ofisini kwa Manase nilikuwa na nia ya kuomba kazi ya muda. Yeye alifikiri kwamba nilikuwa nakuja kumwuliza juu ya kosa alilofanya. Kwa hiyo alijaribu kutumia lugha kali kama kwamba nilikuwa nakuja kwa ugomvi. Kwa kuwa siku hiyo sikusema neno lo lote kuhusu jambo hilo Manase aliona kwamba sikuwa na kinyongo. Sasa nilipoingia hakuwa mkali kama siku ya kwanza. "Karibu ukae, Kazimoto," alisema mara tu nilipoingia. "Asante." "Kuhusu habari ya kazi nafikiri utapata. Tunahitaji vijana kama nyinyi katika kufanya kazi hii ya kuhesabu ng'ombe. 20 Wewe utapata shilingi mia sita kila mwezi ufanyao kazi." Alifungua kabati kutoa karatasi za maswali na mambo mengine yaliyohitajika kujazwa. Alinipa mkononi. "Nafikiri sasa umefurahi, sivyo? Unaweza kwenda." Nilikuwa karibu kutoka nje nilipofikiri kwamba ilikuwa lazima nimwulize juu ya jambo hilo alilotenda - tendo la kinyama. "Manase," nilimwita. Alinitazama. "Jambo gani ulifanya?" nilimwuliza hali nikimtazama usoni. Mara moja sura ilimgeuka. Nilimwona anafungua mdomo pole pole. "Kazimoto, huelewi vizuri hadithi yenyewe." "Hadithi nimekwisha isikia, Manase." "Halikuwa kosa langu." "Ni kosa la nani?" "Hakika Rukia mchokozi sana. Yeye ndiye alinianza." "Alikuanzaje?" "Unaona. Siku moja usiku nilipokuwa nimekwisha lala usingizi nilisikia mtu anagonga mlango wangu, 'Nani huyo!' nilisema kwa sauti. 'Ni mimi Rukia, fungua mlango.' Kuna nini?' nilimwuliza. 'Wewe fungua mlango tu'. Nilipofungua mlango aliingia chumbani mwangu; alilala juu ya kitanda changu. Sasa wewe fikiri Kazimoto, mwanamume kama wewe ungefanya nini?" "Mambo yote ninayafahamu. Unafikiri sifahamu maisha yako?" "Hata mimi ninayafahamu maisha yako. Ninafahamu kwamba usiku ulikuwa na Pili. Huwezi kunidanganya kwamba wewe bikira katika mambo haya (nilishangaa kwa nini sikuweza kumtambua Pili: mwanamke akiwa mawindoni hugeuka sura). Pia ninayafahamu maisha ya Rukia. Bila shaka utakubaliana nami nikisema kwamba Rukia alikuwa malaya tangu alipoota maziwa." 21 "Unamwita malaya!" nilisema kwa hasira. "Ndiyo." "Hebu sema tena!" "Rukia ni malaya. Kama umekasirishwa na jambo lililotokea kwa bahati mbaya unaweza kufanya jambo lo lote upendalo! Sijali sasa! " alisema kwa hasira. "Sasa hata kazi hupati!" Karatasi nilinyang'anywa. "Tutaona! " nilimwambia kwa hasira kubwa. Nilipokuwa njiani kelekea chumbani kwangu niliweza kuyakumbuka yale maneno barabara. Nilijaribu kuyarudia moyoni: "Ndugu zangu, katika mchezo huu mtaona kwamba chuki haina nguvu kama wale uwachukiao wanakupenda. Utawezaje kuwachukia wale wakupendao? Kweli..." 22 2 Rukia hakuwa mwingine isipokuwa ndugu yangu aliyenifua- ta mimi. Ndugu mwanamke pekee, mwema, ndugu mfanya- kazi. Uzuri wake, kama nilivyosikia watu wakisema, ulikuwa uzuri wa aina ya pekee. Uzuri ambao hata kipofu aliweza kuuona. Kwa hiyo sisi nyumbani tukawa tunaona mwanga mbele ya maisha yake. Tabia yake, kama tulivyoiona nyumbani, ilikuwa nzuri ingawa ni vigumu kufahamu mambo ya wasichana. Kwa kuwa alikuwa mzuri Baba na Mama walitaka kumwachisha shule ili aolewe, kwani alipokuwa bado darasa la sita alikuwa amekwisha chumbiwa na vijana watatu. Mawazo ya wazazi wangu niliyapinga, nikayashinda. Rukia alishindwa kuingia darasa la tisa, lakini mimi nilikuwa na nia ya kumwelimisha. Nilimtafutia shule, na baada ya kupita kichinichini kama ilivyokuwa kawaida, nilipata shule moja huko Dar es Salaam. Taabu sasa ikawa 23 mahali pa kupanga: shule yenyewe haikuwa na malazi kwa wanafunzi. Manase wakati huu alikuwa akiishi Oysterbay, na kwa kuwa alikuwa na nyumba kubwa nilifikiri ataweza kuishi na ndugu yangu. Licha ya nyumba kuwa kubwa wakati huu ulikuwa wakati ambao uhusiano kati yangu na yeye ulikuwa mzuri. Nilipomwambia Manase taabu yangu alikubali kukaa na ndugu yangu. Wakati huo mimi nilikuwa nimekwisha ingia Chuo Kikuu. Mwaka wa kwanza nafikiri ulipita salama. Mambo yalianza mwaka wa pili alipoingia darasa la kumi. Nilipozungumza naye mwaka huo alinieleza kwamba alikuwa na shida kidogo tu. Kwa kuwa hakueleza vizuri shida yake nilifikiri kwamba ilikuwa njia ya kuzungukia akitaka kuomba pesa. Nilimpelekea shilingi sitini, nikitumaini kwamba msichana aweza tu kujitunza akiwa na pesa za matumizi. Nilipokutana naye siku ingine alinishukuru kwa pesa nilizompa, lakini katika mazungumzo aliniuliza swali ambalo lilinitia wasiwasi. Alisema: "Sijui Manase ni mtu wa namna gani." Hapo ndipo nilipoanza kuhisi kiini cha shida yake. Niliona wazi kwamba Manase alikuwa akijaribu kufanya mambo yasiyotakikana. Siku chache baadaye nilipata barua kutoka kwa ndugu yangu. Ilikuwa imeandikwa kwa hasira. Msitari wa kwanza ulisema: "Kaka usiponitafutia mahali pengine pa kukaa mimi nitarudi nyumbani. Heri kuacha shule!" Niliona kweli kwamba alikuwa amekwisha sumbuliwa sana. Siku hiyo nilipanda basi hadi Oysterbay. Nilipofika nyumbani kwa Manase sikukuta mtu ye yote nyumbani, isipokuwa mbwa aliyekuwa amefungwa karibu na mlango kulinda wezi. Nilirudi mjini. Nilijitahidi kutafuta nafasi, lakini rafiki zangu wengine waliokuwa wakiishi mtaa wa Magomeni Mapipa 24 walikuwa na vyumba viwili tu. Chumba cha maongezi na chumba cha kulala, basi. Niliona hatari zaidi katika uchache wa vyumba kuliko katika tabia ya mtu mwenyewe. Kwa hiyo nilimwandikia barua ndugu yangu nikimweleza shida ya kupata mahali pengine. Nilimwomba avumilie, mwaka huo uishe. Kwa muda wa mwezi mmoja sikuonana naye na sikupata barua kutoka kwake. Nilifikiri kwamba Manase alikuwa ameacha mchezo wake na kwamba ndugu yangu alikuwa akiishi bila kusumbuliwa. Ilikuwa baada mwezi mmoja uliofuata nilipopata tena barua kutoka kwake, nayo nilipoifungua ilikuwa imeandikwa, juu kabisa, neno "SIRI". Niliisoma. Kaka mpendwa, Moyo wangu siku hizi hauna raha. Lakini leo nimechukua kalamu ili nikueleze mambo yote. Nimeona kwamba siwezi kuwa nakuficha wewe mambo, hali mambo yenyewe sasa hayawezi kufichika. Wewe ukiwa kaka yangu na ndiye uliyenitafutia nafasi hii ya shule ninakupa heshima. Fahamu kwamba mambo haya sijapata kumweleza mtu mwingine isipokuwa wewe peke yako. Kaka, uliponileta hapa nilikaa kwa raha kwa muda wa juma moja tu. Baada ya juma hiyo niliona Manase anaanza kunitazama kwa njia ya ajabu. Baada ya majuma mawili mambo yalizidi kuwa mabaya, kwani nilipokuwa naoga siku moja niliona jicho lake kwenye tundu la ufunguo. Mwishowe aliniambia wazi alichokuwa anataka. Nilimwambia: 'Manase! Kaka yangu akifahamu litakuwa jambo la aibu sana!' Lakini yeye alijibu 25 kwamba wewe ni mwanamume kama yeye. Alifikia hata hatua ya kutumia nguvu! Na kweli alitumia nguvu bila utashi wangu. Kaka, sitaki kukupotezea muda wako wa kujifunza kwa kusoma barua ndefu. Mimi maisha yangu yameharibika. Shule nimekwisha acha. Jambo ambalo limenisikitisha sana ni hili lifuatalo: Jana usiku, Manase alirejea nyumbani mlevi. Alikuwa na tikiti ya basi. Baada ya kunitukana kwa maneno ambayo siwezi kukuandikia alianza kupanga vitu vyangu sandukuni. Leo atanisindikiza hadi kituo cha basi. Kaka, machozi yanilengalenga, sijui nitasema nini kwa Baba na Mama. Usifike kuja kuniaga kwenye kituo cha basi nisije nikazimia. Sina mengi. Nduguyo, Rukia Mafuru. Hasira iliyonipata baada ya kusoma barua hii haina kifani. Nilijikuta nasema moyoni "Kulikokuwa na mwanga sasa giza! Manase ana kiburi namna gani! Mimi mwanamume kama yeye!" Kwa muda wa siku moja sikuweza kuhudhuria masomo kwa vile kichwa changu kilivyokuwa kimevurugika. Wakati huu sikuweza kwenda kumwona Manase. Hasira yangu ilikuwa kubwa vile kwamba kama ningekwenda bila shaka ugomvi na vita vingalitokea. Licha ya hasira wakati wa mitihani ulikuwa umekaribia, nami nikiwa mwaka wa pili nilipaswa kufanya vizuri ili kuingia mwaka wa tatu. Miezi miwili ilipita. Na baada ya mitihani nilikata shauri kwenda nyumbani nikiwa na wazo la kutafuta kazi ya muda 26 kama ikiwezekana. Wakati huu sikuwa na habari kwamba Manase alikuwa amekwisha hamishwa. Nikiwa ndani ya stima kuelekea nyumbani kisiwani, hadithi hii yote ilinijia kichwani tena. Nilitoa ile barua niliyoandikiwa na ndugu yangu. Niliisoma tena kwa makini kuona kama kulikuwa na uwongo ndani yake. Niliona wazi kwamba Manase alikuwa akisema uwongo. "Manase anamwa ndugu yangu malaya!" nilisema moyoni. Niliikunja ile barua nikairudisha mfukoni. Nilianza tena kufikiri jinsi ya kujilipia kisasi. Nilikumbuka kwamba nilikuwa nimekata shauri kufanya maisha yake yawe magumu hapa duniani. Watu walipoanza kuinuka waliniondoa katika ndoto. Nilipotazama nje niliona kwamba mji wa Nansio ulikuwa umekaribia. Niligundua kwamba hata stima ilikuwa imekwisha punguza mwendo. Baada ya dakika tano tulifika. Nilipotoka nje nilikwenda nilikwenda mara moja kwenye kituo cha basi. Kwa nauli ya shilingi moja nilipanda basi lililokuwa likipita katika kijiji cha kwetu-Mahande. Kutoka barabarani pale basi liliponishusha, ulikuwa mwendo wa kilometa moja kufika nyumbani. Njiani nilikutana na watu wengi; ajabu ilikuwa kwamba kila mtu niliyekuwa nikikutana naye njiani alinitazama kwa mshangao hata wale walionifahamu. Mtu wa kwanza kuzungumza naye alikuwa kijana mmoja tuliyekuwa tukisoma pamoja zamani. Yeye sasa alikuwa ameoa na alikuwa na watoto watatu. "Wewe kwa nini umekuja nyumbani?" aliniuliza kwa mshangao bila hata kunisalimu kwanza. "Kwa nini? Mbona huwa nakuja nyumbani karibu kila likizo?" "Heri ungebaki huko. Huku umejileta hatarini." "Hatari gani?" "Hatari gani? Hujui? 27 "Hata sina habari!" "Ndugu yangu, utasimuliwa nyumbani." Aliponiambia maneno haya ya mwisho alikwenda zake. Sikupata nafasi ya kuweza kumwuliza zaidi. Lakini nilianza kufikiri moyoni ni mambo gani aliyokuwa akizungumzia. Sikuweza kuelewa. Mtu wa pili kukutana naye alikuwa mzee. Mzee huyu alikuwa akipeleka ng'ombe wake mtoni kunywa maji. Alikuwa ameenea vumbi nyweleni. "Kazimoto! Umekuja kujionea mwenyewe!" alisema. "Kuona nini?" "Ha! Huna habari?" "Hata sina!" "Mambo fulani yametokea pale nyumbani kwenu ambayo yameshangaza kijiji kizima cha Mahande." Nilianza kufikiri kwamba mimba ya ndugu yangu ndiyo ilikuwa ikikanganya kijiji kizima. Lakini kwa wakati huu hili halikuwa tena jambo la ajabu kama zamani. Lilikuwa limekwisha tokea kwa wasichana wengi kijijini, wasomao na wasiosoma. Zaidi ya hayo kwa njia gani mimba ya ndugu iliweza kuniweka hatarini? Nilikuwa nimekaribia kisima walichokuwa wakikoga na kuteka maji wanawake wa kijijini. Njia hii ilikuwa ikipita karibu sana na kisima hiki. Nilipokaribia karibu kabisa, nilisikia sauti za wasichana. Kama ilivyo desturi, nilipiga kelele. "Vaeni nipite!" "Nani wewe?" "Vaeni wanaume tupite!" "Ngoja kidogo!" walijibu. Baada ya muda nilisikia, "Tayari!" Nilipojitokeza walikuwa bado hawajavaa. Nilipita na sanduku langu, sasa begani, hali nikitazama pembeni. 28 Niliwasikia wakicheka. Lakini mimi sikuwatazama. Nilisikia wakimwambia msichana mmoja: "Furahi basi! Bwana yako amekuja!" "Sasa mnataka nini?" msichana yule aliwajibu. "Mbona sanduku lataka kumwangusha na wewe huendi kumpokea?" Nilifahamu huyo msichana alikuwa nani. Hata nilipokuwa nimefika mbali kidogo niliweza bado kusikia sauti zao. Walikuwa wakicheka. Niliona kwamba sasa wakati wa kusahau vitabu ulikuwa umeingia na kwamba nilikuwa nimeyafikia maisha yanayoitwa "maisha". Njia ya kwenda nyumbani kwetu ilipita nyumbani kabisa kwa Mzee Kabenga - baba'ke Manase. Nilimkuta Kabenga amekaa juu ya kichuguu kilichokuwa karibu na mji wake, fimbo mkononi, akitazama ng'ombe wake wawili wakila majani. "Kazimoto," alisema kwa unyenyekevu, "sisi tu wazima, lakini mambo yanayotokea nyumbani kwenu hapo yanatushangaza." "Mambo gani?" "Wewe nenda tu nyumbani. Baba yako hutamkuta, lakini nafikiri mama yako ataweza kukueleza." "Amekwenda wapi?" "Hayo pia mama yako atakueleza." Nilipokuwa nazungumza na Mzee Kabenga sauti yangu ilikuwa imesikika nyumbani. Niliwaona wadogo zangu wanakuja mbio kama kwamba atakayekuwa wa kwanza kunifikia atapata zawadi. Mara moja sanduku langu lilichukuliwa juu juu. Wengine hawakupata mzigo. "Mimi ndiye nilikuwa wa kwanza kumwona." "Mimi nilimsikia zamani!" 29 "Baba amekula kuku wako wote; alikuwa anasema kwamba ukifika tukwambie kwamba wameliwa na bweha!" "Machungwa yameiva; mwaka huu mengi sana!" Mwishowe nilikata shauri kuzungumza nn mmoja tu kati yao yaani Kalia, mtoto ambaye nilikuwa nampenda sana kati ya wadogo zangu. "Baba yupo nyumbani?" nilimwuliza Kalia. "Baba! Nyumbani hayupo!" "Amekwenda wapi?" "Sisi hatukuambiwa." "Nyumbani kuna mambo gani?" "Siku hizi hatulali!" "Kwa nini? " "Utaona leo usiku. Siku hizi wanafika karibu kila siku." "Watu gani?" "Watu gani? Nani anawafahamu? Hakuna ambaye amekwisha waona." "Wewe, Kalia, endelea tu kusemasema mambo hayo. Wewe ndiye utapigwa leo," wenziwe walimwonya. "Nani atawapiga?" niliwauliza. Wote walinyamaza. Tulikuwa tumefika nyumbani. Kuingia tu niliona kwamba kulikuwa na mambo fulani ambayo yalikuwa hayaendi sawa. Kila mtu alikuwa na huzuni. Kila mtu alikuwa akitembea pole pole kama mgonjwa, wala hapakuwa na mtu aliyefurahia sana kufika kwangu nyumbani kama ilivyokuwa kawaida nyakati zingine. Hata Mama hakufurahi. Nilipomwona dada yangu Rukia na tumbo kubwa, fikara kwamba Manase alikuwa amemharibia maisha yake ya mbele zilinijia kichwani. Alinisalimu kwa mbali hali ameinamisha kichwa. Hakujaribu kunitazama usoni. Mimi niliona kwamba tatizo la Rukia ndilo lilikuwa bila shaka tatizo lililokuwa likiwasumbua. Lakini baada ya kusalimiana na Mama 30 aliyekuwa amekaa juu ya ngozi ya mbuzi kwa huzuni, nilishangaa kuona kwamba hakuzungumza juu ya tatizo hili la Rukia. Badala yake alianza kuniuliza kwa nini nilikuja nyumbani. "Hufahamu kwamba sisi wote hapa maisha yetu yamo hatarini? Kwa kuwa wewe umesoma nafikiri we ndiwe utakuwa wa kwanza kuuawa." "Kuuawa na nani?" "Ungekuwa mtu mwenye kusikia maneno ya watu ningekwambia urudi huko ulikotoka." "Kwa nini?" "Hayo si mambo ya kuuliza." "Na Baba amekwenda wapi?" "Nitakueleza kesho pumzika kwanza." Wakati huo huo niliona moshi unaanza kutoka jikoni na Rukia alikuwa humo amekaa karibu na mafiga. Nilipomaliza kula nilianza kufungua sanduku langu ili kutoa matandiko na kutayarisha kitanda. Nilikuwa nikipanga vitabu vyangu mezani niliposikia mtu akibisha hodi. Nilifungua. Kabenga akaingia. "Karibu, Kabenga, karibu," nilisema. "Asante, mwanangu," alijibu. "Karibu kiti, usiogope." "Vitabu hivi vyote umekwisha vimalizia kichwani?" aliuliza huku akikaa. "Mbona nimekuja na vichache tu, vingine nimeviacha huko huko shuleni." "Mm! Mna kazi!" "Kazi tunayofanya ni kubwa mno; ngumu kama ya jembe." "Ah, mtoto wangu, usiseme kazi ya jembe. Kazi ya jembe inamnyofoa mtu hata anakuwa mzee siku si zake." 31 "Sisi jembe letu ni kalamu." "Kweli, lakini kalamu haimfanyi mtu akatoka jasho." Alinyamaza kwa muda mfupi. "Kazimoto," alianza tena, nimekuja kuuliza kama una habari yo yote kuhusu mtoto wetu. "Mtoto gani?" "Huyu mwenda wazimu," alijibu. "Manase?" "Huyo huyo." "Kwa nini unamwita mwenda wazimu?" "Kazimoto, hata wewe unafahamu. Mambo aliyoyafanya hayakutupendeza, mimi pamoja na wazazi wako. Wewe fikiri, watu tumesikilizana namna hii kwa muda mrefu, halafu Manase anatenda jambo kama hili!" "Hata mimi niliposikia nilishangaa," nilisema. "Ni mwenda wazimu. Ninakwambia ukweli ni mwenda wazimu. Tena kabla ya kuendelea ningependa utusamehe kwa mambo aliyoyatenda. Ni mwenda wazimu! Wewe tazama - ndugu yako alipokuja nyumbani na kutueleza yote yaliyotokea, mimi pamoja na mke wangu Tuza na wazazi wako tulikata shauri amwoe. Tulimwandikia barua, na wote tuliweka sahihi zetu. Mimi nilianza kazi ya kuposa. Barua ya kwanza tuliyopata kutoka kwake ilisema kwamba atafikiri. Hii hapa, unaweza kuisoma." Niliisoma. "Umeona?" "Ndiyo." "Sasa, baada ya muda tulimwandikia tena barua tukimwuliza kama alikuwa amekwisha kata shauri. Kusema kweli tulimwambia wazi kwamba hapakuwa na haja ya kukata shauri: alikata shauri siku ya kwanza alipoanza mambo hayo. Lakini barua aliyotuandikia tena ilikuwa ya kijinga. Isome mwenyewe, mimi siwezi kukwambia maneno ya kijinga kama 32 hayo kwa mdomo wangu." Niliichukua na kuisoma. Haikuwa ndefu: Ninawaarifuni kwamba kwa sababu fulani kubwa siwezi kumwoa Rukia. Nimekwisha pata mchumba mwingine, na mzuri kuliko Rukia. Kama nia yenu ni kutaka mimi nioe, semeni tu, nami nitawaambia mahali anapoishi ili muanze kazi ya kuposa. Lakini Rukia siwezi. "Umeona sasa kijana mwenzio!" "Nimeona." "Sasa sisi hatufahamu jambo la kufanya. Lakini siwezi kuamini kwamba mtoto wangu Manase anaweza kuharibu uhusiano wetu mzuri kati yangu na baba'ko. Vijana vya siku hizi! Eti mpaka mjichagulie wenyewe! Msichana mzuri huonekana na watu wengi. Hivi ulipokuwa safarini kuja huku hukupata kuonana naye?" "Ndiyo, nilimwona." "Alisemaje?" "Hata mimi mwenyewe niligombana naye. Anamwita ndugu yangu malaya." "Unaona sasa! Watu mmesoma pamoja." "Manase anaonekana kuwa mtu mwenyewe kiburi sana siku hizi." "Hicho ni kiburi hakika, na kiburi hakifai." Kabenga alitikisa kichwa chake kwa huzuni. "Hata kama amekataa kumwoa msichana huyu, maadam amekubali kwamba mimba ni yake angekuwa anamtumia pesa za matumizi mbeba mwana. Lakini mtoto wetu amekataa. Kama angetuma pesa sisi tungeendelea kumnunulia samaki mpaka atakapojifungua, maana mtoto ni wetu." 33 Tulinyamaza kwa muda. "Labda una habari zo zote juu ya binti yangu Sabina," aliniuliza. "Sabina sina habari zake maana huwa hatuandikiani barua." "Labda naye amekwisha pata mimba, nasikia siku hizi anafundisha huko Tabora." "Sabina ni msichana atunzae usafi." "Dansi ya kushikana wawili-wawili ilipoingia nchini usafi ukaisha, mwanangu." "Atakuja lini livu," niliuliza. "Ametuandikia barua kwamba atakuja mwezi ujao. Mama yako amekwisha kueleza mambo yanayotokea hapa?" "Hata kidogo." "Labda atakueleza baadaye." "Ni mambo gani hayo?" "Mambo haya yalianza kuonekana na baba yako. Alipojaribu kufahamu watu wanaofanya hivyo alipigwa. Baadaye alikuja kuniambia mimi. Tukiwa wawili tulijaribu kuwatafuta kwa mikuki lakini kila mara nilipokuwapo hawakuonekana. Ni wajanja sana." "Mimi nitajaribu kuwapiga," nilisema. "Wewe bado mtoto mdogo, afadhali usijaribu, watu hao wana nguvu sana. "Wana nguvu sana!" nilistaajabu. "Ndiyo. Mambo yenyewe si ya kuambiwa, Kazimoto, utayaona mwenyewe karibuni. Kijiji kizima kinafahamu." "Kuna habari fulani ambazo zimenishangaza sana," nilisema. "Habari gani?" Kabenga aliuliza. "Nimesikia kwamba Manase atamwoa Vumilia karibuni. Kabenga alishangaa. Hakuwa na neno la kusema kwa muda. "Hayo pia nilikuwa nataka kukwambia. Mimi huwa sifichi jambo lo lote," alisema. 34 "Nieleze, nilimwambia. "Kwanza nikuulize swali moja," alisema. "Uliwahi kusikia kwamba Manase ana kimada?" "Nimesikia kwamba siku hizi ni kama ameoa." "Jina la msichana huyo nimelisahau kidogo lakini ni jina kama Salima." "Salima! " "Ndiyo, Salima. Sasa tuliposikia kwamba mtoto wetu amepotoka na kwamba anataka kuoa mwanamke kutoka mbali tulikata shauri kumtafutia mchumba mwingine. Mke wangu Tuza akatoa wazo kwamba tumchumbie Vumilia kwa sababu tuliona alikuwa hawezi kushaurika kumwoa Rukia. Unaona?" "Nimeona." "Hata Manase naye tumemwandikia barua amekubali kumwoa Vumilia. Kama mambo yakienda vizuri nafikiri atamwoa baada ya miezi miwili." Kabenga aliyasema maneno haya hali akiinuka kwenda nyumbani kwake. Giza lilikwa limekwisha ingia. Aliniacha mimi na mawazo mengi. Ilikuwa usiku tunakula na wadogo zangu karibu na moto. Wanawake walikuwa wakila jikoni, niliposikia mbwa wanaanza kubweka hali wakitazama upande kulikokuwa mwembe. Niliona watoto wanaanza kutetemeka kwa hofu. Wanawake jikoni walikaa kimya. "Kuna nini?" niliuliza. Watoto walinyamaza. "Sh! Kamata!" niliwahimiza mbwa wawili. Hapo hapo nilisikia sauti ya Mama kutoka jikoni. "Kazimoto! Unataka kufanya nini? Wewe nyamaza tu! Sikutaka kusikiliza maneno ya Mama. Niliinuka. Nilikwenda 35 chumbani kwa Baba kuchukua mkuki. "Sh! Kamata!" Mbwa waliponiona nakuja na mkuki mara moja walikimbia kuelekea kwenye mwembe, mimi nikawa nawafuata nyuma. Kwa kuwa nilikuwa nimekaa kwenye moto kwa muda mrefu, sikuweza kuona vizuri. Nilikuwa sijafika mbali niliposikia mbwa mmoja aliyekuwa ametangulia anabweka. Nilimwona anarudi akichechemea, mguu mmoja juu, huku akilialia kwa maumivu. Mbwa wa pili alikimbilia miguuni mwangu. Wadogo zangu walikuwa wamekwisha kimbilia jikoni. Hofu kubwa ilinipata kama kwamba simba wa Tsavo walikuwa mbele yangu. Hofu yangu ilikuwa kubwa zaidi kwa sababu sikuwa na bunduki, na wala sikufahamu hatari iliyokuwa mbele yangu ilikuwa kubwa kiasi gani. "Umeona?" Mama alisema. "Unafikiri wewe mwanamume kuliko baba yako?" Nilirudisha mkuki mahali nilipoutoa. Nilikwenda ndani ya nyumba yangu kulala. Nilipofika kitandani nilianza kufikiri: "Haya ndiyo mambo niliyokuwa nikiambiwa. Hao ndio watu wanaosemekana kuwa na nguvu. Lakini kwa nini wawe wanakuja nyumbani kwetu tu? Sijui nifanye jambo gani ili niweze kuwakomesha! Siamini kwamba kuna wachawi duniani. Lazima tu wawe watu wa kawaida. Na ni watu ambao wanaishi kijijini humu humu." Niliona kwamba watu wote wa nyumbani kwetu walikuwa wamekwisha nyang'anywa utu wao, hapakuwa na mtu tena pale nyumbani. Sikutaka kugeuzwa na hofu kama wao; wao walikwisha kuwa watu ambao hawawezi hata kuguna. Niliona kwamba kazi kubwa iliyokuwa ikinikabili sasa ilikuwa siyo ya Rukia lakini kufikiria njia ya kuweza kuwakomesha watu hawa waliokuwa wakiuchezea mji wa kwetu. 36 Usingizi ulikuwa bado kunipata wadogo zangu walipokuja kulala chumbani ndani ya nyumba yangu. Rukia alikwenda kulala na Mama ndani ya nyumba ya Baba. Usiku wa manane nilisikia vishindo nti! nti! kuzunguka nyumba yangu. Hofu ilinishika lakini nilipiga moyo konde. Niliamka kwenda kuchungulia dirishani. Mara vishindo vilikoma, lakini sikuweza kuona mtu ye yote. Vishindo vilipoacha kusikika nilikwenda tena kulala kitandani. Nilikuwa bado sijajifunika niliposikia ndani ya nyumba ya Baba, Rukia na Mama wakipiga mayowe: "Tumekufa ! Tumekufa! " Mara moja nilitoka nje na shuka yangu pamoja na panga maana mimi ndiye mwanamume peke yangu niliyekuwa nikitegemewa. "Kuna nini?" niliuliza. Nilipofika karibu na nyumba nilisikia watu kama wawili wakikimbia. "Fungueni mlango!" Walifungua, nikaingia: Niliona mchanga mwingi sana juu ya vitanda. "Basi - " Mama alisema, "mchanga huu ulikuwa ukimwagika kama mvua kupitia dirishani. "Ondoeni mchanga mlale," niliwaambia. Walifanya hivyo. Niliondoka kwenda nyumbani mwangu. Nilikuwa bado sijafika niliposikia wadogo zangu wanalia. Nilipoingia tu, mchanga haukumwagwa tena. Nilikata shauri kulala na kuwaacha wafanye mambo yao. Sikusikia vishindo tena nilipolala kitandani. Kwa muda nilifikiri juu ya maajabu haya, lakini mwishowe usingizi ulinichukua mpaka asubuhi nilipoamshwa na Kalia. Wakati nikipiga mswaki asubuhi nilitembeatembea kuzunguka mji nikitazama chini. Niliweza kuona nyayo za watu, lakini sikuweza kuzitambua. Nilipofika chini ya mwembe niliona nyayo nyingi. Ilionekana kwamba hapo ndipo walipokuwa wamesimama. Siku nzima sikuwa na raha. Nilikuwa nikifikiria jambo la 37 kufanya. Hata chakula cha mchana sikula vizuri. Baada ya kula nilijaribu kusoma hadithi lakini niliona kwamba nilikuwa siifuati. Nilitupa kitabu juu ya meza, nikachukua sabuni kwenda kuoga mtoni. Niliporudi nilianza kuchana nywele zangu, mara nikamwona Kalia anaingia chumbani mwangu hali akitabasamu. "Umefurahia nini?" nilimwuliza. "Yuko pale." "Nani?" "Yuko pale! Husikii!" "Lakini nani?" "Yule wako." Mara moja nilifahamu, maana Kalia ndiye tulikuwa tukimtumia kama posta yetu. "Anafanya nini?" nilimwuliza. "Anakungoja." "Amesema hivyo?" "Ndiyo, ameniambia kwamba ametangulia." "Ametangulia wapi?" "Amesema pale mahali penu pa kawaida." "Asante, Kalia, nitakwenda sasa hivi." "Amesema usikawie sana." "Haya." Kalia aliondoka chumbani anakimbia kuwaona wenzake ambao walikuwa wakimpigia miunzi waende mtoni kuoga. Nilipomaliza kuchana nywele nilifungua sanduku na kutoa kitambaa cha gauni. Nilikikunjia ndani ya karatasi na kuondoka kabla ya Mama kuniuliza mahali nilikokuwa nakwenda. Maswali ya Mama kuhusu kokote nilikokwenda yalikuwa yamekwisha niudhi. Mahali petu pa kawaida hapakuwa mbali sana. Lilikuwa ni shamba la mihogo mbali kidogo na nyumbani kwetu. Mwenye 38 shamba hili alikuwa mvivu kupalilia; kama angekuwa na nguvu za kupalilia mahali petu pangekuwa wazi. Lakini kwa mshangao nilikuta mihogo yenyewe imekwisha chimbwa na mahali petu palikuwa wazi kama uwanja wa mpira. Nilikuwa bado nikishangaa nilipoona, mbele kidogo karibu na shamba jingine la mihogo, msichana amesimama amenipa mgongo, kanga ilikuwa imeshuka kutoka kichwani kufunika mabega. Moyo wangu ulianza kudunda; naye aliposikia viatu vyangu alianza kung'oa vijani na kukata vijiti vilivyokuwa karibu. Nilipomkaribia nilimshika begani na kujaribu kumgeuza anitazama. "Niache," alisema huku akicheka. "Kwa nini?" "Unaponishika unaniumiza." "Mimi nakutazama tu." "Kwani hujaniona, au labda umenisahau " "Vumilia, habari ya siku nyingi?" "Hali yangu nzuri kama mti usioliwa na mchwa." "Mti usioliwa na mchwa una nini?" "Unafanya nyumba isianguke mapema," alisema. Halafu aligeuka kunitazama. "Kazimoto, mimi mzima kama shilingi ya masikini iliyosahaulika mfukoni." "Sielewi." "Hata barua hamna!" Nilikosa la kujibu. "Mama yako amefika? Tulikuwa naye kisimani." "Amefika." "Ndiye ameniambia kwamba alikuacha nyumbani wakati alipoondoka; na jana je, ulifika salama? Tulikuona na sanduku zito." "Kwa nini hukuja kunisaidia?" "Acha," alisema pole pole, "watu wanakuja." "Niache nini?" 39 "Ninasema acha; mimi hayakunileta hayo." "Acha mchezo," nilimwambia kwa ukali kidogo. "Mwenye baridi ndiye ajongeaye moto. Wewe ulipaswa kuja kabla yangu." "Nilikuwa nataka kumtuma Kalia. Uliniwahi kidogo tu." Alinitazama. "Vumilia, kweli tuondoke hapa, tumesimama njiani." "Tangulia," aliniambia. Nilitazama kila upande wa njia, halafu niliingia mihogoni hali nimeinama. Wakati huo nilikuwa nimesahau uanachuo. Nilipofika katikati ya shamba nilikaa. Nilianza kung'oa majani ili kutayarisha kitanda. Kwa muda wa dakika tano sikusikia kama Vumilia alikuwa anakuja. Baada ya muda nilimwona anakuja. "Kwa nini umekawia namna hii?" nilimwuliza. "Ulipotoka tu baba yako akapita. Anasema anatoka safari." "Ameniona?" "Hata!" "Mbona unakaa mbali namna hii? Huoni?" Nilimwonyesha majani yangu. "Mm!" aliguna na kupandisha mabega juu kama alama ya kukataa. "Umesema mwenyewe - mwenye baridi ndiye ajongeaye moto," nilisema. Niliinuka kwenda karibu naye. Nilianza kumpapasa kiunoni. Nilianza kumvua nguo. "Acha nivue mwenyewe!" alisema. "Upesi kabla majani yetu hayajakauka." Muda ulikuwa mfupi. Ilikuwa baada ya muda huu nilipotambua kwamba majani tulikuwa tumekwisha yaacha pembeni, na kwamba mti mmoja wa mhogo niliokuwa nimekanyaga ulikuwa umeng'oka. Nilianza kumkumuta mchanga kichwani. 40 "Kazimoto, unafahamu livu hii tunaagana!" "Bado sijafahamu sawa sawa." "Mpango wangu wa ndoa umekaribia kutekelezwa. Nafikiri baada ya miezi miwili!" "Bahati mbaya sana." "Kwa hiyo utakapokuwa unakuja kunichukua usiku fika kwa uangalifu, kwa sababu siku hizi Mama ananichunga sana. "Nitakuja kukuchukua Jumamosi," nilimwambia. "Jumamosi hapana." "Kwa nini?" "Sina nafasi siku hiyo; fika Jumapili." "Haya nitakuja. Nilikuwa na zawadi kidogo ya kukupa." Nilimpa kile kitambaa. Aliifungua upesi ile karatasi. Alikiona. Alitabasamu. "Asante sana," alisema. "Nafikiri kimekugharimu shilingi nyingi. "Thelathini na tano tu." "Thelathini ni pesa nyingi sana." Alikitia ndani ya kanga. "Nakwenda. Kwa heri," alisema. "Unapita wapi?" nilimwuliza. "Huku." "Mimi napita huku." Kila mtu alishika njia yake na kutopa upande mwingine wa shamba. Nilipofika nyumbani nilikuta kweli Baba amekaa "Tutayazungumza kesho," alisema. Baada ya kumsalimu nilikwenda nyumbani mwangu. Nilikuta Kalia amekwisha toka mtoni. Alikuwa akitumia shanuo langu. Nipoingia aliguna. "Kwa nini unaguna?" nilimwuliza. "Hata mimi naona tu," alisema. "Unaona nini?" "... kwamba yule msichana ulimwona." 41 "Umefahamuje?" "Tumekutana naye njiani anatoka huko huko ulikokuwa. Alikuwa amefurahi sana. Mara kwa mara huwa anatuuliza utakuja lini." Alinyamaza kwa muda. "Ngoja niweke wei halafu nikupe mambo yako," alisema. Alijaribu kuweka wei aliyokuwa anasema. Alipomaliza niliona kwamba wei aliyoweka ilikuwa imejipinda kama alama ya vema. Alichukua kitabu changu kimoja kilichokuwa mezani, na humo alitoa barua. "Hii barua yako. Nilikuwa nayo hata kabla hujaenda kumwona. Lakini alikuwa ameniambia nikupe baada ya kuonana." Niliifungua kwa haraka. Bila kutegemea, poda nyingi ilimwagika juu ya kitanda changu na kipande kidogo cha karatasi kilitoka. Kalia alitoka nje huku anacheka. Nilimsikia akiwaeleza wenziwe nje. "Kalia, nitakupiga!" nilimwambia. Lakini Kalia alicheka tu na kukimbilia nyumbani kwa Kabenga kula machungwa. Nilisikia Kabenga akimwambia Kalia angoje mpaka kesho, kwani ilikuwa haifai kula machungwa jioni. Kalia alikuwa kijana ambaye mara nyingi aliweza kuzungumza nami kama mwenzangu ingawa alikuwa na umri wa miaka kumi na mitano tu. Tulikuwa tumezoeana, naye alikuwa haniogopi tena. Mimi mwenyewe nilipenda kutembea naye; wasichana wangu wote aliwafahamu na matendo yangu nao aliyaona. Yeye pia alipenda sana kunifuata. Mara fulani nilikuwa namrudisha nyumbani hasa nilipokuwa na safari ya kwenda mbali. Alizoea kusikitika, kwa hiyo nikawa namtoroka. Kalia alimaliza darasa la saba tu. Aliposhindwa alianza kujishughulisha nyumbani na takataka; mwishowe akawa fundi wa kushona viatu na kunyoa. Kalia alipokimbia nilifungua kile kijikaratasi ili kusoma 42 ujumbe uliokuwamo. Niliona msitari mmoja tu: "Ninaomba tupendane." Giza lilikuwa limekwisha ingia na niliona Baba akikoka moto. Furaha yangu ilipungua nilipokumbuka yale mambo yalioyokuwa yakitokea nyumbani kwetu usiku. Niliona kwamba hata mimi hofu ilikuwa imekwisha anza kunitawala. Siku hiyo tulikula bila kusikia vishindo vyo vyote, hata mbwa hawakubweka. "Umekwisha zungumza na ndugu yako?" Baba aliuliza baada ya kula. "Bado," nilijibu. "Jibu lako nililifahamu. Kazimoto, mambo ya wasichana yamekuingilia vile kwamba watu wa nyumbani umewasahau." "Mambo ya wasichana sihusiani nayo." "Unasema nini? Mtoto gani wewe? Unataka kunidanganya mimi? Kazimoto, uwongo huu wote uliupata wapi? Unafikiri mimi sikukuona unanyatia mihogoni?" "Basi, basi Baba, nisamehe," nilisema upesi. "Ndiyo, Kazimoto, ukitaka kuwa rafiki yangu sema ukweli daima." "Ndiyo uliniona," nilisema. "Kwa kuwa hufahamu habari za hapa nyumbani, basi mimi nitakuambia. Kazimoto, tangu ufike hapa ndugu yako amekataa kula," Alipomaliza kusema maneno hayo aliinuka kwa hasira kwenda kulala na kuniacha mimi nikishangaa. Nami niliinuka kwenda jikoni alikokuwa amekaa Mama na Rukia. Nilipoingia jikoni nilimkuta Mama anakula; lakini niliona kwamba hakula chakula kingi maana ugali ulikuwa umenyofolewa mara tatu tu. Nilimwona Rukia amelala chini juu ya kanga, kichwa chake amekiweka juu ya miguu ya Mama. Mama alikuwa akimpangusa kwa kanga machozi yaliyokuwa 43 yakitiririka kila wakati. "Rukia," nilimwita pole pole. "Rukia," niliita tena. Hakuniitikia. Nilijaribu tena. "Rukia, jaribu kula chakula kidogo." Hakuniitikia. Badala yake alianza kulia kwa kelele. "Kazimoto," Mama alisema. "Kazimoto, tuache tupumzike, tuache tulie. Huu ni ugonjwa umeletwa na vijana na utatuma- liza sisi kina mama wenye mabinti. Ninajiona kwamba nitakwenda pamoja na binti yangu." Machozi yalimlengalenga. Niliona hapa hapa kuwa mahali pangu. Niliondoka pole pole nikawaacha wanalia wote pamoja huku wamekumbatiana. Kesho yake asubuhi Kalia ndiye aliyeniamsha. Nilipokuwa nikipiga mswaki niliwaona Kabenga na mkewe wakiongozana kuja nyumbani kwetu. Kwa kuwa kulikuwa na baridi bado wote walikuwa na shuka mabegani. Walipofika ndani ya nyumba ya Baba, niliwasikia wakiuliza habari ya Rukia. Mama aliwajibu kwamba mgonjwa aliomba uji asubuhi. Walifurahi na kusema kwamba maadam ameanza kunywa uji karibu atakula chakula cha kawaida. "Tunamwombea apone," walisema. Nilipomaliza kuvaa nilistukia kumwona Kalia anakuja chumbani mwangu. "Kazimoto, unaitwa na Baba." "Wapi?" "Ndani ya nyumba yake. Amesema harakisha." Nilikwenda. Nilipofika chumba cha mazungumzo nilikuta kiti kimoja kimebaki kwa ajili yangu. Kabenga na Baba walikuwa pia wamekalia viti. Tuza na mama yangu walikuwa wamekaa chini. "Kazimoto," Baba alianza kuzungumza, "tumekuita ili tujadiliane juu ya mambo ambayo hata wewe mwenyewe umekwisha yaona. Yalipotokea, mimi pamoja na Kabenga 44 tuliona hawa hawakuwa watu wengine isipokuwa wachawi. Nilifunga safari kwenda nchi za mbali kuwaona waganga. Huko waganga wameniambia wazi kwamba ni kina Masesa na watoto wake. Hawa ndio watu ambao huwa wanakuja hapa usiku. Na sababu yenyewe nimeambiwa kwamba ni mashamba. Unafahamu kwamba sisi tuliletwa hapa na serikali, ingawa kweli tumekaa kwa muda mrefu. Sasa Bwana Masesa anataka tuhame ili achukue tena mashamba yake." "Masesa anaishi wapi?" niliuliza. "Ni kaka yangu," Kabenga alijibu, "isipokuwa yeye anaishi katika kijiji kifuatacho cha Kigara." "Kwa hiyo mashamba haya ni yenu?" nilimwuliza Kabenga. "Ni yetu ndiyo, lakini mimi sina matata." "Sasa tufanyeje?" Baba aliuliza. "Hata mimi nimo hatarini," Kabenga alisema, "kwa hiyo mimi naona afadhali tupeleke mambo haya barazani." "Barazani kama kwamba tumekwisha waona!" Mama alisema. "Wachawi hatuwezi kuwaona," Tuza naye alijitokeza. "Mimi nitawashika," nilisema. "Wewe!" Baba alishangaa. "Ndiyo," nilijibu haraka. "Wachawi wajanja," Kabenga alisema. "Hata sasa inawezekana wapo hapa wanatusikiliza." Hapo ndipo nilipowaambia maneno niliyoambiwa na padri mmoja: "Kuwashika wachawi ni jambo rahisi sana," nilianza. "Jambo moja kuhusu wachawi ni kwamba wana pua kali sana kama wanyama. Wanafahamu sana harufu ya mwanadamu, kwa sababu mtu ambaye huota moto ana harufu ya pekee. Wachawi wakitaka kwenda kutembea usiku hawasogelei moto muda wa siku tatu nne; halafu wakitoka nje usiku 45 huvaa nguo ambazo huwa zimetunzwa nje majanini ili kupoteza harufu kwa umande. Wengine huenda uchi. Kwa hiyo watembeapo ni vigumu kuwaona. Ukitaka kuwaona fanya kama wao." "Labda kuna ukweli ndani yake," Kabenga alisema. "Jaribu," Baba alisema. "Leo," Mama alisema. "Mimi sidhani kwamba atafanikiwa," Tuza alisema. "Leo haiwezekani," nilijibu, "kwa sababu nguo zangu lazima zikae nje kwa muda wa siku kadhaa." Mkutano ulipokwisha, wote walikubali kwamba nijaribu. Kwa muda wa siku tatu sikukaa karibu na moto na mara nyingi mchana nikawa nakaa kivulini ili kupoteza harufu yote ya kibinadamu. Nguo za kaniki zilipelekwa majini. Mwishowe siku ambayo nilikuwa nimeahidi kuwavizia ilifika. Nilitengeneza kiti cha kamba juu ya mwembe ambao, chini yake, nilizoea kuona nyayo zao. Ilikuwa siri kubwa, hata wadogo zangu nyumbani hawakufahamu isipokuwa sisi watano. Siku hiyo Kabenga alikuja kulala kwetu ili kuona yatakayotokea. Siku hiyo nilikula chakula cha jioni kama saa kumi na mbili. Baada ya kula nilipanda mtini pamoja na upinde, mishale minne na mkuki. Usiku huo hawakuja. Nilifanya hivi kwa muda wa siku tatu, lakini sikufanikiwa. Kiini cha mambo haya kiliendelea kuwa fumbo kubwa. 46 3 Jumanne, niliondoka nyumbani asubuhi. Nilikuwa na nia ya kumtoroka Kalia. Rukia alikuwa bado hajaanza kula vizuri, lakini niliona lazima kwenda kumsalimu rafiki yangu na kumpa pole kwa maafa yaliyompata. Rafiki yangu, Kamata, alikuwa akiishi katika kijiji cha Saku. Kamata alikuwa mmoja kati ya rafiki zangu ambao nilizoea kuwate- mbelea mara nne au zaidi wakati wa likizo. Yeye alikuwa ameoa na alikuwa na watoto wawili. Alikuwa na mji wake peke yake, wenye nyumba mbili, ya kulala na jiko. Nilipokuwa nikisoma naye katika shule ya msingi, Kamata alikuwa amenitangulia mwaka mmoja, lakini alishindwa kuingia darasa la tisa. Aliposhindwa, hakufanya uhuni wafanyao watoto wengi washindwao darasa la saba siku hizi. Alitambua mara moja kwamba kazi ya ofisi haikuwa yake tena. Alikaa miaka miwili halafu akaoa. Mama yake alipofariki, 47 siku chache baada ya harusi, Kamata alishika mji na kuuchukua. Baba yake alikufa zamani, na Kamata hakupata kuona sura yake; alikuwa bado mtoto mchanga wakati huo. Kamata alikuwa mkulima stadi. Alikuwa na shamba kubwa la migomba; shamba la mpunga karibu na ziwa; kishamba kidogo cha kabichi na shamba kubwa la viazi. Alikuwa pia na mitego mitano ya samaki. Alikuwa kijana nadhifu sana. Wakati alipokuwa hafanyi kazi nguo zake zilikuwa safi daima. Baiskeli yake ilikuwa ikisafishwa karibu kila siku. Visu vyote nyumbani vilikuwa na makali daima. Ubaya wake ambao ulifanya vijana majirani wamchukie kidogo ni kwamba alikuwa haazimi kitu chake. Hata juu ya baiskeli yake alikuwa ameandika: "Utaazima Kesho". Huyu ndiye Kamata, rafiki yangu, ambaye nilikuwa nikienda kumtembelea. Asubuhi kabisa nilichukua baiskeli yangu juu juu ili isipige kelele na kumwamsha Kalia ambaye alikuwa bado usingizini. Nilipoitoa nje nilifunga mlango pole pole. Baba, Mama, Rukia, sikuwasabahi. Niliondoka bila kumwambia mtu ye yote mahali nilikokuwa nakwenda. Ulikuwa karibu umbali wa kilometa tano hivi kutoka Mahande kwenda Saku. Njiani nilikutana na watu wengi: wenye majembe; wenye watoto mgongoni na wengine waliokuwa na safari kama mimi. Niliendesha baiskeli yangu nikipanda vilima na kushuka. Ule utoto wa kupanda kila kilima ulikuwa umekwisha ondoka. Nilifika nyumbani kwa Kamata saa nne. Nilimkuta Matilda, mke wa Kamata, akichanja kuni kwa shoka. Mtoto mmoja alikuwa mgongoni, wa pili alikuwa amekaa chini ya kivuli cha mti, kiazi mkononi. Mji wote ulikuwa umefagiliwa vizuri. Matilda alitupa shoka chini aliponiona. "Karibu! Karibu!" alipiga kelele. "Starehe, Kamata hayupo?" 48 "Hayupo. Amekwenda kuondoa mitego yake majini." "Atarudi karibuni?" "Lazima atakuwa hapa kabla ya saa sita." "Ninakwenda ziwani kumngojea." "Kaa tu atakuja." "Ninakwenda kupunga hewa ziwani kidogo." "Kazimoto, hata wewe unafahamu Kamata alivyo. Asipokukuta nyumbani atakuja kunikaripia kwamba sikukukaribisha vizuri." Baada ya kuzungumza naye kwa muda aliniruhusu kwenda ziwani. Nilimwacha akiingiza baiskeli yangu ndani. Nilipofika ziwani nilikuta wavuvi watano wakishona matundu ya mitego yao. Walikuwa wakifanya kazi hii kwa haraka sana. Mikono yao ilikuwa myepesi sana. Walikuwa wakifanya kazi hii hali wakisimuliana hadithi na kucheka kwa sauti za ajabu. "Kamata anaweza kuwa wapi?" niliuliza. "Kamata?" mmoja aliniuliza tena. "Ndiyo," nilijibu. "Kuna uzima au msiba?" "Uzima." "Wewe nani?" "Kazimoto." "Kazimoto?" "Ndiyo." "Mtoto wa nani?" "Mafuru." "Kijiji gani?" "Mahande." "Hapo Mahande unatoka sehemu gani?" "Karibu na mto." "Kamata atarudi karibuni. Ameondoka zamani na 49 mtumbwi wake, Wewe mgeni wake, sivyo?" "Ndiyo." "Unaweza kukaa hapo mchangani umngoje." Nilikaa, nikawa nawatazama wanafanya kazi yao. Kijana mmoja ambaye nilifikiria mjinga kati yao ndiye alikuwa akisimulia hadithi. Alikuwa kijana mfupi mwenye ndevu. Meno yake yalikuwa nje daima utafikiri anacheka. Baada ya kijana huyu kusimulia hadithi yake ambayo ilichekesha sana watu, kila mmoja alianza kutoa hadithi yake; zote zilihusu wanawake. Walisema kwa lugha ya matusi vile kwamba nilianza kufikiri moyoni kama walikuwa wamekwisha sikia kitu fulani kiitwacho dhambi. Mmoja kati yao alijidai kwamba kwa wanawake tu alikuwa amebakiza makabila machache ya nchi hii. Alianza kutaja kila kabila akitoa kasoro zao. Hapo ndipo nilipoanza kufikiri moyoni kwa nini nilisoma mpaka Chuo Kikuu. Nilianza kujiuliza kwa nini nilisoma kile kitabu cha zamani - Biblia. Niliwaonea wivu wenzangu ambao tuliachana darasa la nne. Wao sasa walikuwa wakicheza zeze na kupiga vishindo kwa furaha. Niliona kwamba elimu ilikuwa sumu ya furaha yangu. Kila siku kusoma vitabu na magazeti nisiwe nyuma ya wakati. Sasa niliona tofauti kati ya maisha yangu na yao. Kwa wakati huu wazo la kuacha shule ili niishi kama wao lilinijia kichwani. Sikuona sababu ya kusumbuliwa na mawazo, kuwa na wajibu mkubwa zaidi, halafu kufa kama wao na labda kwenda motoni, wao mbinguni - faida gani? "Huyo Kamata anakuja," walisema wakitazama ziwani. Jinsi walivyoweza kuona mtumbwi sijui, maana mimi sikuweza kuuona. "Inaonekana kwamba leo hakupata samaki wengi," mmoja kati yao alisema. Alipofika karibu niliona mtumbwi wake ukipanda na 50 kushuka juu ya mawimbi. Alipofika karibu sana niliona kwamba hakuwa na shati kifuani. Mwishowe mtumbwi wake uligusa mchanga. Kamata alitoka na kusukuma mtumbwi wake. Alikuwa amekwisha niona. "Kazimoto! Nisamehe, sikujua! La sivyo nisingekawia sana huko majini." "Umefanikiwa?" wavuvi walimwuliza. "Siku hizi samaki wamekataa kufa," aliwajibu. Na kweli hakufanikiwa. Wale samaki wachache aliokuwa nao aliwafunga kwenye ncha mbili za mti. Yeye alisimama katikati na kuwabeba. Wengi walikuwa bado wazima na mikia yao ilikuwa ikipigapiga. "Twende nyumbani, Kazimoto," aliniambia. "Jamani mtanisamehe nimepata mgeni." "Lakini utakuja?" wavuvi walimwuliza. "Wapi?" "Kule. Umlete mgeni." Walipeana alama fulani ambazo sikuelewa. "Ndiyo nitakuja," aliwajibu. Tuliondoka kuelekea nyumbani. Tulipokuwa njiani Kamata aliniita "Kazimoto." "Naam." "Bila shaka ulikuwa umekwisha sikia mambo yaliyonipata." "Ndiyo, nilisikia bado nikiwa Dar es salaam. Kusema haki nimekuja leo kukupa pole kwa yote yaliyokupata. Nilifika Jumamosi; ingawa Rukia hana hali nzuri nimeona vizuri kuja kukusalimu mapema." "Nitakusimulia tukifika nyumbani," alisema. Tulipofika nyumbani, Matilda alituandalia chakula - ndizi mbichi ambazo zilikuwa zimepikwa vizuri sana, samaki wengi sana na viazi vichache. Matilda alikula peke yake jikoni pamoja na watoto. Baada ya kula Kamata alianza 51 hadithi yake. "Kazimoto, furahi kuniona sasa. Nilikuwa maiti, na ninafikiri kwamba sasa ungekuwa unalia karibu na kaburi langu. Nilikuwa mfu. Hadithi yenyewe ni hivi: Siku moja vijana wawili walinipitia hapa kwenda kunywa pombe. Vijana hao ni majirani. Tulipofika huko kwenye pombe tulikunywa sana. Kumbe wenzangu walikuwa na hila mbaya. Giza lilipoingia walianza kuwa wanajitilia pombe kidogo, mimi nikitiliwa pombe nyingi. Mwishowe nilijiona naanza kulewa. Niliwaomba ruhusa kuondoka, lakini wao walikataa. Waliahidi kunisindikiza mpaka nyumbani. Niliendelea kunywa. Karibu kama saa sita za usiku waliniambia kwamba walikuwa tayari kunisindikiza. Nilijaribu kusimama, nilijiona bado na nguvu za kuweza kutembea bila kushikiliwa. Tulipofika mbali kutoka mahali pa kunywea pombe, mmoja wao alisema: 'Kamata'." "Nilisimama. Mara niliona kila mmoja kati yao ameshika rungu. Hofu kubwa ilinishika na pombe yote iliruka. Niliona mwisho wa maisha yangu hapa duniani. "'Jamani! Kweli mniue! Mniue kabisa', nilijitetea." "'Ua kabla hajasema maneno mengi!' mmoja alisema. Hapo hapo nilipigwa rungu la mgongo. Nilianguka chini." "'Jamani kweli sasa mmeniua!'" "Mara moja nilisikia rungu linalia juu ya kichwa changu. Nilizimia. Kesho yake asubuhi nilipozindukana nilijiona nimelala ndani ya maji. Majani yalikuwa marefu hata sikuweza kuona mahali po pote. Akili ziliponirudia sawa sawa nilikaa kwa muda nikifikiri. Nilikumbuka hadithi kidogo. Niliona nguo zangu zimeenea damu. Nilipojishika kichwani nilishangaa kutupa vidole ndani ya shimo. Nilianza tena kuogopa. Nilijiona maiti tena. Nilijaribu kusimama. Maumivu yalikuwa mengi mno. Niliposimama niliona kwamba nilikuwa nimelala 52 karibu na ziwa. Nilisikia sauti za watu. Nilijivuta pole pole. Wale watu waliponiona walistuka, kama kwamba waliona mzuka fulani. Ndio wale vijana ambao ulikuwa nao ziwani. Nilipowakaribia walinitambua: "'Kamata! Umekuwaje?'" waliniuliza. "Nipelekeni nyumbani nikamwone mke wangu," niliwaambia. "'Waliponifikisha nyumbani, mke wangu alianza kulia badala ya kunitafutia maji na kunisafisha.' Wale vijana waliosha vidonda vyangu. Maumivu yalikuwa makali. Niliomba nipelekwe hospitali mara moja. Baada ya kuwaeleza kwa ufupi walinipeleka hospitali ya Bukonyo. Siku hiyo daktari alikuwa amelala. Nilishugulikiwa na mayaya. Baadaye tuliambiwa kwamba daktari alikuwa amelewa pombe ya moshi na alikuwa hawezi kuwaona wagonjwa. Kesho yake asubuhi daktari aliniona. Nilimweleza kisa chote. Polisi walipelekwa kuwashika wale vijana ili wawekwe rumande mpaka nitakapopona. Inasemekana kwamba mtu fulani aliwaona huko Uzinza Geita wakijiita majina mengine. Mimi nilikaa hospitali kwa muda wa mwezi mmoja. Tazama kichwa hiki!" Alinionyesha ngeo yake. "Kule mtoni ulifikaje?" nilimwuliza. "Mimi sikuwa na fahamu wakati huo. Lakini inaonekana kwamba waliponipiga sana na kudhani kwamba nimekufa waliniburura na kunitupa ziwani. Mungu bariki walinitupa maji mafu, na badala ya kuanguka kifudifudi nilianguka chali pua na mdomo juu ya maji. Umande wa usiku pamoja na maji chini ya mgongo yalinisaidia na kunifanya nizindukane asubuhi. "Unafahamu kwa nini walitaka kukuua?" nilimwuliza tena. Kamata alitazama upande wa jikoni. Matilda alikuwa naye akisikiliza. "Sababu yenyewe mpaka leo hii sijapata kuielewa vizuri," alisema. 53 "Lakini mimi ninafahamu wazi kwamba sijawatendea jambo lo lote baya," alimaliza. Tulinyamaza kwa muda. "Kazimoto, utaweza kukaa hapa nasi majuma mangapi?" aliuliza. "Ikiwezekana nitarudi leo saa kumi; hiyo ndiyo saa niliyokuwa nimepanga." "Labda unataka kunichekesha. Huwezi kuja kuzungumza nasi kwa muda mfupi namna hii. Lala mpaka kesho. Huu ni mji wako, Kazimoto." "Ndiyo - lakini kama nilivyokwambia hapo awali nilimwa- cha Rukia mgonjwa sana." "Bado hajajifungua?" Matilda aliuliza kwa sauti. "Bado." "Labda atazaa mapacha. Nilimwona majuma mawili yaliyopita. Tumbo lilikuwa kubwa." "Sijui wasichana wanafikiri nini,"Kamata alisema. "Ulikuwa umekazana kumsomesha lakini shukrani yake ni kutojiheshimu. Nafikiri amekusikitisha sana." "Sana," nilijibu. Kamata alitazama jua. Aliinuka. Alijinyosha halafu alipiga - mwayo mrefu. "Matilda sisi tunakwenda matembezi. Tutarudi usiku. Fahamu kwamba tuna mengi." "Kamata, huo ndio ubaya wako. Sasa unakwenda kumnywesha mgeni. Yeye atarudi amelewa wewe mzima. Usimpe mgeni mapombe mengi." "Kwani mimi nitakuwa namnywesha? Lete kibuyu. Nitakuletea hata wewe." Matilda alitafuta kibuyu upesi upesi. Alikileta baada ya kukiosha ndani. "Twende, Kazimoto." Tuliondoka. Tulipokuwa tumefika mbali na mji, Kamata aliniita, "Kazimoto." "Naam." 54 "Sikutaka kukueleza pale nyumbani kisa kilichofanya nipigwe." "Ebu nieleze." "Sababu yenyewe ni kwamba wale vijana walijaribu kumtongoza mke wangu. Alipowakataa waliona kwamba alikuwa akiwakataa kwa sababu mimi nilikuwa hai. Kwa hiyo walikata shauri kuniua. Lakini siku za mwanadamu kweli zimehesabika. Makumi yangu yaliyokuwa yamewekwa pembeni na Mungu kwa ajili yangu yalikuwa hayajatimia." Kamata aliponiambia hivyo niliamini, kwa sababu Matilda alikuwa mwanamke mzuri sana. Ingawa alikomea darasa la saba watu wengi wa maana - yaani wenye vyeo vya juu - walipeleka posa. Uzuri wake ulivuma Ukerewe nzima. Alipokata shauri kuolewa na Kamata kila mtu alishangaa. Wazazi wake walijaribu kupinga uchumba huu, lakini Matilda hakupenda kuolewa na mtu mwingine isipokuwa Kamata. Mwishowe wazazi wake walikubali, lakini moyoni kitu fulani kilikuwa bado kikiwachoma. Kwa kutaka kumkatisha tamaa Kamata walidai mahari makubwa sana. Kamata alikuwa tayari kulipa, kwani baba yake alipofariki alimwachia pesa nyingi kutokana na kazi ya uvuvi. Kamata alimwoa Matilda. Watu wengi walisema kwamba Matilda alivutwa na ule usafi wa Kamata. Kwa kuwa Kamata mwenyewe alipenda usafi alimtunza mkewe vizuri sana akawa anaonekana bado msichana hata baada ya kuzaa watoto wawili. "Hata mimi zamani nilikuwa na nia ya kuoa msichana mzuri sana, sasa ninaona kwamba ni hasara," nilisema. "Unasema uzuri wa sura?" aliniuliza. "Ndiyo." "Kwa nini usioe msichana mzuri?" "Wanaomtamani wanakuwa wengi mno. Kutoka maskini hadi tajiri." 55 "Labda usemayo ni kweli, Kazimoto; mke wangu amekwisha nipoanza mara nyingi mno. Na mara hizo zote nikiponea chupu chupu. Utaoa lini?" aliniuliza. "Sijapata bado msichana anayenipenda. Ye yote nimwendeaye ananirusha. Mwishowe nimekata tamaa." "Usikate tamaa," aliniambia. "Katika kutafuta mchumba usiogope kushindana. Hata kama alikurusha usikate tamaa. Mimi mwenyewe wakati nikitafuta mwanamke wa kuoa nilirushwa mara nyingi sana. Mwishowe nilianza kufikiri kwamba labda duniani hapa nilikuwa wa mwisho katika ubaya. Lakini hiyo yote ilikuwa kumbe haraka ya bure. Wangu alikuwa bado hajaja. Kwa hiyo, Kazimoto, wako yupo atakuja. Lakini hawezi kujileta kama wewe hujaribu." "Lakini mimi ninataka kuoa mapema iwezekanavyo; mwaka kesho kama ikiwezekana." "Haraka ya nini? Kijana kama wewe na elimu yako hiyo wanawake utawaona wengi baada ya masomo. Kwa sasa wewe soma tu. Sisi wakulima na wavuvi tunaoa mapema kwa sababu ndilo jambo la maana tu tunalofahamu katika maisha yetu na watu wengine. Lakini wewe elimu bado iko mbele yako. " "Hakuna huku msichana ye yote asomaye?" niliuliza. "Huku wanaosoma ni wachache. Wengi wanakomea darasa la saba. Kama unataka hao ni wengi." "Nikioa msichana wa darasa la saba lazima awe mzuri sana." "Kwa nini?" "Bila shaka umekwisha sikia kichekesho cha mwanamke aliyekwenda kwao kwa sababu bwana'ke alisema 'some coffee to day'." "Kazimoto, mke ni mke tu. Kwani wale waliosoma wameongeza nini katika hali yao ya uke? Utalipiga litalia 56 kama buyu." "Ingawa litalia kama kibuyu, lakini linafikiri na ninaweza kujadili nalo mambo ya juu yaliyoandikwa na wataalamu." "Kazimoto, acha mchezo. Mambo ya maana ya kuzungu- mza na mke wako ni yale yahusuyo aila. Na hayo hayakuandikwa." Nilisikia mlio wa ngoma na kelele za watu. "Kuna harusi?" niliuliza. "Hapana. Hizo ni ngoma ziitwazo Mbugutu; zinachezwa kwenye pombe, hasa pombe ya ndizi." "Ndiko tunakokwenda?" "Ndiyo, tumefika." Tulipofika wale wavuvi walikuwa wametungoja kwa hamu sana. Mara tu walipotuona walitukaribisha. Huo ndio ulikuwa mji wao. Ulikuwa mji mkubwa sana wenye nyumba kumi. Kama tukihesabu na majiko zilikuwa nyumba kumi na tano. Mji wote ulikuwa umezungukwa na shamba kubwa la migomba, na ulikuwa mji wenye mawe mengi katikati. Mawe haya ndiyo wanywaji walikuwa wamekalia. Wapiga ngoma walikuwa na mtungi wao mkubwa sana. Mimi na Kamata tulipelekwa katika kikundi cha wazee. Nafikiri kwamba hawa wazee walikuwa pia wamekaribishwa kama sisi. Kundi la vijana na wanunuzi lilikuwa mbali kidogo na wazee. Wengi kati ya vijana walikuwa wakicheza ngoma. Kulikuwa na vikundi vingine vidogo vidogo vimetapakaa huko na huko kati ya migomba. Wanawake fulani fulani walikuwa wamechanganyikana na wanaume. Wanawake watatu walikuwa wakicheza ngoma. Tulipokaa nilimwona yule kijana aliyekuwa akisimulia hadithi kule ziwani asubuhi, amebeba mtungi mkubwa kati ya mikono na miguu yake. Aliuweka katikati. Tulimshukuru. Baada ya kuuwekea mchanga pembeni ili usianguke aliuacha. 57 "Wazee," alisema, "na mgeni wetu ambaye ametujia leo. Karibuni. Wakerewe walisema kwamba asiye na kiuno naye huvua. Hiki ndicho nilichoweza kupata." Wote tulishukuru pamoja. Tulianza kunywa tukifuata duara. Pombe ilikuwa nzuri, nami niliinywa kwa pupa. Mazungumzo ya wazee yalianza. Kila mtu alikuwa kimya na walikuwa wakizungumza mmoja mmoja. Walizungumza juu ya watemi wa zamani; mwanzo wa makabila na matawi mbali mbali ya watu wa Ukerewe. Walizungumza juu ya vita vya zamani; juu ya watu mashuhuri; watu ambao waliweza kupanda mti hali mkono mmoja wameshika fahali; watu ambao waliwanyoa wenzao kwa chupa watake wasitake. Walizungumza juu ya mwanamke aliyesemekana kaanguka kutoka mbinguni na mkia akazaa watoto na baadaye akatoweka. Walizungumza juu ya mashindano ya ngoma kati ya Wakerewe na Wasukuma. Kwa vyo vyote, mambo mengi yalikuwa mazuri kusikiliza lakini mimi nilijiona niko nje ya mazungumzo hayo. Niliwauliza maswali kadhaa, lakini hayakujibiwa vizuri. Baada ya kuchoka na hadithi zao walinielemea mimi. Walianza kuniuliza maswali: "Unasoma wapi?" mzee mmoja aliniuliza. "Dar es salaam. " "Rafiki yako alikuwa akisema unasoma Makerere." "Ndiyo," Kamata alidakia, "nilikuwa nikiwaeleza kwamba unasoma katika shule kama ile ya Makerere." "Kumbe wewe umesoma sana," yule mzee aliniambia. "Sijui kama utaweza kunieleza jambo hili: Uhuru tumekwisha upata. Zamani mkoloni alikuwa akitengeneza pesa kidogo kwa sababu alikuwa hataki tuendelee na alikuwa akituonea katika mambo mengi. Hii haikuwa nchi yao. Yote haya tumeambiwa na wanasiasa. Sasa uhuru tumepata. Kwa nini 58 Serikali haiwezi kutengeneza pesa nyingi sana kila mtu awe tajiri?" Lilikuwa swali gumu la uchumi kueleza hasa kati ya wazee kama hawa. Uchumi nilikuwa sijui lakini ili kutunza heshima yangu ya elimu nilijitahidi kuwaeleza lakini hata hivyo walikuwa bado wakinitazama tu wakitegemea kuelezwa zaidi. Niliona kwamba walikuwa hawaelewi. Mzee yule aliendelea kuniuliza, "Lakini wewe huoni dhahiri kwamba wakuu wa Serikali ndio wanaozitengeneza. Wao wanazo sisi hatuna; na hawafanyi kazi kutuzidi." Nilijaribu kueleza. Hata hivyo hawakutosheka na jibu langu. Mzee mwingine aliuliza, "Swali la pesa tuliweke pembeni. Mimi nitafurahi sana kama utaweza kunieleza kwa nini mwezi unapoonekana ni mdogo na unapotua unakuwa mkubwa na mwekundu." Hapo nilipashwa kukiri kwamba nilikuwa sijui. Niliwaambia kwamba nilikuwa sijifunzi somo hilo na kwamba somo hilo liliitwa Jiografia. Niliposema hivyo tu wazee hawakuwa na shauku tena ya kuniuliza maswali. Hawakuona tofauti kubwa kati yangu na wao. Mambo yaliharibika nilipoanza kuwaambia kwamba huenda hakuna Mungu. Wazee wote walikataa kabisa. Mzee mmoja aliinuka kwenda nyumbani. "Mnazungumza na mwehu!" alisema kwa kelele. "A! Anasema kwamba hakuna Mungu! Yeye nani! Labda yeye ndiye anataka awe Mungu. Hakuna Mungu! Mtoto wa nani? Mababu na mababu wamekwenda; wamechukuliwa na nani? Nafikiri mnafunzwa kusoma kumbe mnafunzwa kuvuta bangi!" Alipomaliza kusema maneno haya alikwenda nyumbani akitupa mikono juu kwa kutokubaliana na usemi wangu: "Hakuna Mungu! Mwehu! Mwehu!" Nilisikia yule kijana aliyeleta pombe akimnong'oneza Kamata: "Mgeni wako ameanza kupatwa na pombe. Lakini 59 mwambie azungumze juu ya mambo mengine au aache kabisa la sivyo ataharibu kikao." "Tunaweza kuhama," Kamata alimwambia. "Ndiyo. Mnaweza kwenda nyuma ya nyumba yangu. Nitawaletea pombe yenu huko." Kamata aliponiambia kuhama sikupinga, nilikuwa nimesikia maneno yote. Tulipofika nyuma ya nyumba hiyo, kijana alituletea mtungi mdogo wa pombe. Kamata alikaribisha vijana wawili zaidi waje wanywe pamoja nasi, lakini yule kijana alikataa na kuwafukuza. "Kama pombe ikiwashinda chimbeni shimo mumwage humo," alisema. Tulianza kunywa peke yetu. Kwa kuwa kila mmoja kati yetu aliogopa kulewa sana tulikunywa pole pole. "Unamwona yule mwanamke aliyevaa kitambaa kichwani," Kamata aliniambia. Kabla sijajibu aliinuka na kwenda kuzungumza naye. "Kila kitu tayari," Kamata alisema aliporudi, "isipokuwa angependa kuzungumza nawe kwa muda mfupi." "Yaani niende pale alipo kama wewe?" "Hapana atakuja hapa mwenyewe." Baada ya muda mfupi yule mwanamke kweli alikuja. "Kaka, habari?" alisema. "Nzuri," nilimjibu. "Unakaribishwa." "Asante." "Kazimoto," Kamata alisema, "ninakwenda kucheza ngoma kidogo, nikute mambo yenu yamekwisha malizika." Aliondoka. Nilianza kufikiri namna ya kumwanza huyu mwanamke ambaye nilikuwa sijapata kukutana naye. "Karibu pombe." "Asante," alijibu. Nilimtilia pombe nyingi. Alikunywa kidogo halafu akanirudishia. "Nafikiri rafiki yangu amekwisha kueleza kila 60 kitu, sivyo?" Aliinamisha kichwa chini. "Bado," alisema. "Unataka nirudie tena maneno yale yale." "Rudia." "Ninakuhitaji wewe." "Unanihitaji mimi?" "Ndiyo." "Mm!" aliguna. "Sasa unasemaje?" "Unanihitaji mimi vipi?" aliuliza. "Mwanamke anahitajika kwa kitu gani?" "Kwa ndoa; wengine kwa siku moja." "Tuseme kwa siku mbili." "Haiwezekani." "Kwa nini?" "Sina nafasi." "Sasa tukatishe mambo. Leo usiku au vipi?" Alinyamaza kwa muda. Alinitazama. "Wewe nani?" "Nitakwambia tukionana." "Unasoma au unafanya kazi?" "Ninasoma." "Kumbe mtoto mdogo. Unasoma wapi?" "Dar es salaam. Bado hujajibu swali langu." Aliinama. Halafu sauti ndogo ilitoka. "Haya." "Sikusikia," nilisema kwa sauti. "Haya," alirudia tena kwa sauti hali ameinama. "Kunywa pombe." Alikunywa kidogo. Halafu aliinuka kuondoka. "Unaondoka!" "Ninakwenda kucheza. Nitamwambia Kamata zaidi." "Asante." 61 Nilimwona akizungumza na Kamata. Baada ya mazungumzo yao alikuja kunywa pombe. Yule mwanamke aliendelea kucheza. Tulikunywa mpaka tulipoona kwamba tulikuwa tumekwisha lewa. Kwa vyo vyote tulikuwa hatuwezi kuumaliza ule mtungi. Tuliwaita wale vijana waliotukaribisha. Tuliwashukuru na kuwaomba ruhusa ya kuondoka. Walitwa- mbia twende na pombe yetu. Pombe iliyotushinda tuliiweka ndani ya kibuyu. Wale vijana walitusindikiza kidogo halafu walirudi. Tulipokuwa njiani peke yetu Kamata aliniambia, "Yule mwanamke amesema atakuja nyumbani peke yake. Yeye akisema huwa hadanganyi. Huo ndio uzuri wake." "Labda wazazi wake wakali. " "Wapi! Ni wajinga. Binti yao huwa anawatukana wanapomzoza." "Kwa nini?" "Kwa sababu yeye ndiye huwa anawalisha na kuwavika kwa pesa apatazo kutoka kwa mabwana mbali mbali." "Kwa nini hawawezi kumwoza?" "Hajapata wachumba. Nani ataoa makapi. Huyo sasa amekuwa mpira, wa kudunda na kuacha hapo, wengine pia wadunde." Tulipofika nyumbani Matilda aliamka mara moja kuja kutupokea. Alituletea chakula. Ajabu kwangu ilikuwa kuona wingi wa samaki unapita ugali. Wakati wa kula, Kamata alinihimiza kumeza samaki tu niache kula ugali. Baada ya kula tulianza kunywa pamoja na Matilda. Pombe hiyo ndiyo ilinifanya nilewe kuzidi kiasi changu. Tulipokuwa tunakunywa tulisikia hodi mlangoni. "Karibu," Kamata alisema. Yule mwanamke aliingia. Alikuwa amevaa nguo zingine, na alikuwa akinukia marashi. Alikaa. Tulikunywa pamoja naye. 62 "Jina lako nani?" nilimwuliza. "Nyabuso," alijibu. "Na wewe jina lako nani?" "Mimi Kazimoto bin Machozi ya Simba." Alicheka kidogo. Tuliendelea kwa muda. Kamata alipotambua kwamba usingizi ulikuwa umenipata aliniomba nifuatane naye ili anionyeshe kitanda changu. Tulikwenda kulala. Kesho yake asubuhi Matilda ndiye aliyeniamsha. "Kazimoto, saa nne sasa, amka!" "Saa nne!" nilishangaa. Nilipotazama saa yangu niliona kwamba ilikuwa saa nne na nusu. Nilitafuta suruali yangu ili nivae, lakini sikuiona. "Suruali yangu niliacha wapi?" niliuliza. Nilipouliza hivyo tu Matilda alicheka sana. Nilimsikia Kamata pia akicheka. Nilihisi kwamba jambo la ajabu lazima liwe limetokea. Kama si la ajabu basi lilikuwa jambo la kuchekesha. "Lakini suruali yangu niliacha wapi? Sidhani kwamba nililewa vile kwamba nilianza kutembea uchi!" "Kazimoto," Kamata alisema, "nitakueleza baadaye. Kwa sasa nitakuazima suruali yangu moja." "Maji ya kuoga nimekuwekea tayari uani," Matilda aliniambia. Nilikwenda kuoga. Baada ya kuoga nilijiona afadhali kidogo. Nilivaa suruali ya Kamata. Suruali ya mwingine ni ya mwingine. Niliona kwamba upepo ulikuwa ukiingia mwingi sana. Kamata alikuja chumbani kunieleza. "Kazimoto," alisema hali akicheka, "suruali yako imechukuliwa na Nyabuso." "Kwa nini?" niliuliza. "Anasema wewe si mwanamume." "Mimi! " "Ndiyo, wewe. Hukuweza kufanya jambo lo lote." "Sema kweli!" 63 "Amechukua suruali yako kama adhabu." "Adhabu!" "Ndiyo. Ulimpotezea muda wake na ulimsumbua bure." "... Sumbua bure?" "Ndiyo. Bila shaka unafahamu ninataka kusema nini." "Sasa nitafanya nini?" "Utafanya nini? Sahau tu suruali yako." "Suruali yangu ninaweza kuisahau. Lakini..." "Lakini nini?" "Sifa yangu imeharibika. Yule mwanamke atatangaza." "Unataka kurudisha jina lako?" "Kama ikiwezekana." Aliinuka. Alinipiga begani. "Kazimoto, jina la bure lakini moto hauwaki. Nitamleta tena leo. Usiniaibishe tena." "Leo sitakunywa pombe. Unafahamu usiku nilipofika kitandani nilikufa." "Haya tutaona leo. Usife tena kwa usingizi." Baada ya chakula cha mchana Kamata aliondoka nyumbani. Aliniambia nimngoje nyumbani kwa muda mfupi." "Unakwenda wapi?" nilimwuliza. "Hapa karibu. Nitarudi sasa hivi." Alipoondoka nilikwenda kupiga usingizi kidogo. Kwa kuwa nilikuwa bado nimechoka usingizi ulinipata mara tu nilipoweka mbavu zangu juu ya godoro. Matilda aliniamsha saa kumi na moja. Aliniambia kwamba nilikuwa naitwa katika chumba cha maongezi. Niliinuka. Nilipofika chumba cha maongezi nilimwona Kamata na vijana wawili kati ya wale watano wamekaa kimya wakiningoja. Mtungi mkubwa wa pombe ulikuwa mbele yao. Nilikaa. Baada ya kusalimiana na wale vijana Kamata alisema, "Kazimoto, jana tulikuwa tumekaribishwa na hawa vijana. Mimi nilikuwa bado sijakufanyia jambo lo lote. Kwa hiyo leo nami nimejaribu 64 kupata kitu kidogo kama hiki ambacho tutakifurahia pamoja na vijana hawa." Wote tulishukuru. Tulianza kunywa. Lakini mimi nilikuwa mjanja. Mara nyingi niliweka mdomo tu. Muda mrefu haukupita mara Kamata akatambua. Alinishurutisha kumaliza kiasi alichonitilia. Wakati huu mazungumzo kuhusu vijana wa siku hizi yalianzishwa na wale vijana. Mwanzoni mazungumzo yalikuwa kati yao wawili tu. "Nasikia binti Kasembe ana mimba ya miezi saba," mmoja kati yao alisema. "Mama yake anasema mitano." "Mimi nimesikia saba na ametiwa mimba hiyo na kijana fulani mchafu mchafu. Sijui wasichana hawana macho?" "Msichana alikuwa darasa la kumi na mbili na ametiwa mimba na kilevi kama sisi." "Wazazi wa msichana huyu wamekataa kumkubalia kijana huyo kumwoa binti yao." "Kwa nini?" niliwauliza. "Wanasema hastahili," mmoja kati yao alisema. "Mnafikiri nini kisa cha uovu huu wote?" niliwauliza. "Uovu gani?" Kamata aliniuliza. "Huu uovu wa watoto kuanza mchezo mbaya wangali watoto wadogo." "Kazimoto," Kamata alisema, "mimi nafikiri maovu haya yote yameletwa na watu wa nje. Kwanza Waarabu. Hao ndio wameharibu nchi za pwani. Halafu Wazungu hawa, Waingereza. Mjerumani nasikia hakukaa muda mrefu sana. Lakini Mwingereza ameleta sinema, magazeti na mambo mengine mengi ambayo hukimbiliwa na vijana wa siku hizi." "Hayo yote ni bure," kijana mmoja alisema, "sababu hasa ni kwamba ulimwengu umegeuka. Zamani mvulana alipata umri wa miaka kumi na tisa au ishirini kabla ya kujiona mtu 65 mzima. Siku hizi mvulana mwenye umri wa miaka kumi na minne amekwisha anza kununua wembe dukani. Wasichana hao ndio wamezidi. Miaka kumi tu, utafikiri maziwa ya mwanamke mzima. Ulimwengu huu umegeuka." "Haya yote ni sawa," Matilda alisema, "lakini nionavyo mimi sababu yenyewe hasa ni kwamba malezi ya watoto siku hizi yamelegea sana. Wakati mimi nilipokuwa kama wao ilikuwa mwiko kukutwa na kaka nimesimama na mvulana ye yote; siku hizi kaka anaweza kumletea ndugu yake barua kutoka kwa mvulana mwenziwe. Maana yake nini? Wengine wanaweza kushikana viunoni dansini - kaka na dada!" Kijana mwingine alitoa wazo lake pia. Yeye alisema kwamba sababu kubwa ilikuwa kwamba vijana wa siku hizi wanadharau wazazi wao. Dharau hii imeletwa na elimu. Wanafikiri kwamba mawazo yote ya wazee ni ya kijadi. Mazungumzo yaliendelea kwa muda mrefu, kila mtu ameshikilia wazo lake. Mimi mwenyewe ingawa niliuliza swali hili, nilikuwa sijapata kulifikiria kwa makini. Nilikaa kimya. Tuliendelea kunywa mpaka saa mbili usiku Matilda alipoivisha chakula. Baada ya kula tuliuzunguka ule mtungi. Saa tatu Matilda alikwenda kulala. Alituacha sisi tunaendelea. Saa tatu na nusu Kamata alikwenda kufungua mlango wa nyuma. Alikawia sana kurudi. Tulifikiri kwamba alikuwa amekwenda kujisaidia. Aliporudi alininong'oneza sikioni: "Yumo tayari chumbani mwako." "Tunafahamu sana," kijana mmoja alisema. "Kwa nini msimwambie aje kunywa tu pombe pamoja nasi," kijana mwingine aliongezea. Sisi hatukutaka kusema zaidi juu ya jambo hilo. Kwa kuwa wote tulikuwa tumekwisha patwa na pombe tulianza kuimba. Kamata ndiye alianzisha: 66 Kula tunakula lakini wafuasi wangu, Tunakwenda tunalia kama bibi arusi, Kule gizani kwenye mlango usiofunguka, Kwa yule amezaye bila kutafuna, Kuzimuni wote tutakwenda. Wote tuliitikia kwa kurudia maneno hayo hayo. Wimbo huu hata mimi niliufahamu kichwani kwa sababu ulikuwa wimbo wa mshairi mashuhuri kisiwani ambaye nyimbo zake zilikuwa zikiimbwa hata na watoto wadogo. Pombe ilikwisha saa tano usiku. Tulipeana kwa heri ya kuonana kesho yake asubuhi. "Wazee wetu walisema kwamba usiku wageni hawasindikizwi," Kamata aliwaambia wale vijana. Waliondoka kwenda kwao wakiyumbayumba. "Kila mtu amekwisha ingia ndani ya nyumba?" Kamata aliuliza baada ya muda mfupi "Ndiyo," nilimjibu. Alifunga mlango wa nyumba. Nilipoingia chumbani mwangu taa ilikuwa bado ikiwaka. Yule mwanamke alikuwa amekwisha lala. Pembeni niliona suruali yangu imewekwa juu ya kiti kama kikombe cha mashindano. Ilikuwa imefuliwa na kunyooshwa vizuri sana. Nilikaa kitandani. Yule mwanamke aliamka. Aliponiona alipiga mwayo mrefu. "Usingizi ulikuwa umenipata," alisema. "Umechoka sana leo nini?" nilimwuliza. "Shauri ya pombe," alijibu. Alianza kunipapasa mgongoni. "Nilisikia watu wakiimba," alisema. "Tulikuwa sisi." "Nilikuwa nawasikia kwa mbali." "Kwa nini hukuja kunywa pombe?" "Sikutaka wale vijana wanione, ni waongo sana." 67 "Mbona wamekuona?" "Basi kesho utasikia maneno. Leo pia umelewa sana?" aliniuliza. "Leo ni mzima kabisa." "Jana ulifanya nini? Ulinisumbua bure. Sikuweza kupata usingizi." "Utanisamehe. Tuone leo mambo yatakwendaje." Baada ya kuvua nguo zangu nilijitupa kitandani tukawa tunatazamana uso kwa uso. Tulicheka. "Wewe kijana mpole sana. Kijana mpole namna hii kwa nini hutafuti mwanamke mzuri ukaoa kuliko kusumbuka na mikweche kama sisi?" "Kwani wewe mkweche?" nilimwuliza. "Unanionaje?" "Nakuona bado u msichana. "Nina watoto wanaolingana na wewe." "Ninafahamu kwamba una watoto wawili wadogo." "Kamata ndiye amekwambia?" "Watu wengine. Ninataka nami unizalie watoto wangu." "Nani atawatunza?" "Wewe na mimi," nilisema. Tulitazamana machoni. Tulinyamaza na kuzima taa. Kesho yake asubuhi yule mwanamke aliniamsha saa kumi na moja. Tulizungumza kwa muda wa robo saa. Aliniomba anwani. Niliwasha taa na kumwandikia. Yeye pia alinipa yake. Saa kumi na moja na nusu aliniomba nimsindikize ili afike nyumbani kwao kabla ya wazazi wake kuamka. Tukiwa njiani kwenda kwao aliniomba nisimsahau kwa barua. Aliniomba nirudi tena kumtembelea Kamata kabla ya kwenda shule. Mimi nilimwahidi kwamba sitamsahau kamwe. Nilimwambia kwamba nikipata nafasi nitarudi tena. Nilimsindikiza 68 mpaka nyumbani. Alipoingia ndani ya nyumba nilirudi peke yangu. Nilifika nyumbani kwa Kamata saa moja na nusu baada ya kutangatanga. Sababu yenyewe ilikuwa kwamba nilipotea njia. Nilipofika nyumbani nilikuta maji ya kuoga yenye moto tayari uani. Baada ya kuoga nilimwambia Kamata na Matilda kwamba nilitarajia kuondoka siku hiyo saa kumi. Wote walisikitika sana. Waliniomba nikae nao juma moja. Niliwaeleza hali ya nyumbani. Mwishowe waliniruhusu niondoke lakini kwa huzuni. Mazungumzo yetu siku hiyo yalikuwa juu ya yule mwanamke - Nyabuso. Waliniambia kwamba huyo Nyabuso aliweza kunifuata hata Dar es salaam kama akipata nauli. Walinieleza kwamba alikuwa mwanamke ambaye alikuwa akichukiwa sana na wanawake kijijini. Yeye aliweza kumfuata mume nyumbani na kumwita "bwana'ngu" mbele ya mke wake halali. Aliweza kumzomea mwanamke ye yote ambaye alikuwa akifahamiana na bwana'ke. Walinieleza kwamba walimu wa shule moja ya msingi ndio walikuwa mawindo yake. Walinieleza pia kwamba Mkuu wa Wilaya alikuwa naye amejijenga hapo. Mazungumzo yaliendelea mpaka saa sita. Ingawa yalikuwa mazuri, hayakuwa ya kusisimua sana. Kamata na Matilda walikuwa bado na huzuni kwa sababu ya kuondoka kwangu siku hiyo. Baada ya chakula cha mchana, Kamata alichukua mundu wake. Aliniomba nimngoje kwa muda mfupi. Aliingia ndani ya shamba lake la migomba. Baada ya muda mfupi alirudi na mikungu miwili ya ndizi. Alikwenda tena. Alirudi na mikungu mingine miwili. Saa zangu za kuondoka zilipokaribia alifunga mikungu hii juu ya baiskeli yangu. Aliifunga kwenye ncha za mti mikungu miwili upande mmoja, miwili upande mwingine. Saa kumi kamili niliondoka. Niliwaambia kwamba muda ulikuwa hauniruhusu kukaa zaidi. Niliwaambia wawape 69 salamu zangu wale vijana na wawaambie kwamba sikuweza kufika kwao kuwaaga kwa sababu ya haraka. Kamata alifunga nyumba. Alichukua baiskeli yangu kunisindikiza. Mbwa wake alikuwa mbele kabisa akiongoza njia. Naye alikuwa akikojoa katika kila njia panda. Kamata na baiskeli alifuata. Mimi nilikuwa nyuma yake nikifuatwa nyuma na Matilda na watoto. Walinisindikiza mpaka barabarani, kilometa moja hivi kutoka nyumbani. "Nafikiri sasa utaweza kupanda mpaka nyumbani bila kushuka," Kamata alisema. "Hakuna mipando mingi. Tutakuacha ujiharakishe mwenyewe." "Asante kwa kunisindikiza," niliwambia. "Utarudi lini kututembelea?" Matilda alisema. "Sidhani kama nitapata nafasi tena. Nina kazi nyingi sana nyumbani." "Fika tena siku ingine," Matilda alisema kwa sauti yenye masikitiko. "Haya, nitajaribu, lakini siwezi kusema kwa uhakika." Kamata alinipa baiskeli yangu. Tuliagana tena. Nilipanda na kukanyaga baiskeli yangu. Niliondoka. Nilipotazama nyuma niliwaona bado wamesimama wakinitazama. Baadaye nilipotazama nyuma tena sikuweza kuwaona. Nilikuwa nimekwisha kata kona ya barabara. Mimi mwenyewe nilianza sasa kusikitika. Niliwakumbuka kina Kamata, Matilda, wale vijana na yule mwanamke. Nilijaribu kukumbuka jina lake. "Nyabuso," nilisema moyoni. Nikiwa juu ya baiskeli nilijiona katika hali ya upweke. Mawazo mengi yalinijia kichwani. Mara niliona baiskeli yangu inaongeza mwendo: nilikuwa nimefikia mteremko mkali. Nilijaribu kufunga breki baada ya kuona kundi la ng'ombe mbele yangu barabarani kabisa. Nilifunga breki 70 kwa nguvu. Nilisikia kitu fulani kama mlio wa chuma. Badala ya kupunguza mwendo, baiskeli ilianza kwenda kasi sana. Nilitambua mara moja kwamba sikuwa tena na breki za nyuma. Niliogopa kutumia za mbele. Kutahamaki niliona ng'ombe mmoja hatua kumi hivi mbele yangu. Nilimgonga ubavuni. Nilisikia ng'ombe analia. Baiskeli ilianguka mbali na mimi nilipita juu ya mgongo wa ng'ombe na kuanguka upande mwingine. Kidogo ng'ombe yule anikanyage tumboni aliporuka kuwakimbilia wenzake. Nilisikia watoto waliokuwa wakichunga wale ng'ombe wakinicheka na kunizomea: "Hilo! Lina bahati! Kama lingeanguka juu ya pembe, leo lingeona cha mtema kuni!" "Tazama mandizi yake!" walisema. Niliinuka. Niliona damu kidogo juu ya goti. Nilipotembea sikusikia maumivu yo yote. Baiskeli yangu haikuharibika. Usukani tu ndio ulikuwa ukitazama pembeni. Niliunyosha tena. Ndizi zangu kweli ziliharibika sana, lakini kati yake mikungu miwili ilikuwa mizuri bado. Ile iliyoharibika niliifunga vizuri juu ya karia, miwili mingine niliiacha ikining'inia pembeni. Nilipotazama baiskeli vizuri niliona kwamba mnyororo ulikuwa umetoka. Niliuweka tena. Nilipanda. Niliona inakwenda sawasawa. Kwa kuwa haikuwa na breki nilishuka katika kila mteremko. Kwa sababu hii nilifika nyumbani usiku kabisa kila mtu amekwisha lala. Mbwa wa nyumbani kwetu waliponiona walibweka, lakini waliponita- mbua walikuja kunilaki na kupigapiga mikia yao juu ya miguu yangu. 71 4 Ile mibweko ya mbwa mwanzoni ilimwamsha Mama. Nilipofika chumbani mwangu nilikaa kwanza kwa muda juu ya kitanda nikifikiria mambo niliyoyaona kwa siku mbili zilizopita. Lakini mara nilisikia mlango unagongwa. "Ingia!" nilisema kwa sauti. Mama aliingia mikono nyuma kama mtu aendaye kilioni. "Ulikuwa wapi?" aliuliza kwa upole. Mimi nilinyamaza kwa sababu mara nyingi nilikuwa nimemwambia asiniulize swali kama hilo. "Kazimoto, ulikuwa wapi kwa muda wa siku mbili zilizopita? Uliondoka bila kutuarifu na kurudi kwenyewe unarudi usiku wa manane. Umezaliwa, Kazimoto, na kuna watu wanaokujali." "Unataka nini?" nilimwambia. "Kazimoto, fahamu kwamba mimi ninakupenda sana, 72 huwezi kuondoka bila kunipasha habari. Ungeuawa je - tungemshuku nani?" "Mapenzi ya kitoto namna hiyo mimi siyapendi. Kila siku niondokapo nyumbani unaniuliza 'Unakwenda wapi?'. Mimi nimekwisha kuwa mtu mzima sasa, na sitaki wewe uwe unafahamu njia zangu zote. Hata kama nikiwa nakwenda kwa wanawake unataka nikueleze?" "Kazimoto, mtoto wangu, ulimwengu wa sasa hauna rafiki. Mambo yanayotokea hapa yaonyesha kwamba lazima ujiangalie. Jana usiku mambo haya yametokea tena. Kwa hiyo jihadhari." "Mimi siioni hatari yo yote." Alinitazama. Mara moja aliona vumbi kidogo juu ya nguo zangu. "Umeanguka nini?" "Ndiyo, lakini sikuumia." "Huwezi kutambua sasa, maumivu utayasikia kesho. Lakini bila shaka umeumia. Nikuchemshie maji?" "Hapana, sikuumia. " Aliondoka. Nilifunga mlango. Mara baada ya muda mfupi mlango uligongwa tena. Nilifungua tena. "Kazimoto, usifunge mlango, ninakutayarishia chakula." "Usihangaike namna hiyo. Nitakula kesho." "Hapana, huwezi kulala na njaa." Alikwenda jikoni. Baada ya muda mfupi chakula kililetwa. Nilishangaa kumwona mama analia machozi. "Kazimoto, ninasikitika mboga haitoshi." "Inatosha sana," nilimwambia. Baada ya kuweka chakula mbele yangu, nilianza kula. Yeye alisimama pembeni kidogo. Aliponiona nakula alitabasamu kidogo. "Utakapomaliza kula weka vitu pembeni. Nitavichukua 73 kesho asubuhi." Alitoka nje. Ingawa alitoka amefurahi kidogo nilianza kumhurumia. Nilianza kujilaumu kwamba nilikuwa mkali kwake bila sababu. Lakini baadaye niliona kwamba nilifanya vizuri kumwambia, kwani nilikuwa sitaki mapenzi ya namna hiyo yaendelee. Kesho yake asubuhi, yaani Ijumaa, Mama ndiye alikuwa wa kwanza kuja chumbani mwangu kuchukua vyombo. Kwa kuwa sasa nilikuwa nasikia maumivu kwenye goti na bega nilimwambia Mama atafute njia ya kuweza kunikanda. Kwa haraka alitafuta yale majani yatumikayo katika kazi hii. Baada ya muda mfupi niliitwa jikoni. Majani yalikuwa yamelazwa juu ya makaa ya moto. Alianza kunikanda mguu, halafu bega. Wakati akinikanda nilimwuliza habari kuhusu Rukia. Aliniambia hali yake haikuwa mbaya sana. Alikuwa amekwisha anza kula kidogo. "Lakini kwa nini Rukia amesikitishwa sana na mimba? Wasichana wengine wanapata mimba, lakini wanacheka na kufurahi kama kawaida." "Aibu, Kazimoto, aibu ndiyo inamsumbua. Rukia ni msichana mwenye haya sana. Hataki kuonana na watu. Na anaona aibu hasa mbele yako." "Lakini kweli hakuna sababu ingine?" "Ninakumbuka siku moja nilipokuwa namtuliza aliniambia, 'Mama hufahamu masikitiko yangu. Nilitegemea sana kukusaidia lakini sasa siwezi: maisha yangu yameharibika.'" Baada ya kunikanda nilimwambia achukue zile ndizi chumbani mwangu, ili akampikie Rukia badala ya ugali. Mama alifurahi sana. Saa tatu, Baba na Kabenga waliingia chumbani mwangu. Hawakukaa. Baba alichungulia tu, aliponiona aliniambia niende nyumbani kwake. Nilipokwenda niliwakuta Kabenga na Baba wananingoja. Nilipokaa Baba alianza: "Kazimoto, 74 tuna maneno machache ya kukwambia. Kabenga, ebu mweleze mtoto huyu." "Ndiyo, Kazimoto," Kabenga alianza, "unafahamu sasa umekuwa mtu mzima. Huwezi kurudi kutoka safari ukafika kukaa ndani ya nyumba yako kimya mpaka baba yako aje akuone. Mtu akitoka safari anasalimiana na watu wote wa nyumbani. Hata kama hukutoka safari ni kawaida kuamkia; lazima ufahamu uzima wa nyumba ingine ingawa mnaishi mji mmoja. Ukitembea huko nje watu watakuuliza 'nyumbani hawajambo?' Utajibuje kama hukuwasabahi asubuhi? Kuna hadithi ya kijana mmoja ambaye alikuwa hamjulii hali mama yake wakati wa asubuhi. Mama yake alikufa usiku. Yeye bila kujua alikwenda kilabuni kunywa pombe. Watu walikuja kumpasha habari huko huko kilabuni. Kazimoto, wewe ni mtu mzima sasa." "Jambo la pili," Baba alisema, "ni kwamba uliondoka hapa bila kutuarifu. Mama yako alikuwa halali. Siku moja alitembea kijiji kizima akiuliza kama maiti yako ilikuwa imeonekana mahali fulani. Mambo ya kina mama usiyachukulie kama ya kipuuzi. Ninasikia ulimjibu kwa ukali sana usiku. Ninataka kusikia ukinijibu hivyo hata mimi." Sikutaka ubishi nao. Kwa hiyo nilikiri makosa yangu. Baada ya kunipa maonyo zaidi walinipa ruhusa kuondoka. Kwa muda wa siku mbili kichwa changu kilikuwa kimepumzika huko nyumbani kwa Kamata. Sasa matata yalianza tena. Nami nilikuwa nimekuja nyumbani likizoni kupumzisha kichwa changu ambacho kilikuwa kimekwisha anza kuwanga kwa sababu ya kusoma. 75 5 Ikiwa siku ya Jumapili, siku ambayo Vumilia alikuwa ameniambia niende kumchukua, na ndugu yangu akiwa amekwisha anza kula kidogo ingawa si sana, sikuona kipingamizi cho chote cha kuweza kunizuia kwenda matembezi usiku. Ni kweli kwamba Baba alikuwa amenionya, lakini sikuona kwa nini alipaswa kuhusika sana na mambo yangu. Kwa hiyo siku nzima nikawa namfikiria Vumilia, jinsi ya kumleta na kumrudisha bila mama yake kutambua. Katika kumfikiria, hadithi yake ilinijia tena kichwani. Vumilia alikuwa mmoja kati ya wale wasichana ambao hutunza ahadi. "Mungu mmoja, sikuongopei!" alizoea kusema wakati akitoa ahadi. Lakini Vumilia hakuonekana kuwa msichana mwenye furaha: alikuwa hajapata kumwona baba yake. Jambo hili lilimfanya apoteze wachumba kwani wengi walimwita mtoto wa vichakani. 76 Hili halikuwa kosa lake. Lawama yote ilimwendea Tegemea - mama yake. Tegemea alipokuwa bado mwanamwari alifanya kazi ya umalaya. Alikuwa ametembelea miji mingi ya mwambao, Mombasa hadi Mtwara. Katika kurandaranda kwake alizaa watoto kadhaa, lakini wote hao walichukuliwa na baba zao. Tegemea alipoona kwamba vijana walikuwa hawamchukui, na kwamba kwa siku nzima alilala na shilingi tatu tu za mlevi fulani, alijiona siku zake zinakwisha, akakata shauri kuacha umalaya. Mimba aliyokuwa nayo aliitunza vizuri, akamzaa Vumilia, na mara moja akarudi kisiwani Ukerewe kabla ya yule bwana aliyehusika kuja kudai mtoto wake. Mahali alipokuja kuishi hapakuwa mbali sana na kwetu. Tegemea akajulikana sana kijijini kwa Kiswahili chake cha upesi na mawimbi; akaitwa Mswahili. Buibui alilokuja nalo kutoka pwani likawa kitisho kijijinii, akaacha kulivaa. Pole pole Uislamu akauvua, akaanza kula nyamafu na Ramadhani akawa anaisikia tu redioni. Mwishowe akaanza kuwa anapika pombe ya moshi. Pesa alizopata humo ndizo zilizomwezesha kuishi, kwani aliporudi kutoka pwani mikono yake, kama ya kiwete, ilikuwa haiwezi kushika jembe kutwa nzima. Maisha ya Tegemea mimi nilikuwa siyajali. Mimi nilimfa- hamu sasa Vumilia ambaye nilikuwa na uhusiano naye. Ya zamani hayanuki. Usiku ulipoingia, baada ya kula, tulikwenda kulala. Tulipoona kwamba wazee walikuwa wamekwisha lala, mimi na Kalia tulichukua fimbo zetu, tukashika njia kuelekea nyumbani kwao Vumilia. Kwa kuwa tulikuwa wawili na mwezi ulikuwa ukiwaka hatukuogopa cho chote. Nilishangaa nilipomwona Kalia aliyekuwa nyuma yangu, anakimbilia mbele. "Kuna nini?" nilimwuliza. "Mtu anatufuata!" 77 Kutazama nyuma tuliona mbwa wa nyumbani kwetu. Tuliwarudisha kwa kuwatupia mawe. Tuliendelea. Yeye mbele, mimi nyuma. Mwishowe tuliukaribia mji wa Tegemea. Mji wenyewe ulikuwa na nyumba moja yenye vyumba vinne. Yeye alilala chumba chake, Vumilia chumba kingine karibu na mlango wa nyuma. Chumba kingine kilikuwa cha maongezi, na kilicho- baki kilikuwa kikitumika kama jiko. Tulipofika nyumbani kwa Tegemea tulianza kutembea pole pole kwa uangalifu, lakini hata hivyo, ng'ombe aliyekuwa amefungwa kwenye mti alitoa pumzi ndefu tulipopita karibu naye. Kalia sasa alirudi nyuma yangu, tukawa tunanyatia kuelekea upenuni. Ndani ya chumba cha Vumilia taa ilikuwa imekwisha zimwa. Chumba cha Tegemea kilikuwa bado na mwanga. "Tumewahi sana," Kalia alisema pole pole. "Nyamaza," nilimwambia. Tulikwenda kwa vidole mpaka mlango wa nyuma, tukajibanza ukutani. "Ha! ha! ha! ha!" tulisikia sauti ya jambazi fulani likicheka chumbani kwa Tegemea. "Kama ningeoa mwanamke kama wewe, nafikiri ningepata furaha hapa duniani. Mke wangu, ingawa nimezaa naye watoto wamekua, nilimwoa kwa kufanyaje tu. Leo nikitoka hapa nafikiri nitampa mgongo usiku mzima." "Uwongo wako!" Tegemea alisema. "Babu atafufuka kama nikisema uwongo. Unafikiri nina haja naye tena?" "Uwongo wako! Mbona hata hujafikiria kunioa?" "Mimi ningeweza kukuoa isipokuwa jambo moja kuhusu wewe linanichukiza." "Jambo gani hilo?" "Usikasirike lakini." 78 "Sema, ni jambo gani?" "Una tamaa sana ya pesa, yaani huwezi kumpenda mtu bila pesa. Huku shamba mwanamke hanunuliwi. Lakini mimi umenimalizia karibu pesa zote anazoniletea mtoto wangu. Hata hivyo bado hutosheki. Sasa unadai gauni. Unafikiri mimi pesa nitazitoa wapi?" "Kama jambo la gauni limekuudhi vaa suruali yako uende zako! Gauniii! Gauni! Gauni limekuwa gauni. Vaa suruali uende zako! Leo hufanyi jambo lo lote nami. Yaani unanifikiria mimi masikini omba-omba. Gauni! Mwenzio napoteza heshima yangu yote mbele ya binti yangu kwa ajili yako; unafikiri kuwa hatusikii! Mapenzi gani kuliko hayo? Gauni! Haya chukua suruali yako!" "Hasira yote hii ya nini?" "Nimesema v-a-a s-u-r-u-a-l-i u-ende zako!" "Unataka kunitoa nje kama kwamba sikuzaa! Haya chukua!" "He! he! he! " Tegemea alicheka. "Sasa hizi pesa umezitoa wapi? Bwana'ngu kila siku matata. Ngoja kidogo niweke mto wa pili." Tulisikia mlango wa chumba unafunguliwa. "Ninakwenda kujisaidia, nitarudi sasa hivi. Nikute umelala." Tuliposikia hivyo tuliondoka karibu na ukuta. Tuliinama ndani ya majani yaliyokuwa karibu na nyumba. Tegemea alitoka nje na kanga moja, akakojoa karibu sana nasi. Hakukawia akarudi ndani. Tulirudi tena ukutani. Kalia alikuwa akicheka kwa ndani hali ameziba mdomo. "Anayezungumza humo ndani umemtambua?" aliniuliza. "Nafikiri nimemtambua." "Ni Kabenga." "Kumbe mzee huyu hatari! Uhusiano ulianza lini?" "Tangu zamani," Kalia alisema, "isipokuwa mlikuwa bado 79 hamjagongana kama leo. Nasikia uhusiano huu ndio umeleta ule mpango wa kumwoza Vumilia kwa Manase. Tuza anapinga sana uchumba huu, na Manase mwenyewe hapendi. Juzi juzi walimtuma Vumilia kwenda kuzungumza kidogo na Manase. Lakini nasikia Vumilia alimkuta Manase anaishi na kimada. "Gonga dirisha umechukue mke wako twende, naona baridi." Alipomaliza kusema hivi mlango wa nyuma ulifunguliwa pole pole. "Mbona mnazungumza kwa sauti ya juu namna hii?" Vumilia alisema. "Tayari twende?" nilimwuliza. "Ngoja nivae,"alijibu. Alirudi ndani. Hakukawia. "Twendeni; tangulieni mbele kidogo." Tulitangulia. Tulimwacha nyuma akifunga mlango. Baada ya muda alikuwa pamoja nasi. "Wanaume wawili bado mnatembea na fimbo; woga gani huo!" alisema. "Hatuogopi kitu cho chote," nilijibu. "Mtanirudisha saa ngapi?" aliuliza. "Saa kumi na mbili." "Saa kumi na mbili kutakuwa karibu mchana. Mimi nataka kurudi saa kumi. " Wakati huu nilisimama kujisaidia. Kalia na Vumilia waliendelea mbele. Hawakufika mbali nao wakasimama kuningoja. Nilimwona Kalia anamshika Vumilia kiunoni. "Acha! Humwogopi kaka yako?" Vumilia alisema. "Wewe shemeji yangu, kwa hiyo usijali sana." Nilipowakaribia Kalia aliondoa mkono wake. Tuliendelea kimya mpaka nyumbani. Tulipofika nyumbani, tulipita mlango wa nyuma. Ndani ya nyumba Kalia alianza kutoa manung'uniko yake ambayo nilifikiria kuwa ya kitoto. miaka mia moja iliyopita, Afrika Mashariki imekumbwa na mabadiliko mengi ya kiuchumi na kisiasa. Mifumo ya jamii imebadilika. Katikati ya karne iliyopita baadhi ya jamii zetu zilikuwa katika hatua mbalimbali za mfumo wa ujima; baadhi zilikuwa katika hatua mbalimbali za mfumo wa ukabaila. Bali katika kipindi hiki dharuba ya ubeberu katika umbo la ukoloni na baadaye ukoloni mam- boleo imezisukumizia jamii zote hizi katika mfumo wa ubepari. Ukoloni umerutubisha mbegu za upinzani na utaifa, na umejikuta ukikabiliwa na madai ya wananchi ya uhuru na demokrasi na usawa wa kiuchumi. Baada ya uhuru madai haya yamepenya pia - na ilibidi yapenye - katika utamaduni, katika fasihi, na hasa katika ushairi. Mikatale ya kisiasa na kiuchumi ya ukabaila na ukoloni imekataliwa. Mikatale ya kisanaa (km. katika ushairi) vile vile imekataliwa. Mipaka ya kisanaa iliyowekwa na jamii hizo kwa matumizi na manufaa ya mabwana wa jamii hizo imekiukwa. Mgogoro huu wa ushairi ni sehemu na ni tokeo la mivutano hiyo ya kijamii. Mazingira mapya ya mwamko wa kitaifa baada ya uhuru, mwamko wa kujitafuta asili na kujitafutia mustakbala wenye matumaini mapya kwa umma umewachochea watu waanze kusaili mapokeo yote, mazuri na mabaya, na waanze kutafuta miundo mipya ya kijamii na miundo mipya ya kisanaa yenye kusadifu vizuri zaidi hali na migogoro ya leo. Bali miundo hii mipya ya kisanaa haitafutwi 2 ile iwe badala ya ile ya zamani; inatafutwa ili iwe ni nyongeza kwa ile iliyopo, na iwe ni mchango wa kizazi hiki katika utajiri wa sanaa tulioachiwa na vizazi vilivyotangulia. Na si miundo yote ya sanaa inayopendekezwa kutumika sasa ni mipya; baadhi ni ya kale iliyokuwa imesahauliwa na ambayo sasa inafufuliwa kwa sababu inaweza kubeba maudhui ya leo. Baadhi ni miundo ya kawaida ya kifasihi simulizi ambayo inaingizwa katika fasihi andishi ya Kiswahili. Mgogoro huu, basi, ni wa kihistoria na umekusanya nguvu zake toka nyakati za nyuma. Tangu mwanzo wa ukoloni pamekuwa na ukinzano "usiotamkwa" baina ya wale waliotunga kwa kufuata kanuni za mapokeo na wale waliotunga mashairi guni. Mvutano huu uliendelea hadi ukafikia wakati ambapo ilibidi hata kina Amri Abedi waukubali ushairi huu ni mtindo katika ushairi wa Kiswahili, hasa baada ya tafsiri ya Shakespeare: Juliasi Kaisari, iliyofanywa na Rais J.K. Nyerere. Kadhalika mgogoro huu umekusanya nguvu kutoka katika uwili wa fasihi yetu: fasihi simulizi na fasihi andishi, na mwamko wa kifasihi wa kuiangalia fasihi simulizi kwa jicho jipya, kwa madhumuni ya kuitumia kuirutubisha fasihi andishi (katika ushairi wa fasihi simulizi ambayo haijaathiriwa hata kidogo na maandishi ni nadra sana kukuta vina na urari wa mizani). Kwa hiyo, basi, chimbuko la mgogoro huu limechangamana sana. Maelezo ya wanajadi hayatuambii lolote juu ya jambo hili. Licha ya mazingira ya kiuchumi na kisiasa, hata mazingira ya kiisimu ni mazuri, na yanaurutubisha mgogoro huu. Hivi leo Kiswahili si lugha ya Pwani tena kama ilivyokuwa karne mbili zilizopita, ila inazidi kuwa chombo cha utamaduni wa Afrika Mashariki nzima. Leo hii maana ya dhana "fasihi ya Kiswahili", "ushairi wa Kiswahili" si ushairi au fasihi ya watu wa Pwani, bali ni ushairi na fasihi ya watu wa Afrika Mashariki inayoeleza hali halisi ya hapa kwa lugha ya Kiswahili. Kwa ufupi, leo Kiswahili katika matumizi yake mbali mbali (ya kawaida, ya kifasihi, n.k. ) hakikubali ufafanuzi wowote uliojikita katika misingi finyu ambayo haizingatii hali mpya iliyopo. Maendeleo na mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa tuliyoeleza yamekuwa na tokeo moja kubwa na muhimu sana la kitamaduni: kukua na kupanuka kwa elimu. Baada ya Uhuru, elimu ya msingi, sekondari, vyuo na chuo kikuu 3 imepanuliwa. Somo la Kiswahili (lugha na fasihi) limewekewa mkazo mkubwa katika mashule na vyuo. Wanafunzi na walimu wa Kiswahili wamepata nafasi ya kudadisi kitaaluma masuala mengi ya kifasihi, likiwemo suala la "ushairi ni nini". Wamepata pia nafasi ya kusoma fasihi za mataifa mengine, na hivyo kupanua mawazo yao kuhusu fasihi. Wameona namna watu wa mataifa mengine wanavyotunga au walivyokuwa wakitunga ushairi wao. Wameulinganisha ushairi huo na ushairi wa Kiswahili na wa makabila mbali mbali ya Afrika Mashariki na wamegundua kuwa, mbali na lugha, yapo mambo mengi yanayofanana baina ya ushairi wa mataifa mbali mbali - ule ulioandikwa na ule unaosimuliwa kwa mdomo tu. Imedhihirika pia kuwa msisitizo juu ya vina na mizani ulikuwa umeukwamisha ushairi wa Kiswahili katika umbo lisilobadilika. Hali hii ilipingana kimsingi na kanuni ya sanaa ya uumbaji. Washairi wengi wa Kiswahili wakawa hawaumbi; wakawa wanayapanga tu mawazo yao katika umbo la vina na mizani na mhariri wa Uhuru na Mzalendo anayachapisha. Zaidi ya hayo, imedhihirika pia kuwa fikra kuwa vina na urari wa mizani ni "roho" na "uti wa mgongo" wa ushairi imepotoka kimsingi; ni nadharia ya ushairi ambayo haiwezi kuthibitika katika uchambuzi thabiti wa kitaaluma. Kwa hiyo, basi, upotofu wa fikira yenyewe ni kichocheo kingine cha mgogoro huu. Katika makala haya nia yetu ni kuyachunguza madai na hoja za wanajadi ambazo wamekwisha kuzitoa katika mjadala huu. Tutachunguza dai lao kuwa ushairi wa mtiririko ni wa kigeni (Kizungu); tutachunguza fikira zao kuhusu ushairi guni wa Kiswahili; tutachunguza fafanuzi zao juu ya hulka ya ushairi; tutayahakiki maelezo yao juu ya maana ya ushairi; na kisha tutatoa maelezo yetu kuhusu ushairi ni nini. Kwa hakika mawazo mengi ambayo tutayasema hapa tulik- wisha kuyasema katika makala ambazo tumeandika juu ya suala hili, katika makongamano, mihadhara, malumbano ya kishairi, n.k. Hata hivyo, kwa faida ya wale ambao hawajasoma makala zetu, na kwa manufaa ya wale wadhanio kuwa nia yetu ni kuua ushairi wa Kiswahili, na mwisho, kwa faida ya wale wadaio kwamba eti sisi tunadai kuwa "ushairi wa Kiswahili wenye kanuni za kawaida haufai tena", tunaziweka hoja na maelezo yetu hapa ili yaeleweke 4 kinaganaga, kama watakuwa tayari kuyasoma kwa nia ya kuelewa. Upekee wa ushairi wa Kiswahili uko katika kanuni za vina na urari wa mizani? Vina na urari wa mizani ni mambo ambayo kwa karne nyingi yalifikiriwa kuwa muhimu sana katika ushairi wa Asia na Ulaya. Mpaka hii leo, ushairi wa Kiarabu, kama ushairi wa Kiswahili, bado unayasisitiza mapambo haya. Lyndon Harries ameeleza hivi: Kwa mujibu wa arudhi ya Kiarabu, ilishikiliwa kuwa, bila ya kujali urefu wa shairi, vina vya mwisho katika kila ubeti lazima vipatane tangu mwanzo hadi mwisho wa shairi. Kwa hiyo hata katika tungo zenye vina vya kati, mtunzi akisha amua tu kutumia kina fulani katika kipande eha kwanza, ilibidi akitumie kina hicho hicho hadi mwisho. Watunzi wengi walipendelea zaidi kutunga mashairi ambayo vina vyake vya kati ni tofauti na vile vya mwisho... Utaratibu wa namna hii bado unafuatwa katika mashairi mengi ya Kiswahili. Maneno haya karibu yanakubaliana na maneno ya Mnyam- pala, ambaye amesema: Shairi liwe na vina vinavyopatana, hususa mwishoni mwa kila ubeti, kwa shairi lote zima, ingawa vina vya katikati vikosekane kwa utenzi wote. Kauli ya Amri Abedi pia inakubaliana na maneno hayo: Kwa desturi vina vya silabi ya 16 (vya mwisho) huwa vya namna moja katika beti zote za shairi zima. Sheikh Amri Abedi mwenyewe, kwa kusoma mashairi ya Kiingereza, Kihindi, na Kiarabu, alikiri kuwa ushairi wa Kiswahili hauna upekee wowote na wala siyo tofauti sana na ushairi wa mataifa hayo: Mpaka makamo haya nimesoma mashairi ya lugha ya Kiingereza, ya Kiurdu, ya Kiarabu, na kadhalika ya Kiajemi aliyonifundisha mmoja katika masheikh zangu, Maulana Jalal-ud-Din Qamar H.A. Kwa njia hii nimeweza kujua angalao chembe namna watu wa mataifa mengine wanavyokusanya fikira na Kuzipanga, namna ambayo si mbali na ile iliyotumiwa na watungaji mashuhuri wa Kiswahili 5 wa zamani na sasa. Katika utangulizi wake kwa diwani ya Mnyampala, Waadhi wa Ushairi,Amri Abedi alitoa kauli ambayo inabidi ijadiliwe kwa kuwa imezua upotofu usio wa lazima. Alisema: Wasemao kuwa mashairi ya Kiswahili asili yake ni Kiarabu wanazua. Lau wangekuwa wanajua Kiarabu wasingesema hivyo. Taratibu za mashairi ya Kiarabu na ya Kiswahili ni tofauti kabisa. Ukweli ni kwamba Waislamu waliandika habari na masimulizi ya dini na nyimbo au ushairi wa Kiarabu kwa herufi za Kiarabu. Lakini kanuni za mashairi ya Kiarabu ni tofauti kabisa na za mashairi ya Kiswahili. Kauli hii ya Sheikh Amri Abedi ni potofu kabisa. Ushairi wa Kiswahili na Ushairi wa Kiarabu si tofauti kabisa. Sheikh Saadani Kandoro, kwa kutaka kuonyesha ushairi wa Kiswahili ulivyo tofauti kabisa na ushairi wa Kiarabu, anaziorodhesha tofauti hizo: 1. Ubeti wa shairi la Kiswahili huwa na mistari 3, 4, 5, au zaidi. Na hivyo ndivyo yalivyo mashairi mengi ya Kiswahili katika vitabu na magazeti. Lakini ubeti wa shairi la Kiarabu huwa na mstari mmoja tu. 2. Mstari huo wa shairi la Kiarabu hugawanyika sehemu mbili na kila sehemu inaitwa misraa. 3. Mashairi ya Kiarabu hayana shuruti za vina. Shairi lenye kuendeleza vina vya kati mpaka vya mwisho huonekana si shairi la Kiarabu. 4. Mashairi ya Kiswahili si lazima vina vya mwisho vifanane tangu mwanzo hadi mwisho, ingawa huwa vizuri zaidi hali hiyo ikiwepo katika shairi la Kiswahili. Kitu cha lazima ni kufanana kwa vina vya kila ubeti." Hebu tuzidadisi kauli hizi za Kandoro. Anasema ubeti wa shairi la Kiswahili huwa na mistari 3, 4, 5 au zaidi. Kauli hii inabidi kurekebishwa na kuwa: ubeti wa shairi la Kiswahili huwa na mistari 2, 3, 4, 5 au zaidi. Anasema kuwa ubeti wa shairi la Kiarabau huwa na mstari mmoja tu. Jambo hili lazima litazamwe kwa uangalifu zaidi, na haifai kulipitia juu jau tu. "Ubeti" (wingi: beti) ni neno lenye asili ya Kiarabu. Kufuatana na utaratibu wa kijadi 6 wa shairi (kasida) la Kiarabu, kila ubeti unazo misraa mbili. Lakini neno hili, katika ushairi wa Kiswahili, inavyoelekea limepanuka: shairi la Kiswahili siku hizi laweza kuwa na ubeti wenye vipande au "misraa" nyingi. Hili si jambo la kustaajabia. Isitoshe kabla ya kuingizwa kwa hati ya Kirumi, mashairi na tenzi nyingi za Kiswahili zilizoandikwa kwa hati ya Kiarabu zilikuwa na mstari mmoja tu kila ubeti. Mstari huo (au ubeti huo) ulitakiwa ujitosheleze kwa maana. Sifa hii ya kujitosheleza imo pia katika ushairi wa Kiswahili, ingawa Saadani Kandoro hakuitaja. Washairi wa Kiswahili wanakubaliana kuwa ubeti wa shairi la "jadi" ni lazima ujitosheleze kwa maana, yaani maana yake isiwe nusu nusu. Kadhalika, mstari wa shairi la Kiswahili unapaswa kujitosheleza, yaani utoe dhana kamili, usiwe nusu sentensi. Kanuni hii ya kujitosheleza imo pia katika ushairi wa Kiarabu. Mtaalamu mmoja wa ushairi wa Kiarabu, A. J. Arberry, anaeleza hivi "Katika ushairi wa Kiarabu, ilifikirika kuwa ni dosari kuruhusu muundo wa sentensi kuvuka ubeti (au mshororo mmoja wenye misraa mbili) na kuendelezwa katika mshororo unaofuata, kila mshororo ulifikiriwa kuwa ni kauli inayojitosheleza." Anasema kuwa "shairi la Kiarabu halina shuruti za vina". Kauli hii lazima irekebishwe na kuwa: Shairi la Kiarabu halina shuruti za vina vya kati. Na kwa nini "shairi lenye kuendeleza vina vya kati mpaka vya mwisho" lionekane siyo la Kiarabu? Kwa kweli hata shairi la Kiswahili halina shuruti ya vina vya kati na yapo mashairi mengi ambayo hayana vina vya kati na bado yanakubalika kuwa ni ushairi wa Kiswahili. Utenzi wa Hamziya, mathalan, una kina cha bahari tu, hauna vina vya kati. Mashairi mengi ya zamani (kabla ya mwaka 1700) hayana vina vya kati (vya misraa), yamezingatia kabisa kawaida za ushairi wa Kiarabu kama anavyozieleza Kandoro (ingawa anasahau au hajui kuwa baadhi ya mashairi ya Kiarabu yana vina vya kati). Aidha, kauli hii ya Kandoro haikubaliani sana na kauli ya Amri Abedi isemayo: Kwa desturi vina vya silabi ya 16 huwa vya namna moja katika beti zote za shairi zima, na vina vya silabi ya 8, kwa desturi inayotumika sana, huwa tofauti ubeti hata ubeti. Sheikh Amri Abedi alitaka kutueleza kuwa ushairi wa 7 Kiswahili ni tofauti kabisa na wa Kiarabu, jambo ambalo hakuthibitisha. Kandoro alitaka kututhibitishia kuwa ushairi wa Kiarabu ni tofauti na wa Kiswahili. Je, ni kweli kuwa ushairi wa Kiswahili ni tofauti kabisa na ushairi wa Kiarabu? Kwa hakika ingewafalia sana wanajadi iwapo wangejion- doa katika "uzalendo" finyu, katika gamba la "Uswahili", na kuuona ukweli kuwa arudhi ya Kiswahili imeathiriwa sana na arudhi ya Kiarabu, ingawa ushairi wa Kiswahili asili yake siyo Uarabuni. Kanuni iliyotajwa hapo juu, ya "vina vya silabi ya mwisho kuwa vya namna moja katika beti zote za shairi zima, na vina vya kati kuwa tofauti tofauti" iko katika ushairi wa Kiarabu na wa Kiswahili. Vile vile urari wa mizani katika beti zote za shairi ni kanuni katika ushairi wa Kiarabu na wa Kiswahili. Mifano aliyoitoa Kandoro katika kitabu chake haitupatii picha sahihi ya muundo wa shairi la Kiarabu kwa kuwa amedondoa mshororo mmoja mmoja tu. Hebu tutoe mfano wa shairi zima hapa chini: (Katika hati ya Kiarabu) (Katika hati ya Kirumi) Abu Nuwas Hamil - ul - hawa ta'ibu yastakhifuhu - utarabu Inn baka'a yahikku lahu laysa maa bihi la'abu 8 Kulama inaqadha sababu minki 'ada li sababu Tadhakina lahiyatan wal - muhibu yantahibu Ta'a jabiyna min sagamy sihaty hiya al - ajabu 14 Maana yake: Mtu mwenyewe hawa yu mchovu, jaziba humpepesua. Akilia yuna haki, jukumule si mzaha. Sababu moja ya dhiki yangu ikiisha nyingine hurejea kwangu toka kwako. Wewe wacheka kwa furaha wakati muhibu wako aom- boleza. Waajabia dhiki yangu - kwamba ningali na siha ndiyo ajabu kabisa. Hapa tunaona kuwa kina cha kati katika mstari wa kwanza kinapatana na kina cha mwisho, lakini vina vya mwisho ni vile vile toka mstari wa kwanza hadi wa mwisho. Na hii ndiyo desturi ambayo imekuwa ikifuatwa katika ushairi wa Kiarabu, na hata leo hii inafuatwa. Suala la athari za ushairi wa Kiarabu kwenye ushairi wa Kiswahili si jambo ambalo lahitaji mjadala mrefu kwa vile ni dhahiri sana. Waandishi wa kwanza wa mashairi ya Kiswahili wali kuwa masheikh na walimu wa dini, waliotaalamika katika lugha ya Kiarabu na Kurani (wengi wao wakiwa Waarabu au wale waliochanganya nasaba). Na kwa kuwa kila kitu eha asili ya Kiarabu kilikuwa ndicho kipimo eha ustaarabu, hata walipoanza kuandika mashairi au kutafsiri kasida au tenzi za Kiarabu kwa Kiswahili walilichukua kuwa ni jambo linalokubalika kuwa shairi lazima liwe na urari wa vina na mizani. Dhana nyingi za ushairi wa Kiarabu zikaanza kutumika katika ushairi - andishi wa Kiswahili. Msamiati wenyewe unaotumika, shairi, ubeti, mizani, hamziya, tasmit, takhimis, tathlitha, tarbia, n.k., ni wa Kiarabu. Ni kweli ingawa mitindo mingi ilianzishwa, lakini mitindo hiyo yote ilikuwa kwenye urari wa mizani na vina. Hali inayosemwa hapa inafanana na ile iliyousibu ushairi wa Ulaya baada ya enzi za ustawi wa himaya ya Wayunani, ambapo washairi wengi walifuata kanuni zilizokuwa na asili ya kanuni za ushairi wa Kiyunani. Kumbe utungaji wa mashairi katika vina na urari wa mizani si aambo liwezalo kuupambanua ushairi wa Kiswahili: 9 kwa asili si jambo la Kiswahili, bali ni athari ya kigeni (Kiarabu). Kuyaita mambo haya "roho" ya ushairi wa Kiswahili ni sawa na kusema kuwa hapakuwa na ushairi wa Kiswahili kabla ya kufika kwa Waarabu. Maneno ya wanajadi yangeweza kusemwa pia na Mwarabu au Mwajemi kuhusu ushairi wa kwao. Kwa kweli yalikwisha kusemwa na mtaalamu mmoja wa ushairi wa Kiarabu, R.A. Nicholson, am- baye anatuambia hivi: Ushairi usio na vina ni jambo geni kwa Waarabu, ambao kwao vina si pambo la kuvutia au "kifungo chenye udhia", bali ndiyo roho ya ushairi. Kwa upande mwingine, ushairi wa asili wa Kiswahili (na wa Kibantu kwa jumla) hausisitizi vina wala urari wa mizani. Kwa hiyo basi malenga wa Kiswahili wanaotetea vina na mizani hawatetei mambo ya msingi katika ushairi wa Kiswahili, bali wanatetea athari za Kiarabu, ijapokuwa kinafsi sio kusudi lao. Kwa kweli wengi wanaamini kuwa wanachokitetea ndio "Uafrika". Vina na mizani haviupam- banui ushairi wa Kiswahili, bali vinaunasibisha na ushairi wa kigeni, hasa wa Kiarabu na Kiajemi. Lipo dai moja la kuchekesha kuwa ushairi wa mtiririko ni barua, insha au mkusanyo wa maneno tu bila utaratibu wowote. Dai hili ni la kuchekesha kwa sababu hakuna andiko lolote lenye mantiki na maana ambalo halina utaratibu wowote. Pili barua si lazima iwe nathari. Katika ushairi wa Kiswahili ipo desturi ya kuandikiana barua kishairi. Barua hizo huitwa risala, na kwa kawaida huanza kama hivi: "Risala ninakutuma..." au "Tumwa ukifika (mahala)..." n.k. Kwa hiyo inawezekana shairi fulani la mtiririko likawa ni barua na ni ushairi wakati huo huo. Kuhusu ushairi wa mtiririko kuwa "insha" jibu litatolewa baadaye tutakapojadili maana ya ushairi na mbinu za ushairi. Jambo la kudokeza hapa ni kwamba mashairi ya mtiririko si "huru" hata kidogo, yanazo mbinu, kunga na kanuni yake, na si rahisi kuyatunga. Ila katika kanuni zake hizo kuna uhuru mkubwa wa kubuni na kutunga. Kanuni yake kuu, ambayo kila mtungaji wa shairi yabidi aitimize, kanuni ambayo ndiyo roho ya mashairi haya, na roho ya fasihi kwa jumla, ni kwamba muundo wa shairi lazima uamuliwe na kufungamana na mawazo, mtiririko wa hisia, na makusudio ya mtunzi. Msimamo wetu hapa ni kwamba hakuna muundo au 10 miundo maalum ambayo lazima ivaliwe na kila shairi, au sheria maalum zisizotanguka ambazo lazima zikaririwe na kila mshairi kama "sala ya bwana". Sasa na tuyapitie kwa ufupi madai mawili yanayotumiwa na wanajadi kuuhujumu ushairi wa mtiririko. Dai la "ugeni" na dai la "uguni". "Ugeni" katika Ushairi wa Kiswahili Wanajadi kama vile hayati Chiraghdin, Mayoka, Kandoro, Al - Amin Mazrui na Ibrahim Sharif wanakubaliana kuwa vina na urari wa mizani ndivyo vitambulisho vya ushairi wa Kiswahili. Ndiyo maana wakauita ushairi wa mtiririko wa kina Kezilahabi, E. Hussein, Jared Angira, Crispin Hauli. F. Senkoro, na wengine kuwa ni mtindo wa Kizungu kwa lugha ya Kiswahili. Wanajadi wengine, kama Tigiti Sengo, wanaukubali kuwa ni ushairi, lakini si ushairi wa Kiswahili. Msimamo huu wa wanajadi unatokana na fikira potofu juu ya "ugeni", au "upya"; pili unatokana na kutoijua hulka na historia ya ushairi wa Kiswahili. Kwani ugeni wanaouhofu ni nini? Ugeni si jambo la ajabu sana. Ugeni wa kitu katika uwanja fulani wa maisha unaweza kujitokeza kwa namna tatu: ama kitu chenyewe ni kipya kabisa, na kimetoka nje; au kitu cha asili kilichokuwepo kimeathiriwa na kitu kigeni ama kitu hicho ni kipya na kimegunduliwa mahali hapo hapo. Ndipo watu baadaye huweza kusema kuwa "kitu hiki kina asili ya huko" au "kile kimeathiriwa na hicho", au "hiki kilibuniwa na fulani". Kwa mujibu wa maelezo haya, Uislamu una asili ya Kiarabu, Ukristu una asili ya Kiyahudi, mifumo ya elimu na serikali tuliyo nayo ina asili ya Kizungu, riwaya na tamthiliya ya Kiswahili vina asili ya Kizungu, taarabu ina asili ya Kiarabu, .nk. Sasa je, ushairi wa mtiririko una asili ya Kizungu? Kwa hakika, dai hili la wanajadi lingekuwa sahihi iwapo mtindo wa namna hii usingekuwapo katika fasihi simulizi ya Kibantu, ambayo ni pamoja na ile ya Kiswahili; na iwapo ingekuwa ni kanuni mojawapo ya sanaa ya ushairi kutovyaza mitindo mingine ghairi ya ile iliyopo. Mtindo usiofuata vina na urari wa mizani ni wa kijadi katika fasihi ya Kiswahili na Kibantu. Na ujadi wa mtindo huu ni ujadi wa utangu; mtindo wa vina na urari wa mizani umekuja baadaye kabisa. Kwa mtu yeyote ambaye amekwisha kushughulika na 11 fasihi simulizi lau kidogo jambo hili si gumu kueleweka. Ipo mifano mingi ya ushairi wa namna hii. Hapa chini tutatoa mifano michache kwa manufaa ya wale ambao hawajui tunaongelea nini. Mfano wetu wa kwanza ni wimbo (ushairi) wa kubem- bele za mtoto: silie mama silie ukalia waniliza wanikumbusha makiwa makiwa ya baba na mama baba na mama watende wanioza dume kongwe halisafiri halendi kazi kumega matonge. Huu ni wimbo ambao umekuwa ukiimbwa na kina mama wa Kiswahili kubembelezea wana wao, ingawa unagusa pia hali halisi ya kukandamizwa kwa wanawake: kulazimishwa na wazazi kuolewa na mwanamume mzee. Athari ya mguso wa wimbo huu hasa unatokana na lugha ya mkato, na takriri, yaani marudiorudio ya maneno au silabi fulani fulani yanayovuta hisi za msikilizaji, mwimbaji, au msomaji (silie... silie... wani... wani... makiwa...makiwa... baba na mama... baba na mama... wa... wa... hali... hale... ). Katika wimbo huu tunaona kuwa kipande cha kwanza, cha pili, cha tatu, cha tano, cha sita, cha saba, cha nane vina urari wa mizani nane; kipande cha nne kina mizani tisa. Vina katika maana ya wanajadi havipo ila katika misitari minne ya mwisho tunaona utaratibu namna hii: baba na mama watende wanioza dume kongwe halisafiri halendi kazi kumega matonge Katika mstari wa kwanza fungu-konsonanti -nd- linalingana na fungu-konsonanti la mwisho katika mstari wa tatu; na silabi ya mwisho mstari wa pili -ngwe- inatofautiana kidogo na -nge- ya mstari wa nne. Lakini, ukweli ni kuwa urari wa mizani unatokana na mahadhi ya wimbo huo, na haupo kwa sababu ni "roho" ya ushairi! Sasa tutazame mfano wa ushairi wa majigambo kutoka kwenye fasihi simulizi ya Kihaya. Jigambo hili ni la kiwindaji; mwindaji alilitamba mbele ya mtemi baada ya kutoka kwenye 12 uwindaji wa mafanikio: ( Akaruru) Natonya nko'rulabyo, ninye Nilyegira eya Ngaiza Ngaiza eya Ruyango Ruyango eya Karashani Karashani eya Keitirimbila Keitirimbila eya Kagomborora Kambaile ndy'omwange mpulila engoma zajuga zona Ngambila mukazi wange Kabigumila Nty'ompe eichumu Iyange Kanywa-bwamba amoi no omuhoro gwange. Rutema bitega nturuke ntabale Omukazi ai mushaija wange kankuchumbile akatoke Nti mukazi wange tokichumba byakuhya mara kandi tokokya byakujumbula, nti shana okwate akashweko kake ondabye omumaino nturuke ntabale! (Akaruru) Nilwo nayebembeize embwa yange Owo Otakiau Ekajumala kuluga Omwihangiro Lyamkumbya na Kairu, ekashoora Omurushanga Iwa Karebe nkahulila yambilikira, nti tora! Waitu elyo nachumisile nilyo Rugaba kandekelele ao, ebigambo bingi bikatanga enkoko okwekukusa Waitu batole ebikwato byange ebi. Tafsiri: (Vigelegele) Naingia kama radi, ni mimi Niyegira mtoto wa Ngaiza Ngaiza mtoto wa Ruyango Ruyango mtoto wa Karashani Karashani wa Keitirimbila Keitirimbila wa Kagombolola Nilipokuwa kwangu nilisikia ngoma (za wito) zinalia 13 Nikamwambia mke wangu Kabigumila Nipe mkuki wangu "Mnywa-Damu" pamoja na mundu wangu "Mkata-Miguu" nitoke kuitika wito. Mke wangu akanisihi: Mume wangu hebu nikupikie ndizi kwanza Mimi nikamwambia: Mke wangu huwezi kupika zikaiva Wala huwezi kuchoma upesi upesi labda chukua jani la mgomba (lililotumika kufunikia ndizi) Unipitishie katika meno Niitikie wito. (Vigelegele) Ndipo nilipotangulia na mbwa wangu Usiyem- dhania Aliteremka kutoka mbuga ya Lyamkumbya na Kairu hadi kwenye msitu wa Karebe Nikasikia ananiita (kwa kubweka ) Nikamjibu Kamata ! Mheshimiwa, mkuki mmoja niliotupa mnyama akawa maiti... Ee, Mpaji (Rugaba) nikomee hapo Maneno mengi yalimzuia kuku kutawaza (baada ya kwenda haja) Mpaji, pokea mawindo haya. Hatuna haja ya kujadili mbinu zilizotumika katika kijigambo hiki. Jambo muhimu hapa ni kuona kuwa hakuna urari wa mizani na vina katika ushairi huu. Na ushairi wote katika fasihi simulizi za Kibantu uko hivi - labda tu uwe umeingiliwa na maandishi pamoja na kanuni za vina na urari wa mizani. Kwa nini jigambo hili tunaliita "ushairi"? Jibu la swali hili tutalipata hapo baadaye tutakapojadili maana na kunga za ushairi. Kutokana na mifano hii, tunaweza kuhitimisha kuwa dai la wanajadi kuwa ushairi wa mtiririko una asili ya Kizungu halina msingi wowote. Wahenga wetu wamekuwa wakiimba au kusema ushairi wa namna hii kwa miaka nenda miaka rudi. Hapa lazima tuongeze jambo moja: tusidhani kuwa ipo tofauti ya ajabu baina ya "free verse" ya Kiingereza na ushairi huu. Pengine tofauti kubwa tunayoweza kuitaja ni kuwa "free verse" ni ushairi wa vitabuni, na ushairi huu ni 14 ushairi uishio pamoja na shughuli za kimaisha, kama kubem- beleza mtoto, kujigamba, n.k. Je, mtiririko ni mashairi gani? Suala la ushairi guni lilijitokeza katika mgogoro huu hasa kwa sababu ilitokea rai kuwa mashairi "mapya" ya mtiririko ni mashairi guni. Ushairi guni, Chiraghdin anasema, ni "tungo ambayo haikutosheleza sharuti za lugha, mizani, na vina". Kwa Sheikh Amri Abedi, ushairi guni ni ushairi "usio na vina". Kandoro na Mayoka wanakubaliana kuwa ushairi guni ni "ushairi wenye dosari". Kwa jumla, wanajadi wanakubaliana kuwa ushairi guni haufuati kanuni za vina au za urari wa mizani, au yote mawili. Kwa nini basi mashairi sa mtiririko yasiitwe mashairi guni, hasa kwa kuwa hayafuati kanuni za "kijadi"? Swali hili limepatiwa majibu tofauti toka kwa wataalamu na washairi mbalimbali. Farouk Topan anasema mashairi haya hayawezi kuitwa guni kwa kuwa "uguni" ni tokeo la kushindwa kufuata kanuni za vina, urari wa mizani na kutosheleza na watunzi wa mashairi haya hawajashindwa lolote. Chiraghdin naye, kwa kuwa anaamini kuwa mtindo huu ni wa Kizungu (blank verse au free verse), hawezi kuyaita mashairi guni. Hatuelezwi tofauti iliyopo baina ya mashairi guni na blank verse au free verse, bali tunaelezwa tu kuwa "tungo hizi zikikubaliwa .. basi ushairi wa Kiswahili utakuwa umeanguka kitakotako" (Iwapo ushairi guni umekuwepo tangu zamani na haujauangusha ushairi wa Kiswahili, kuna haki gani ya kudai kuwa ushauri wa mtiririko utauangusha ushairi wa Kiswahili?) Hata hivyo, msimamo wa Chiraghdin unaelekea kuwa na mkinzano ndani yake. Katika utangulizi wake kwa Malenga wa Mrima, anasema: "Shairi la Kiswahili hukosa umbo lake likikosa vina na mizani; na hapo huwa haliitwi tena shairi." Kisha anaongeza: "Umbo lake likilemaa huwa bado ni shairi, lakini huwa ni guni." Iwapo umbo la shairi ni vina na mizani, tungo itaendeleaje kuitwa shairi Iwapo haina vina na mizani? Upotofu wake unazidi anaposema kuwa umbo la ushairi la vina na mizani limekuwepo tangu ukale wa ushairi, na kwamba kilichobadilika ni kuv- yazwa kwa bahari mbalimbali za ushairi: "Kumetokea na kukua kwa bahari mbalimbali za ushairi katika hilo umbo lake." Tumeshaonyesha kuwa vina na urari wa mizani ni 15 athari za kigeni; hatuna haja ya kujirudia hapa. Mayoka na Kandoro wanakubali kuwa shairi guni ni shairi lenye dosari, lakini wanakanusha kuwepo kwa ushairi huu katika ushairi wa Kiswahili. Mayoka anasema: "Kwa kweli ushairi guni hauko katika ushairi wa Kiswahili." Kan- doro naye anasema: "Kwa ufupi wa maneno, hakuna aina ya shairi 'guni'. Mtunzi mwenye kujua hawezi kujigamba kwa kutunga tungo zenye kasoro na kuziita mashairi. Hathubutu hata kidogo kwani jambo hilo litamvunjia hishima yake." Ama kweli hii ni "ufupi wa maneno.. kwani "urefu" wake unaonyesha kuwa ushairi guni upo, hata kama wautungao hujivunjia "hishima". Kitu ambacho Amri Abedi mwenyewe (ambaye wanadhani wanatetea sheria alizoandika) alikikiri na kukiheshimu, Mayoka na Kandoro wanakikanusha. Yaelekea walifanya hivyo kwa kudhani kuwa wakikubali kuwepo ushairi guni katika ushairi wa Kiswahili basi tungedakia na kuuita mtiririko ushairi guni. Kwa kuwa yaelekea wapo watu wengine wenye fikira kama za kina Mayoka, basi inafaa tuchunguze, lau kidogo, iwapo kweli guni ni umbo mojawapo katika ushairi wa Kiswahili, au la. Historia ya ushairi-andishi wa Kiswahili inatuonyesha kuwa ushairi guni umekuwepo tangu zamani. Pili, historia hii inatuonyesha kuwa kwa kadiri ushairi guni ulivyozidi kuishi pamoja na ushairi uliofuata kikamilifu kanuni za vina na urari wa mizani, ndivyo ulivyozidi kukubalika kuwa ni fani mojawapo ya ushairi wa Kiswahili, hasa baada ya malenga mashuhuri kuukubali, na hata baadhi yao kuutunga. Tuchunguzapo kurasa za matoleo mbalimbali ya gazeti la Mamboleo tunakuta mashairi ambayo hayakufuata kanuni hizo. Katika toleo la 10, Oktoba 1923, tunakuta shairi "Shangilieni Mgeni Mambo Leo Kaingia", lililotungwa na Said Bin Kikulacho, ambalo, kwa kadiri ya kanuni za wanajadi lina dosari. Hapa tunadondoa beti chache: Mamboleo ana sifa zilizotupendeza Na mtakapo sifa zake kidogo nitawaambia Habari nyingi za pwani na bara hutuambia Shangilieni mgeni Mamboleo kaingia... 16 Na zikiwa habari ambazo hazipendezi Wenyi kuleta habari za fitina na kutukanana Fahamu atakujibu pasipo jina kutaja Shangilieni mgeni Mamboleo kaingia... Atupa habari za wezi waliopo tuwajue Twajua kuvunja nyamba kuna na wa Relwe Kuna Kampuni Sinzia mikononi hukuibia Shangilieni mgeni Mamboleo kaingia..." Kwa kweli, baadhi wa washairi wa siku hizo walikuwa hawajali vina vya kati kamwe (k.m. Mdanzi Hanassa), na wengine hawakujali sana urari wa mizani (Limo, Mdanzi) Lakini shairi ambalo halikutumia vina kabisa ni lile lililotoka kwenye Mambo Leo ya Desemba 1928, juu ya mnazi, lililotungwa na A. Pacha. Kwa vile sanaa ya shairi hili ni ya hali ya juu inafaa tulidondoe lote. Mnazi (Jibu la Shairi la Mti Gani wa Faida Ushindao Miti Pia? la Bwana Khamis) 1. Hili ni jawabu, la maswali yako Nililojaribu: na kwa Mamboleo Nasihi niseme: uniwie radhi, Ewe! Bwana Khamis: idadi ya miti Uliyohasibu: imepungukiwa Kwani mimi MNAZI umenirukia. 2. Sitafidhulika: wala kudharau, Utani wa miti: iliyo wenzangu, Kila mmojawapo humfaa bin Adam, Kwa leo, kwa kesho: humleta usalam. Hapana kibovu: kwa mwenyi busara, Na Mwenyezi Mungu yote amelinga. 3. Niruhusu bwana: nitoe sauti, Nionye mafaa: yashindayo miti, Hapa Tanganyika: Unguja na Pemba. Ni tangu asili: watu hunipenda. Linafahamisha: MNAZI jina langu Upunga, kitale, kidaka na dafu. 17 4. Koroma na nazi: mbata na majoya Ni majina nane: tunda langu moja: Kila mtu huchuma: kwa maonji yake. Chakula, cha kunywa: apendavyo yeye. Faida ingine: sijasema bado, Nisaburi tena usivunje moyo. 5. Ijapo kungine: naliwa na mwezi Pia kwa nasibu, kuwa zimwi nazi, Makumbi usumba: hufaa kwa mengi; Hata na kifuu: cha kuteka maji Kizio cha nazi: kombe la kunywea. Sisangae, Bwana, bado sijakoma. 6. Na tui la nazi, bin Adam hufyonza Akiisha kunguta: huweka machicha Kisha pata mbata: huwapa vinyama Vifae kunona: huleta faida. Uwongo sisemi, sicheki dhihaka Sifa yangu mnazi nani atasema? 7. Na matawi yangu, hutumiwa pia. Bora fuadi uwe, ujue kusuka Ukuti ununu: na kifumuwale, Kuti la ukumba: kuti la upande, Kuti la kiungo: toka upongoo, Ufikiri sasa ukaone mambo. 8. Shambani tembea, kaone majengo Yao walimaji, vinyumba vidogo, Pasi mti na nyasi: mimi peke MNAZI, Nakifu kukinga: mvua jua kali, Sokoni enenda: pakacha taona, Ni chombo kizuri pakia matunda. 9. Hayo ni mafaa: na wangu uzuri, Ukiri, naomba: tazama matawi, Kwa pepo mwanana: vizuri hunepa Kama binti Fundi: mikono hupunga. Shingo langu refu: mikono ya mbinu, Umbo langu lote mapambo matupu. 18 10. Hilo ni jawabu: la maswali yako Nililojaribu: na kwa Mambo Leo Nasihi niseme: uniwie radhi. Ewe! Bwana Khamisi: idadi ya miti Uliyohasibu: imepungukiwa Mimi peke Mnazi naweza kushinda. Shairi hili (isipokuwa kwa mistari 6 hivi yenye mizani 13) linao urari wa mizani 12, iliyogawanyika nusu kwa nusu, mizani 6 kila kipande. Ingawa tunakuta hapa na pale upo upatanifu wa vina vya mwisho katika mistari miwili, lakini upatanifu huo umetokea kwa nasibu tu. Katika shairi hili mtunzi, badala ya kuongea yeye mwenyewe na Bwana Khamisi, ameupa mnazi nafsi ya utu; na mnazi umeongea ana kwa ana na Bwana Khamisi kueleza sifa zake. Mbinu hii imelifanya jibu la mtunzi liwe na mvuto wa pekee - mvuto am- bao pengine usingepatikana iwapo Bwana Pacha engeongea ana kwa ana na Bwana Khamis juu ya sifa za mnazi. Bwana Pacha si mtunzi pekee wa kiwango cha juu aliyediriki kutunga ushairi guni. Shaaban Robert, yule "Simba wa Uswahilini, alitunga ushairi huu pia. Ubeti wa kwanza wa shairi lake "Muombwa" umekaa hivi Muombwa ni wewe Mungu Na jamii ya umati, Miili itie nguvu Na heri katika nchi, Astawi kila mtu Zitakate na nafsi. Na katika shairi lake "Nimeambiwa" ubeti wa kwanza una mpangilio huu: Habari nimeambiwa Tanganyika yastawi, Habari hii ni njema nikikumbuka matendo, Na kazi walizofanya watu wenu wa zamani, Kwa bidii kubwa sana mpaka hili likawa. Matendo ya watu wetu, wanawake na waume, Katika kila taifa yanawanyanyua watu, Na nchi ikawa nzuri au kuwatupa chini. 19 Mfano mwingine wa shairi guni lililotungwa na Shaaban Robert ni "Mtu Mwema", na ubeti wake wa kwanza uko hivi: Mtu ambaye ni mwema japokuwa hana dini, Awe kafiri mkubwa wa sala na wa ibada, Lakini huonekana hadhuru mtu mwingine, Na mwanawe hamdhuru au mwana wa mwenziwe, Mwana ambaye si wake kinuni hatamponda, Kisha akaoe mke kusudi azae mwana! Wema ni kama johari tena ni nuru ya mtu. Katika mifano hii ya beti za mashairi ya Shaaban Robert, tunaona kuwa ijapo yanafuata urari wa mizani lakini hayakufuata utaratibu wa vina. Na mifano hii inaelekea kutangua, au kurekebisha, ufafanuzi wa Shaaban Robert juu ya ushairi. Katika hotuba yake ya mwaka 1958, anasema: Ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi, na tenzi... Kina ni mlingano wa sauti za herufi... Mifano hiyo hapo juu inatuonyesha kuwa mashairi haya si sanaa ya vina hata kidogo. Tukifuata ufafanuzi wa Amri Abedi, ni mashairi guni. Tukifuata ufafanuzi wa Kandoro, labda si guni kwa sababu watunzi wameyatunga hivyo kwa kukusudia, si kwa kushindwa. Amri Abedi, alipokuwa akiandika kitabu chake Sheria za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri, alitambua kuwa mashairi guni yapo ila hakuyashughulikia kwa kuwa "hayatiliwi nguvu na sio maarufu". Ndiyo maana Juliasi Kaizari kilipochapishwa na Lyndon Harries akarukia na kusema kuwa mtindo wa taf- siri umefuata ushairi guniwa Kizungu, Amri Abedi alikanusha dai hilo kwa kusema: Ajabu ni kwamba hivi karibuni tu Rev. Lyndon Harries alitamani sana ionekane kuwa baadhi ya mashairi ya Kiswahili yana asili ya mashairi ya Kiingereza. Mheshimiwa Baba wa Taifa alipotoa tafsiri ya Julius Caesar kwa ushairi wa guni au usio na vina Lyndon Harries alirukia kusema kuwa washairi wa Kiswahili hawana desturi ya kuandika 20 mashairi yasiyo na vina, na kwa kuwa Waingereza ndiyo wenye desturi hiyo basi kazi ya Baba wa Taifa asili yake ni ya Kiingereza! Ilimradi hawaoni raha kuona cho chote kina asili ya Kiafrika! Kikifanana na Kiarabu basi Kiarabu ndiyo asili, kikifanana na Kiingereza basi Kiingereza ndiyo asili! Je, Kiswahili chenyewe hakiwezi kuwa na fani ambazo asili yao ni Kiswahili chenyewe? Kweli, bila kusahau kuwa tamthiliya inayozungumziwa ina asili ya Kiingereza, Kiswahili kinazo fani ambazo asili yake ni Kiswahili chenyewe, na miongoni mwa hizo ni ushairi guni na ushairi wa mtiririko. Maneno hayo ya Sheikh yangefaa kuam- biwa wanajadi wanaoshikilia kuwa mtindo huu ni wa Kizungu. Kutokana na hayo tuliyokwisha sema, tunaona kuwa ushairi guni ni mtindo katika ushairi-andishi wa Kiswahili ambao umekwisha kukubalika. Ingawa mwanzoni ulihusishwa na 'dosari', lakini katika miaka ya 1960 ulikuwa unatam- buliwa kuwa ni mtindo wenye hadhi kamili katika ushairi wa Kiswahili. Ndiyo maana Shaaban Robert hakuhofu "kujivun- jia hishima" kwa kuandika ushairi guni, kama ambavyo Bwana Pacha, katika mwaka 1928, hakuingiwa hata na fikira ya kujivunjia hishima" mbele ya malenga wenzake. Sasa basi ushairi huu "mpya" tunaweza kuuita "ushairi guni"? Jibu la swali hili litategemea mtazamo wa mtu kuhusu ushairi guni. Iwapo tutashikilia rai ya Farouk Topan, kwamba "uguni" ni tokeo la kushindwa kufuata kanuni za vina na urari wa mizani, tutasema kuwa mtindo huu siyo guni. Iwapo tutashikilia dhana ya Amri Abedi kuwa mashairi guni ni yale yasiyo na vina tu, bali yana mizani (kama mifano ya shairi la Pacha na mashairi ya Shaaban Robert inavyoonyesha), vile vile tutahitimisha kuwa mashairi haya siyo guni kwa kuwa siyo lazima yawe na urari wa mizani. Lakini iwapo tuna dhana ya "uguni" ambayo ni pana zaidi, ishikiliayo kuwa guni ni shairi lisilofuata kanuni za urari wa vina na mizani, basi mashairi haya tutayaita mashairi guni. Kwa mujibu wa mtazamo huu ushairi wa kitamthiliya tuukutao kwenye kitabu cha F. Nkwera Johari Ndogo na J.K. Nyerere (Mfasiri) Juliasi Kaizari ni ushairi guni; na pia ushairi wa kimasimulizi wa E. Hussein katika kitabu chake, Jogoo Kijijini, tutauita ushairi 21 guni uliochangamana na ushairi wenye kufuata kanuni za vina na urari wa mizani. Yamkini sasa tumefika mahali ambapo inabidi tuliingilie suala lenyewe la msingi: Ushairi ni nini? USHAIRI NI NINI? Hadi hapa tumekwishakuona kuwa ushairi wa Kiswahili si sanaa ya vina kama Shaaban Robert alivyotuambia; na wala vina na urari wa mizani siyo roho au uti wa mgongo wa ushairi wa Kiswahili kama Abdilatif, Mayoka na wanajadi wengine wanavyohubiri. Kwa hakika, mojawapo ya sababu ya wanajadi kuamini kuwa shairi lazima liwe na umbo maalum, na kuwa umbo hilo lazima litawaliwe na vina na urari wa mizani, ni kuwa dhana yao ya ushairi imetawaliwa na utaratibu wa kimaandishi. Hebu tulidadisi jambo hili zaidi. Ni rahisi kuthibitisha kuwa umbo la shairi la vina na mizani ni la kimaandishi, kwani karibu watu wote hapa kwetu hulitambua shairi kama linavyoonekana kwenye ukurasa wa karatasi (uwe ukurasa wa Uhuru, au wa Mzalendo au wa diwani yoyote ya mashairi). Kwa mujibu wa mtazamo huu, in- sha ni insha kwa vile huonekana imeandikwa kwa njia ya mjazo; na shairi ni shairi kwa vile laonekana lina vina na urari wa mizani. Hebu tuangalie andiko hili hapa chini: Pasipo na mwanamke dunia ingekuwaje? Mwanamme peke yake sijui angeishije! Maisha yetu ya kwanza yangekosa msaada; ya kati yakawa giza kwa furaha kuwa shida; na ya mwisho yangekuwa ni ghali kwa pesa moja: ingekuwa si dunia kwa uchache wa faraja. Andiko hili lililoandikwa kwa njia ya mjazo, bila shaka laonekana kuwa nathari. Lakini andiko hilo hilo tukigeuza umbo lake, "dhana" ya watu wengi juu ya hulka yake itageuka pia: Pasipo na mwanamke dunia ingekuwaje? Mwanamme peke yake sijui angeishije! Maisha yetu ya kwanza yangekosa msaada; Ya kati yakawa giza kwa furaha kuwa shida; 22 Na ya mwisho yangekuwa ni ghali kwa pesa moja: Ingekuwa si dunia kwa uchache wa faraja. Umbo hilo haliwakanganyi watu wengi: waliangaliapo mara moja hurukia kusema kuwa ni shairi, na wakiulizwa kwa nini hujibu kuwa andiko lina vina, urari wa mizani, n.k. Tuchukue andiko jingine lifuatalo: Wakadha namshukuru Mungu Kwa ajili ya sahibu yangu Mtunzi na kungwi wa mizungu Mathias Mnyampala Mfadhili na mwenye jamala Mashuhuri kwa mashairi ya muwala Na uandishi wa makala Ambaye ameniomba niandike hii dibaji Asaa iwafariji wasomaji Ambao sanaa hii wanaitaraji Niwabainishie yaliyo muhimu Kuhusu Kiswahili na utungaji Na kubatilisha riwaya za mafukala. Katika andiko hili tunaona upatanifu wa aina fulani wa vina vya 'ngu', 'la', na 'ji', ni 'mu' tu ambayo haina kina chenziye. Na si ajabu wapo watu ambao wanaweza kuliita andiko hili ubeti wa shairi lenye dosari au guni, kwa sababu wameona upatanifu fulani katika umbo lake. Kumbe andiko lenyewe katika uasili wake lilikuwa katika umbo la mjazo kama ifuatavyo: Wakadha namshukuru Mungu kwa ajili ya sahibu yangu, mtunzi na kungwi wa mizungu, Mathias Mnyampala, mfadhili na mwenye jamala, mashuhuri kwa mashairi ya muwala na uandishi wa makala, ambaye aliniomba niandike hii dibaji asaa iwafariji wasomaji ambao sanaa hii wanaitaraji, niwabainishie yaliyo muhimu kuhusu Kiswahili na utungaji, na kubatilisha riwaya za mafukala. Kutokana na hayo yaliyokwishasemwa, tunaona kuwa "ana ya ushairi" ya wanajadi imefinywa kwenye "umbo maalum lenye utaratibu wa vina na urari wa mizani", ambayo 23 kwa kweli ni dhana ya kimaandishi. Na nathari kwao ni an- diko lolote ambalo halina utaratibu huo. Wanayaangalia matumizi ya lugha katika tabaka mbili zisizoingiliana: matumizi ya kishairi na yale ya kinathari. Mtazamo huu kuhusu lugha umepotoka sana, na hapo baadaye tutaonyesha upotofu wake. Kwa sasa inafaa tulikabili suala la ushairi ni nini. Iwapo "umbo" lionekanalo kwenye karatasi haliwezi kutiwa maanami katika ufafanuzi wowote thabiti wa ushairi, basi ushairi ni nini? J.A. Ramadhani, katika makala yake juu ya ushairi, ameeleza kwa urefu na kwa undani maana na sifa za ushairi. Mambo mengi muhimu ameyataja. Anatuambia kwamba: (1) Ushairi huanza na hisi au mchomo unaosababishwa na mazingira; (2) Hisi hizo huwasilishwa kwa msomaji kwa njia ya lugha teule ya kitamathali; (3) Hisi hizo lazima ziambatane na mawazo na mtazamo wa fikira; (4) Hali ya kishairi inahusiana kidogo na hali ya kindoto au tabia ya kuona yasiyoonekana na kuwania yasiyowezekana; (5) Ushairi umefungamana na ubuni, na kwa hiyo hauwezi kuwekewa sheria zisizobadilika, na kwamba kuogopa kubuni kunadumaza maendeleo ya ushairi wa Kiswahili; (6) Uwezo wa kubuni wa mshairi umetoka kwa Mungu am- baye ndiye mfalme wa sanaa zote. (7) Shairi ni muungano wa fani na yaliyomo (maudhui). Kimsingi, ufafanuzi huo wa ushairi hautofautiani sana na ufafanuzi alioutoa Kezilahabi. Anatuambia kwamba: Ushairi ni tukio, hali au wazo ambalo limeonyeshwa kwetu kutokana na upangaji mzuri wa maneno fasaha yenye mizani kwa ufupi ili kuonyesha ukweli fulani wa maisha. Fafanuzi hizi mbili zinarekebisha ile fikira ya wanajadi kwamba ushairi lazima uwe na urari wa mizani na vina. Hata hivyo, fafanuzi hizi zina upungufu wake. Upungufu wa maelezo ya Ramadhan umo hasa katika imani yake kuwa uwezo wa kishairi unatoka kwa Mungu. Hapa sipo mahali pa kujadili imani ya kidini ya Ramadhan 24 juu ya uwezo wa kishairi; suala hili ni kubwa na pengine linahitaji makala ya pekee. Inatosha tu tukisema kuwa ni kawaida ya falsafa za kidhanifu kumuweka Mungu kuwa chimbuko la mema aliyo nayo mtu; na kumuweka shetani kuwa chimbuko la mabaya yote. Upungufu wa kauli ya Kezilahabi hasa umo katika fungu la maneno "ukweli fulani wa maisha". Je, ni kweli kuwa ushairi lazima ueleze ukweli fulani wa maisha, na siyo uongo? Hali halisi inatueleza kuwa wapo washairi wasemao ukweli fulani kuhusu maisha, na wapo wengine wasemao uwongo, na pia mshairi mmoja anaweza kusema ukweli katika shairi moja na uwongo katika shairi jingine. Fikra hii ni potofa kama ile isemayo kuwa mshairi ni chemchemu ya hekima. Jambo ambalo halikutiwa maanani katika fafanuzi hizo linahusu dhima ya fasihi na ushairi kama vyombo vya kuburudisha na kustarehesha watu. Ushairi hauelezi mawazo tu kama kemia au fizikia. Ushairi lazima uguse hisi, lazima umsisimue yule anayeusema, kuusoma au kuuimba na yule ausikilizae. Shairi lisilogusa hisi ni kavu na butu, na hata kama limesarifiwa katika vina na urari wa mizani, shairi hilo litaishia katika kuhibiri tu. Na fasihi ikisha hubiri mahubiri makavumakavu kama kasisi mimbarini, bila mvuto wowote wa kifasihi, itakuwa imeshindwa kugusa pale ambapo inapaswa kugusa - hisi za watu. Kwa hiyo basi ufafanuzi thabiti wa ushairi lazima uzingatie uwezo wake wa kugusa hisi za watu. Kutokana na hayo tuliyokwisha sema, tunaweza kutoa ufafanuzi wa ushairi ambao unazingatia yale yaliyokwisha semwa na hao hapo jua, pamoja na dhima ya ushairi ya kugusa moso au hisi. Nao ni huu: Ushairi ni sanaa inayopam- banuliwa kwa mpangilio maalum wa maneno fasaha na yenye muwala, kwa lugha ya mkato, picha au sitiari au ishara, katika usemi, maandishi, au mahadhi ya wimbo, ili kueleza wazo au mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisi fulani, kuhusu maisha au mazingira ya binadamu, kwa njia inayogusa moyo. Hapa lazima tuseme kuwa, ingawa ushairi wa aina yoyote unaweza kuimbwa, lakini siyo kila kiimbwacho kitaitwa ushairi. Ushairi ni sanaa ya lugha, na usanaa wake uko katika "mpangilio maalum wa maneno fasaha yenye muwala, kwa lugha ya mkato... kwa njia ya kugusa moyo", siyo katika uim- baji, unaweza kuuongezea (au hata kuupunguzia!) mguso. 25 Kwa mujibu wa maelezo haya, uimbaji wa hesabu au aya kutoka kwenye kitabu cha siasa si ushairi. Ufafanuzi huo wa ushairi unazingatia halka ya ushairi usiofuata urari wa vina na mizani na ule unaofuata urari huo; ule ulio katika fasihi simulizi na ule ulio katika fasihi andishi. Jambo moja linalojitokeza ni kuwa ushairi ni lugha katika hali ya matumizi maalum; na matumizi maalum haya ni matumizi ya kisanaa ya vipengele vya lugha. Hapa chini tutajadili kwa ufupi baadhi ya vipengele muhimu vinavyoupambanua ushairi. VIPENGELE VYA USHAIRI Washairi wa jadi wanadai kuwa "vina na mizani ndio uti wa mgongo wa ushairi." Dai hili ni batili kifasihi, kwani linageuza kipengele kimoja kidogo cha kisanaa kuwa ndicho msingi wa sanaa yenyewe. John Ramadhani amezieleza sifa za ushairi kwa urefu na vizuri zaidi. Yeye ametaja mambo yafuatayo yaliyo mahimu: 1) Katika ushairi vitu hupewa nafsi na utu; 2) Picha ni sifa muhimu ya ushairi; 3) Ushairi huweza kuwa na mpangilio wa maneno usio wa kawaida; 4) Ushairi una ridhimu, mlingano wa sauti na mapigo; 5) Shairi ni lazima lionyeshe sifa ya kiumbaji, lisiwe ni nakala ya shairi jingine. Yote haya ni sawa, ila sisi tutajaribu kuyafafanua zaidi na kuongezea sifa zingine ambazo hazikutajwa. Suala hili tutalijadili kwa kufuata vichwa hivi: 1) Mpangilio wa maneno 2) Picha 3) Tamathali za usemi 4) Takriri na ridhimu 5) Hisia za kishairi 6) Fani na maudhui Mpangilio wa maneno Watu wengi wameichukulia kuwa kweli isiyopingika kuwa mpangilio wa maneno (mfuatano wa vipashio vya sentensi) katika ushairi ni tofauti na ule ulio katika nathari. Mpangilio wa maneno hufuata kanuni za miundo inayowezekana katika 26 lugha fulani. Tukichukua Kiswahili, kwa mfano, sentensi iliyozoewa sana ni ile yenye muundo huu: Kiima - Kitenzi - changizo... Nomino - kimilikishi - kitenzi - kielezi... Katika Kiswahili tunaweza kusema: Baba hujua kulima Mama hujua kusaga Mimi sijui chochote Baba yangu anajua kulima kwa plau Hii ni miundo ya kawaida ambayo imezoewa sana na wasemaji wa Kiswahili. Lakini, mzungumzaji anaweza kuipangua miundo hiyo, na kutumia miundo isiyo ya kawaida sana, kwa madhumuni ya kuleta msisitizo wa jambo fulani: Kulima baba hujua Kusaga mama hujua Chochote mimi sijui... Jambo la kusisitiza hapa ni kuwa mtu yeyote, mradi awe ni mzungumzaji wa lugha fulani, anaweza kutunga muundo wa kawaida au usio wa kawaida sana (pengine bila yeye kujua). Mzungumza lugha anao uhuru wa kutamba katika uwanja wa lugha yake ili aweze kueleza hisia na mawazo yake. Jinsi atakavyopanga maneno katika sentensi itategemea ujuzi na ustadi na uzoefu wake katika jambo hili. Je, mshairi anautumiaje uhuru huu wa kutunga miundo iliyo ya kawaida sana, na ile isiyo ya kawaida sana? Jambo la kusisitiza hapa ni kuwa mshairi si mtu wa pekee katika ujuzi wa lugha aitumiayo kutungia mashairi yake. Jambo tuwezalo kulisema pasipo wasiwasi wowote kuhusu tofauti baina ya mshairi na mtu wa kawaida ni hili: mshairi anao uzoefu katika kutunga mashairi, lakini mtu wa kawaida hana uzoefu huo. Uzoefu huu katika sanaa hii humwezesha mshairi kuitumia miundo ya lugha hiyo kutimilizia malengo yake ya kishairi. Uhuru wa mshairi wa kuchagua muundo fulani na kuacha muundo mwingine, kupanga vipengele fulani kwa njia fulani na kuacha kuvipanga kwa njia nyingine, ni uhuru unaotawaliwa na kanuni za sanaa yake, uwezo wake wa kuvipanga vipengele hivyo ili vilete athari iliyokusudiwa hutegemea uzoefu wake, ubingwa wake, na hali aliyo nayo wakati wa kutunga shairi lake. Katika ushairi wa Kiswahili, mbinu ya upangaji wa vipengele vya sentensi kwa njia isiyo ya kawaida hutumika 27 sana. Utakuta washairi wanasema: mzuri msichana, wangu mke, n.k. badala ya msichana mzuri, mke wangu. Miundo mingine ni kama ile tuliyoitoa mfano hapo juu (kulima baba ajua n.k.). Ipo miundo mingine isiyotumika sana katika mazungumzo ya kawaida inayotumiwa na washairi. Mpangilio huu usio wa kawaida huvuta udadisi kuliko ligha ya kawaida, na hutumika katika kusisitiza vipengele fulani vya hisi au wazo la mshairi. Lakini shairi siyo lazima liwe na mpangilio wa maneno usio wa kawaida ili lipendeze. Shairi linaweza kuwa na mpangilio wa kawaida tu, na athari ya mguso ikaletwa na vipengele vingine kama vile picha, takriri, n.k. Kwa hiyo, ingawa mpangilio tulioujadili unaweza kuwa alama mojawapo ya ushairi, lakini si lazima kila shairi lithibiti mpangilio huo. Picha Picha ni matumizi ya lugha yanayopambanuliwa na utenzi mzuri wa maneno, uangalifu na udhahiri wa maelezo wenye kuhusisha na kujumuisha dhana mbali mbali tofauti ndani ya dhana moja ili kuleta taswira na athari maalum katika mawazo ya msomaji (au msikilizaji). Kezilahabi ameeleza kuwa athari hiyo aipatayo msomaji au msikilizaji wa ushairi inaweza kuwa ni ya aina ya vionjo vyenye kuhusiana na milango ya fahamu ya kusikia, kuona, kunusa na kugusa. Kwa hiyo, kwa kutumia picha, mwandishi anaweza kumfanya msomaji wake asisimke, aogope, afurahike, avutike, akirihishwe, alie, anyamae au aghadhabike kwa kuathiriwa na picha zilizoteuliwa na kusanifiwa kwa ufundi. Ugumu wa kutunga mashairi ya mtiririko uko katika utenzi na upangaji wa picha na tamathali za usemi zenye kuoana na maudhui yaliyokusudiwa zisizotengua ridhimu ya shairi na zisizofanya lugha ya shairi ipoteze uasili wake. Wakati huo huo, shairi hili liwe na uwezo wa kindanindani wa kuvutia na kudumisha hamu ya msomaji au msikilizaji hadi mwisho. Katika ushairi wa fasihi-simulizi, hamu ya hadhira hudumishwa na uteuzi wa maneno, muziki (kama ala za muziki zinatumika), mazingira au sherehe inayoambatana na tungo hiyo, ushirikishaji wa hadhira kwa kutumia kibwagizo, makofi na vipengele vingine, na umuhimu wa kijamii au kihistoria wa yale yanayoelezwa. 28 Katika ushairi-andishi wenye vina na mizani, hamu ya msomaji zaidi hudumishwa na ulinganifu wake wa ridhimu na sauti unaotokana na vina na urari wa mizani. Mapigo ya shairi la aina hiyo hufuata mgawanyo wake katika vipande vyenye mizani sawa na shairi husomeka upesi upesi bila kuitumikisha sana akili ya msomaji. Kifani, vina na urari wa mizani katika ushairi-andishi hufanyakazi ya ala za muziki katika ushairi-simulizi. Ushairi wa mtiririko ni wa kiwango cha juu zaidi kwa sababu unakataa kupata uhai wake kutokana na mbwembwe za kijuujuu, mambo ya nje ambayo ni nyongeza muhimu juu ya ushairi, lakini si lazima yawe sehemu ya ushairi: vina na urari wa mizani. Ushairi huo unapata uhai wake na utamu wake kutokana na mfumo wake wa ndani ambao ni fungamano la matumizi mahususi ya lugha nzito, hisia nzito na maudhui ya kishairi. Mashairi haya yanamlazimisha msomaji atumie akili zaidi, ajihusishe zaidi kijaziba katika hisia za mtunzi, na atafakari zaidi, badala ya kumkokota kikuku kwa utamu wa kijuujuu wa muziki wa vina na urari wa mizani. Mtiririko ni mashairi yaliyokusudiwa yasomwe na watu wazima, mengi hayafai kusomwa na watoto wa shule za msingi kwa sababu uwezo wao wa kuichambua fasihi bado ni mdogo. Hivyo hapana shaka kuwa kwa miaka mingi ijayo mashairi yenye vina na mizani yataendelea kupendwa zaidi na watoto wadogo, mradi lugha yake isiwe ngumu sana. Kwa ajili ya adhira hiyo, mashairi ya aina hiyo ni lazima na bora yaen- delee kutungwa. Bali kwa ajili ya watu wazima waliofikia kiwango fulani cha ufahamu wa fasihi, mashairi ya aina hiyo si lazima, ingawa si mwiko kuyatunga. Kila mshairi apewe uhuru wa kutumia fani inayofungamana vizuri zaidi na maudhui yake, uwezo wake, na pia hadhira aliyokusudia. Ingawa matumizi ya lugha huweza kuzindua hisi na maono fulani katika akili ya msomaji juu ya kile kinachozungumziwa, lakini ni muhimu kukumbuka kuwa uhusiano huo unaozinduliwa kati ya picha ya mawazoni na kitu halisi kinachozungumziwa (kinachochorwa) ni wa kinadharia, si wa kimaumbile au wa moja kwa moja. Hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya maana au umbile la kitu na uwakilishaji wa kitu hicho katika lugha - katika neno mofimu na fonimu. Kifasihi uhusiano tuupatao tunapotumia picha ni ule unaoumbwa na akili ya msomaji mwenyewe 29 inapozinduliwa na ustadi wa mshairi wa matumizi ya lugha na kunga nyingine za ushairi. Usanifu wa mashairi humfanya msomaji wake awe msanifu vile vile; mshairi hudokeza, msomaji hukamilisha; mshairi huumba, msomaji humalizia na kuhusisha kile kilichoumbwa na hali halisi anayoijua. Kwa hiyo msomaji wa mashairi si mpokeaji tu wa sanaa hiyo bali ni mpokeaji msanii vile vile. Hebu tuutazame mfano ufuatao unaotoka katika shairi la Shaaban Robert, "Mtu na Malaika". Mtu Na Malaika Neno lenye mzunguko, halipatikani mwisho, Wa huku hafiki huko, wala halina malisho. Halishibishi huchosha, njiaye ina uchovu, Na tabu isiyokwisha, wala hupati utuvu. Heri ya mtu ni kwenda, njia iliyonyooka, Na milima akapanda, apendako akafika. Mabondeni akashuka, mwituni akatumbua, Na mitoni akavuka, hata alikonuia. Na mzunguko wa dira, mwisho wake ni dirani, Hupati kupanda bara, na hushuki baharini. Tazama mashaka gani, njia ya dira si njia. Katika dondoo hii tunapewa picha tatu mahsusi. Picha ya kwanza ni neno linalozunguka... Mshairi anatuambia kuwa neno ambalo halifuati njia iliyonyooka 'neno lenye mzunguko" halifikii mwisho wake na halileti mradi uliokusudiwa "halina malisho". Hapa neno limefanywa kuwa kitu chenye uwezo wa kutembea, kuzunguka. Athari ya neno hilo kwa anayehusika ni kwamba halileti shibe wala utulivu, linachosha: "Halishibishi huchosha". Hapa tunapewa picha ya shibe, neno linapewa uwezo wa chakula - kitu yakini kinachoshikika na kinacholiwa. Bali mtu hatosheki na "chakula hicho" hatatui matatizo yake iwapo njia anayotumia ni ya mzunguko, ya kulegalega, ya ugeugeu na woga. Picha ya pili tunayopewa ni ya mtu aendaye safari ngumu kwa ujasiri na moyo na dhati, akipanda milima na kushuka mabonde, akipenya misitu na kuvuka mito, hadi kufika kule anakokwenda. Huyu ni mtu asiyeogopa matatizo, anayeshikilia njia ngumu lakini nyoofu, alimradi anajua kuwa itamfikisha kwenye lengo lake. Ni mtu anayepambana na 30 matatizo badala ya kuyakimbia. Mtu wa aina hii ndiye hupata mafanikio. "Heri ya mtu ni kwenda, njia iliyonyooka". Picha ya tatu tunayopewa ni dira. Dira ni chombo kitumiwacho na mabaharia na wasafiri wengine kusahihisha majira yao ili wasipotee njia. Dira ni chombo cha mviringo na mshale wake aghalabu huzungukia pale pale ulipo, katu hautoki nje ya dira. Picha hii inasisitiza wazo la mwandishi kuwa njia yenye kuzunguka haiwezi kumfikisha mtu kwenye lengo lake. Mshale wa dira huzunguka daima lakini haufiki kokote. Picha hizi tatu kwa pamoja zinafaulu kutupa ujumbe wa mwandishi kuhusu maisha na namna ya kuyakabili: tuyakabili kwa juhudi na ujasiri na nia. Tuamue jambo na tulifanye bila kutetereka. Tusiogope vikwazo wala matatizo. Maisha ni mapambano. Kwa kutumia picha hizi tatu, mwandishi kafaulu kufikisha kwetu ujumbe wake wa kishairi. Maudhui yake ni ya kishairi, yanapatikana kwa kuzichambua na kuzifafanua picha alizozitumia. (Shairi hili lingeweza vile vile kufasiriwa kidini kama alivyofanya J. Ramadhani katika makala yake "Ustadi wa Shaaban Robert Mshairi" Mulika No. 7, uk. 46-48) Mpangilio wa lugha Katika dondoo tulilolichunguza picha imejitokeza kwa njia ya sitiari (kitu kimoja kuwa badala ya kitu kingine kilicho tofauti: k.m. "msitu" badala ya "matatizo", "dira" badala ya "tabia ya kukwepa matatizo" n.k.) na mpangilio wa lugha na mawazo. Dhana tatu zinazotofautiana - neno linalozunguka mtu anayesafiri kupitia msituni na baharini, n.k. na dira inayozungukia mahali pale pale ilipo zinaleta wazo moja mahsusi. Zote zimechangamana ili kujenga dhana moja. Umoja wa wazo linalozungumziwa unaimarishwa pia na mfungamano wa ubeti mzima - pana mfululizo wa fikra na hisi tangu mstari wa kwanza hadi wa mwisho, kifungu kizima ni ubeti mmoja, hakuna mgawanyo wa beti za mistari miwili miwili au minne minne. Wazo linafululiza bila kusita au kukatishwa hadi mwisho kama vile ambavyo maudhui ya shairi lenyewe yanavyotuhimiza kufululiza katika njia moja bila kutetereka hadi mwisho. Muundo wa shairi umeoana na maudhui yake. 31 Mpangilio wa lugha - herufi, silabi, mofimu hadi maneno na sentensi ni sharti uoane na maudhui. Washairi hutumia kunga mbali mbali za kisauti na kimpangilio ili kuleta hisia fulani. Baadhi ya kunga hizo ni onomatopea, mizani, vina, asonansi (mlingano wa sauti za irabu), konsonansi (mlingano wa sauti za konsonanti) takriri-konsonanti (marudio ya kon- sonanti) takriri-vina, n.k. Vipengele vyote hivi, isipokuwa onomatopea, ni aina ya takriri na tutavijadili chini ya mada ya takriri. Onomatopea Onomatopea ni mwigo wa sauti. Hii ni kunga inayotumiwa na washairi ili kutoa picha au dhana ya kile kinachowakilishwa au kupambanuliwa na sauti hizo. Kwa mfano tukisema: "Maji yalimwagika mwa" neno mwa ni onomatopea, linawakilisha sauti au kishindo cha maji yanayomwagika. Baadhi ya onomatopea ambazo zimekwisha kuwa sehemu ya msamiati wa kawaida wa Kiswahili ni: pikipiki, bombom, mbwa, yowe, ngurumo, bunduki, gumia, kata, n.k. Katika shairi lake la "Cheka kwa Furaha" Shaaban Robert ametumia onomatopea ili kuleta ile dhana ya kucheka: Dhiki ni kama mzaha, asiyecheka ni nani? Haya cheka ha! ha! ha! ndiyo ada duniani. Basi cheka kwa! kwa! kwa! kwa! usafike moyo wako Pamoja na malaika, wema mbinguni waliko; Maneno yaliyoandikwa kwa italiki ni onomatopea, yanatoa picha ya kusikika ya sauti ya mtu anayecheka. Huu ni mpangilio maalum wa sauti ili kutoa picha ya kusikika ya dhana inayozungumziwa. TAMATHALI Tamathali za usemi ni vifananisho au viwakilisho vya dhana fulani kwa dhana nyingine tofauti au zinazofanana. Ni usemi wenye kupanua, kupuuza au kubadilisha maana za dhahiri au za kawaida za maneno ili kuleta maana maalumu ya kishairi iliyokusudiwa na mtunzi. Tamathali nzuri hupanua, huyakinisha na huipa uhai na uhalisi zaidi dhana 32 inayoelezwa, huburudisha na kuzindua akili ya msomaji au msikilizaji wa shairi, na huacha athari ya kudumu katika hisi na mawazo yake. Tamathali zinazotumika zaidi katika ushairi ni tashbiha, meonymy, uhaishaji (personification) (Tashihisi) synecdoche, baalagha, kejeli na sitiari. Tashbiha Hi ni tamathali ya ufananisho au mlinganisho wa vitu viwili au zaidi. Katika tashbiha, kama ilivyo katika sitiari, huwa kuna vitu vitatu vinavyofananishwa ambavyo wataalamu wameviita kizungumzwa, kifananishi na kiungo. Kifananishi ndiyo usemi wenye kuzingatia maana-dhahnia, ni chombo kinachobeba mlinganisho. Kizungumzwa ndicho kitu halisi am- bacho kinazungumziwa na kifananishi kwa mafumbo. Kiungo ni zile sifa ambazo zinapatikana katika kizungumziwa na kifananishi na hivyo kuhusisha vitu hivyo viwili. Katika tash- biha, kizungumzwa na kifananishi huhusishwa bila mafumbo kwa uwazi, moja kwa moja, kwa kutumia maneno fulani ya ulinganisho, km. "kama" "fanana na", "mithali ya" n.k. Katika tashbiha hakuna maana dhahnia, bali kuna ulinganishaji wa vitu viwili vilivyo bayana. Angalia mfano ufutao: Kweli ni sawa na radi inapotoa kauli... Kweli kinywani ikiwa sawa na Mto wa Nili Kweli kama msumeno hukereza sawa kweli. Katika dondoo hilo maneno yaliyochapwa kwa italiki yanaunganisha vitu viwili vinavyotofautiana na kuvifananisha. Mstari wa kwanza "kweli" inalinganishwa na radi, mstari wa pili inalinganishwa na "Mto Nili" na mstari wa tatu inalinganishwa na "msumeno". Tashihisi (uhaishaji) Washairi mara nyingine huweza kukipa kitu kisichokuwa na uhai sifa za kitu chenye uhai, hasa za binadamu. Matumizi ya lugha kwa njia hiyo ndiyo huitwa uhaishaji au tashihisi. Kisanaa maelezo ya kitashihisi huwa na upekee unaomwingia 33 msomaji akilini haraka, kwani si jambo la kawaida, mathalan, kuona mti "ukimpungia mtu mkono" au nyumba "ikimkodolea macho" mgeni. Tashihisi, basi, ni aina ya sitiari na kisanaa kazi yake ni kama ile ya sitiari, japo kwa kiwango cha kidhahnia zaidi. Mfano wa matumizi ya tashihisi: Kimya hakineni jambo, si kimya chawatazama... Kimya chaja zua mambo, pasiwe mwenye kusema... Kimya kipimeni sana, msione kutosema Kimya hakichi kunena, kitakapo kusimama Kimya chaja watukana kizuwe yaliyozama... Katika dondoo hili, "kimya" (ambayo ni nomino-dhahnia) kimepewa sifa za binadamu, kinaweza kunena, kutazama, kuzua mambo, kusimama nakutukana. Katika shairi lake la "Fedha", Shaaban Robert anaipa fedha sifa za binadamu: Fedha huita wazuri, Wakaitika labeka, Wakenda bila hiari, Mahali wasikotaka. Mfano mzuri wa matumizi ya tashihisi kishairi tunauona katika shairi la Bwana Rajabu M. Kianda (Selukindo) liit- walo "Jembe". Jembe wangu nifariji, nami nikupe uzima, Jembe wewe ndiye jaji, twakuenzi zote dhima, Jembe wewe ni mpaji, wa baba na kina mama, Jembe ndiwe mtawala, tangu enzi za wahenga. Jembe wewe msifika, utuonee huruma, Jembe shamba tukifyeka, njoo ufanye kulima, Jembe njoo pasi shaka, ukija lete mtama, Jembe ndiwe mtawala, tangu enzi za wahenga. Jembe kwetu ukifika, tunapata usalama, Jembe kote umeshika, ukweli tunausema, Jembe yakija masika, nawe fika nyuma nyuma, Jembe ndiwe mtawala, tangu enzi za wahenga. 34 Jembe jua likitoka, nawe usife mtima, Jembe usije kuchoka, au kupatwa na homa, Fanya bila kukongoka, fanya usirudi nyuma, Jembe ndiwe mtawala, tangu enzi za wahenga. Mola akupe hakika, usende kamwe mrama, Nenda upate kufika, kama tunavyokutuma, Sote huko tukifika, tutaishi kwa neema, Jembe ndiwe mtawala, tangu enzi za wahenga. Katika shairi hili "Jembe" limepewa sifa za binadamu: ni mfariji, jaji, mpaji, mtawala, mkulima; linaweza kusafiri, kubeba mtama, kufa mtima, na kupatwa na homa. Ingawa tunajua wazi kuwa jembe ni kifaa tu kinachotengenezwa na kutumiwa na binadamu, kuwa halina hata mojawapo ya sifa hizo, lakini tunaposoma shairi tunaathirika na kushawishika kuwa yasemwayo ni kweli na sana maana. Tunalikubali kwa sababu tunaelewa kuwa tukisomacho ni kiwakilishi tu, ni ishara ya dhana nyingine nzito na muhimu: Umuhimu wa kilimo katika uchumi na uhai wetu, na katika historia wa binadamu. Mtunzi katumia uwezo wake wa kisanaa kuumba picha hii ya jembe, nasi wasomaji inatubidi tutumie uwezo wetu wa kuumba na kutafsiri ishara ili tulielewe na kulifurahia shairi hili. Matumizi ya tashihisi yanaliongezea shairi hili uzito wa kimaana, na yanatushirikisha sisi wasomaji katika ufumbuzi wa "kitendawili" chake. Hivyo shairi hili linatuathiri sana kwa kuwa linatushirikisha akili zetu katika kutafakari vipengele vyake na maana yake. Karibu. Jambo! Habari yako? Hujambo? Sijambo! Habari za safari? Nimefurahi kukutana na wewe. Jambo. Hamjambo. Hatujambo. jambo. karibu. habari yako? hujambo? sijambo. habari za safari? nimefurahi kukutana na wewe. habari? |
:: Command execute :: | |
--[ c99shell v. 2.0 [PHP 7 Update] [25.02.2019] maintained by KaizenLouie | C99Shell Github | Generation time: 0.0383 ]-- |